Isaya 44

Isaya 44

Baraka za Mungu kwa Israeli

1Lakini sikia sasa, Ee Yakobo, mtumishi wangu; na Israeli, niliyekuchagua;[#Isa 41:8; Yer 30:10]

2BWANA, aliyekufanya, na kukuumba toka tumboni, yeye atakayekusaidia, asema hivi; Usiogope, Ee Yakobo, mtumishi wangu; na wewe, Yeshuruni, niliyekuchagua.[#Kum 32:15]

3Kwa maana nitamimina maji juu yake aliye na kiu, na vijito vya maji juu ya mahali pakavu; nitamwaga roho yangu juu ya wazao wako, na baraka yangu juu yao utakaowazaa;[#Mal 3:10; Yn 7:38]

4nao watachipua kama nyasi, kama mierebi kandokando mwa vijito.

5Mmoja atasema, Mimi ni wa BWANA; na mwingine atajiita kwa jina la Yakobo; na mwingine ataandika juu ya mkono wake, Kwa BWANA, na kujiita kwa jina la Israeli.[#Kut 13:9; Neh 9:38]

6BWANA, Mfalme wa Israeli, Mkombozi wako, BWANA wa majeshi, asema hivi; Mimi ni wa kwanza, na mimi ni wa mwisho; zaidi yangu mimi hapana Mungu.[#Isa 48:12; 43:1; 41:4; Ufu 1:8,17; 2:8; 22:13]

7Naye ni nani kama mimi atakayeita, na kuyahubiri haya, na kunitengenezea, tangu nilipowaweka watu wa kale? Na mambo yanayokuja na yatakayotokea, wayatangaze.

8Msiogope wala msifanye hofu; je! Sikukuambia haya zamani na kuyatangaza? Na ninyi ni mashahidi wangu. Je! Yuko Mungu zaidi yangu mimi? Hakika hapana Mwamba; mimi sijui mwingine.[#Kum 4:35; 1 Sam 2:2; 2 Sam 22:32]

Upumbavu wa kuabudu sanamu

9Wachongao sanamu, wote ni ubatili; wala mambo yao yawapendezayo hayatafaa kitu; wala mashahidi wao wenyewe hawaoni, wala hawajui; ili watahayarike.[#Isa 41:24; 42:17-20; Kum 4:28; Zab 115:4]

10Ni nani aliyejichongea mungu mmoja, au aliyesubu sanamu isiyofaa kitu?[#Yer 10:5; Hab 2:18]

11Tazama, wenziwe wote watatahayari; na mafundi, hao ni wanadamu; na wakusanyike pamoja, wakasimame; wataogopa na kutahayari pamoja.[#Zab 97:7; Isa 42:17]

12Mfua chuma hufanza shoka, hufanya kazi kwa makaa, huitengeneza sanamu kwa nyundo, huifanyiza kwa nguvu za mkono wake; naam, huona njaa, nguvu zake zikampungukia; asipokunywa maji huzimia.[#Isa 40:19]

13Seremala hunyosha uzi; huiandika kwa kalamu ya mate; huitengeneza kwa randa, huiandika kwa bikari, huifanza kwa mfano wa mwanadamu, sawasawa na uzuri wa mwanadamu, ili ikae nyumbani.

14Yeye hujikatia mierezi, hutwaa mtiriza, na mwaloni, hujichagulia mti mmoja katika miti ya msituni; hupanda mvinje, mvua ikausitawisha.

15Kisha utamfaa mwanadamu kwa kuni; hutwaa kipande, akaota moto; naam, huuwasha moto, akaoka mkate; naam, huufanya mungu, akauabudu; huifanya sanamu ya kuchonga, akaisujudia.

16Sehemu moja huiteketeza; kwa sehemu nyingine hula nyama; huoka chakula kiokwacho, akashiba; naam, huota moto, akasema, Aha, nimeota moto, nimeona moto;

17na kwa sehemu iliyobakia hufanya mungu, yaani, sanamu yake ya kuchonga; husujudu mbele yake akaiabudu, akaiomba, akasema, Uniokoe; maana wewe u mungu wangu.

18Hawajui wala hawafikiri; maana amewafumba macho, wasione, na mioyo yao, wasiweze kufahamu.[#Zab 81:12; Isa 45:20; Rum 11:8-10; 2 The 2:11]

19Wala hapana atiaye moyoni, wala hapana maarifa, wala fahamu kusema, Nimeteketeza sehemu motoni, naam, pia nimeoka mkate juu ya makaa yake; nimeoka nyama nikaila; nami, je! Kilichobaki nikifanye kuwa chukizo? Je! Nisujudie shina la mti?

20Hula majivu; moyo uliodanganyika umempotosha, asiweze kuiokoa nafsi yake, wala kusema, Je! Sio uongo mkononi mwangu?[#Hos 4:12; Rum 1:21; 2 The 2:11]

Israeli hujasahauliwa

21Kumbuka haya, Ee Yakobo; nawe Israeli, maana wewe u mtumishi wangu; nimekuumba; u mtumishi wangu; Ee Israeli, hutasahauliwa na mimi.

22Nimeyafuta makosa yako kama wingu zito, na dhambi zako kama wingu; unirudie; maana nimekukomboa.[#Isa 1:18; 43:25; 53:11,12; Yer 33:8; Mik 7:18,19; Kol 1:14; Isa 43:1; 1 Kor 6:20; 1 Pet 1:18,19]

23Imbeni, enyi mbingu, maana BWANA ametenda hayo;[#Zab 69:34; Isa 42:10; Ufu 18:20]

Pigeni kelele, enyi mabonde ya nchi;

Pazeni nyimbo, enyi milima;

Nawe, msitu, na kila mti ndani yake.

Maana BWANA amemkomboa Yakobo,

Naye atajitukuza katika Israeli.

24BWANA, mkombozi wako, yeye aliyekuumba tumboni, asema hivi; Mimi ni BWANA, nifanyaye vitu vyote; nizitandaye mbingu peke yangu; niienezaye nchi; ni nani aliye pamoja nami?[#Ayu 19:25; 9:8; Isa 43:1,14; 40:22; Zab 104:2]

25Nizitanguaye ishara za waongo, na kuwatia waganga wazimu; niwarudishaye nyuma wenye hekima, na kuyageuza maarifa yao kuwa ujinga;[#Yer 50:36; 1 Kor 1:20]

26nilithibitishaye neno la mtumishi wangu, na kuyafikiliza mashauri ya wajumbe wangu; niuambiaye Yerusalemu, Utakaliwa na watu, nayo miji ya Yuda, Itajengwa, nami nitapainua mahali pake palipobomoka;[#Zek 1:6; Mt 5:18]

27niviambiaye vilindi, Kauka, nami nitaikausha mito yako;[#Yer 50:38]

28nimwambiaye Koreshi, Mchungaji wangu, naye atayatenda mapenzi yangu; hata ataunena Yerusalemu, Utajengwa; na hilo hekalu, Msingi wako utawekwa.[#2 Nya 36:22,23; Ezr 1:2]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya