Isaya 5

Isaya 5

Wimbo wa shamba la mizabibu lisilozaa matunda

1Na nimwimbie mpenzi wangu wimbo wa mpenzi wangu kuhusu shamba lake la mizabibu.[#Mt 21:33; Mk 12:1; Lk 20:9; Zab 80:8]

Mpenzi wangu alikuwa na shamba la mizabibu,

Kilimani penye kuzaa sana;

2Akachimba handaki kulizunguka pande zote,[#Kum 32:6]

Akatoa mawe yake,

Akapanda ndani yake mzabibu ulio mzuri,

Akajenga mnara katikati yake,

Akachimba shinikizo ndani yake;

Akatumaini ya kuwa utazaa zabibu,

Nao ukazaa zabibumwitu.

3Na sasa, enyi wenyeji wa Yerusalemu, nanyi watu wa Yuda, amueni, nawasihi, kati ya mimi na shamba langu la mizabibu.[#Rum 3:4]

4Je! Ni kazi gani iliyohitajika kutendeka ndani ya shamba langu la mizabibu nisiyoitenda? Basi, nilipotumaini ya kuwa litazaa zabibu, mbona lilizaa zabibumwitu?

5Haya basi, sasa nitawaambieni nitakalolitenda shamba langu la mizabibu; nitaondoa ua wake, nalo litaliwa; nitabomoa ukuta wake, nalo litakanyagwa;

6nami nitaliharibu; wala halitapogolewa wala kulimwa, bali litamea mbigili na miiba; nami nitayaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake.

7Kwa maana shamba la mizabibu la BWANA wa majeshi ndilo nyumba ya Israeli, na watu wa Yuda ni mche wake wa kupendeza; akatumaini kuona hukumu ya haki, na kumbe! Aliona dhuluma; alitumaini kuona haki, na kumbe! Alisikia kilio.

Udhalimu wa kijamii washutumiwa

8Ole wao waongezao nyumba baada ya nyumba, na kuweka shamba karibu na shamba, hadi ikawa hapana nafasi tena, nanyi ikawa hamna budi kukaa peke yenu katikati ya nchi![#Mik 2:2]

9BWANA wa majeshi asema katika masikio yangu, Hakika majumba mengi yatakuwa ukiwa, naam, majumba makubwa, mazuri, yatakuwa hayana watu.

10Kwa maana shamba la mizabibu la eka kumi litatoa bathi moja tu, na homeri ya mbegu itatoa efa tu.[#Law 27:16]

11Ole wao waamkao asubuhi na mapema, wapate kufuata kileo; wakishinda sana hadi usiku wa manane mpaka mvinyo imewaka kama moto ndani yao![#Mit 23:29,30]

12Na kinubi, na zeze, na matari, na filimbi, na mvinyo, zote ziko katika karamu zao; lakini hawaiangalii kazi ya BWANA wala kuyafikiri matendo ya mikono yake.[#Amo 6:5; Ayu 34:27; Hos 4:11]

13Kwa sababu hiyo watu wangu wamechukuliwa mateka, kwa kukosa kuwa na maarifa; na watu wao wenye cheo wana njaa, na wengi wao waona kiu sana.[#Isa 1:3,7; Hos 4:6; Lk 19:44; Rum 1:28; 2 Pet 3:5]

14Kwa hiyo kuzimu kumeongeza tamaa yake, kumefunua kinywa chake bila kiasi; na utukufu wao, na wingi wao, na ghasia yao, naye pia afurahiye miongoni mwao, hushuka na kuingia humo.

15Na mtu mnyonge ainamishwa, na mtu mkubwa amedhilika, na macho yao walioinuka hunyenyekezwa,

16bali BWANA wa majeshi ametukuzwa katika hukumu, na Mungu aliye Mtakatifu ametakaswa katika haki.

17Ndipo wana-kondoo watakapojilisha kama walio katika malisho yao wenyewe, na mahali pao walionenepa, palipoachwa ukiwa, wageni watakula.

18Ole wao wavutao uovu kwa kamba za ubatili, na dhambi kama kwa kamba za gari!

19Wasema, Na afanye haraka, aihimize kazi yake, tupate kuiona; na likaribie shauri lake aliye Mtakatifu wa Israeli, tupate kuliona.[#Isa 66:5; Yer 17:5; Amo 5:18; 2 Pet 3:3]

20Ole wao wasemao kwamba uovu ni wema, na kwamba wema ni uovu; watiao giza badala ya nuru, na nuru badala ya giza; watiao uchungu badala ya utamu, na utamu badala ya uchungu!

21Ole wao walio na hekima katika macho yao wenyewe, na wenye busara katika fikira zao wenyewe!

22Ole wao walio hodari kunywa kileo chenye nguvu, na walio hodari wa kuchanganya vileo;

23wampao haki mwenye uovu, ili wapewe ijara, na kumwondolea mwenye haki haki yake!

Uvamizi wa kigeni watabiriwa

24Kwa hiyo kama vile muali wa moto uteketezavyo mabua makavu, na kama manyasi makavu yaangukavyo katika muali wa moto; kadhalika shina lao litakuwa kama ubovu, na ua lao litapeperushwa juu kama mavumbi; kwa sababu wameikataa sheria ya BWANA wa majeshi, na kulidharau neno lake aliye Mtakatifu wa Israeli.[#2 Fal 17:14; Lk 7:30; Yn 12:48]

25Kwa sababu hiyo hasira ya BWANA imewaka juu ya watu wake, naye amenyosha mkono wake juu yao; akawapiga, navyo vilima vilitetemeka, na mizoga yao ilikuwa kama takataka katika njia kuu. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa.

26Naye atawatolea ishara mataifa toka mbali,

Naye atawapigia miruzi tokea mwisho wa nchi;

Na tazama, watakuja mbio mbio upesi sana.

27Miongoni mwao hakuna achokaye wala kukwaa;

Hakuna asinziaye wala kulala usingizi;

Wala mshipi wa viuno vyao hautalegea.

Wala ukanda wa viatu vyao hautakatika;

28Mishale yao ni mikali, na pinde zao zote zimepindika;

Kwato za farasi wao zitahesabika kama gumegume;

Na gurudumu zao kama kisulisuli;

29Ngurumo yao itakuwa kama ya simba;

Watanguruma kama wanasimba;

Naam, watanguruma na kukamata mateka,

Na kuyachukua na kwenda zao salama,

Wala hakuna mtu atakayeokoa.

30Nao watanguruma juu yao siku hiyo

Kama ngurumo ya bahari;

Na mtu akiitazama nchi, ataona giza na dhiki

Nayo nuru imetiwa giza katika mawingu yake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya