Isaya 50

Isaya 50

1BWANA asema hivi, Iko wapi hati ya talaka ya mama yenu, ambayo kwa hiyo niliachana naye? Au nimewauza ninyi kwa nani katika watu wanaoniwia? Ninyi mliuzwa kwa sababu ya maovu yenu; tena mama yenu ameachwa kwa sababu ya makosa yenu.[#Kum 22:17; Hos 2:2; 2 Fal 4:1; Mt 18:25]

2Basi, nilipokuja, mbona hapakuwa na mtu? Nilipoita, mbona hapakuwa na mtu aliyenijibu? Je! Mkono wangu ni mfupi, hata nisiweze kukomboa? Au je! Mimi sina nguvu za kuponya? Tazama, kwa kukemea kwangu naikausha bahari, mito ya maji naifanya kuwa jangwa; samaki wao wanuka kwa sababu hapana maji, nao wafa kwa kiu.[#Mit 1:24; Yer 7:13; Isa 65:12; 59:1; Mwa 18:14; Hes 11:23]

3Mimi nazivika mbingu weusi, nami nafanya nguo ya magunia kuwa kifuniko chao.

Kuaibishwa na kuthibitishwa kwa mtumishi

4Bwana MUNGU amenipa ulimi wa hao wafundishwao, nipate kujua jinsi ya kumtegemeza kwa maneno yeye aliyechoka, huniamsha asubuhi baada ya asubuhi; huniamsha, sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao.[#Kut 4:11; Mt 7:29; Mk 6:7; Lk 4:22,32; Mt 11:28]

5Bwana MUNGU amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma.[#Mt 26:39; Flp 2:8; Ebr 10:5]

6Niliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang'oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate.[#Mt 26:67; 5:39; Omb 3:30; Mik 5:1; Mk 14:65]

7Maana Bwana MUNGU atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama jiwe, nami najua ya kuwa sitaona haya.[#Rum 8:31; Eze 3:8,9]

8Yeye anipatiaye haki yangu yu karibu; ni nani atakayeshindana nami? Na tusimame pamoja; ni nani aliye hasimu yangu? Na anikaribie basi.[#Rum 8:33-34; 1 Kor 4:4]

9Tazama, Bwana MUNGU atanisaidia; ni nani atakayenihukumu kuwa mwenye hatia? Tazama hao wote watachakaa kama vazi; nondo atawala.[#Ayu 13:28; Zab 39:11; Ebr 1:11,12]

10Ni nani miongoni mwenu amchaye BWANA, aitiiye sauti ya mtumishi wake? Yeye aendaye katika giza, wala hana nuru, naye alitumainia jina la BWANA, na kumtegemea Mungu wake.[#2 Nya 20:20]

11Tazama, ninyi nyote mwashao moto, mjifungiao hiyo mienge; endeni ninyi katika muali wa moto wenu, na katikati ya mienge mliyoiwasha. Mtayapata haya kwa mkono wangu; mtalala kwa huzuni.[#Rum 10:3; Yn 9:39]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya