Isaya 54

Isaya 54

Agano la amani la milele

1Imba, wewe uliye tasa, wewe usiyezaa; paza sauti yako kwa kuimba, piga kelele, wewe usiyekuwa na uchungu; maana watoto wake aliyeachwa ni wengi kuliko watoto wake yeye aliyeolewa, asema BWANA.[#Gal 4:27]

2Panua mahali pa hema yako, na wayatandaze mapazia ya maskani yako; usiwakataze; ongeza urefu wa kamba zako; vikaze vigingi vya hema yako.

3Kwa maana utaenea upande wa kulia na upande wa kushoto; na wazao wako watawamiliki mataifa; wataifanya miji iliyokuwa ukiwa kukaliwa na watu.

4Usiogope; maana hutatahayarika; wala usifadhaike; maana hutaaibishwa; kwa kuwa utaisahau aibu ya ujana wako, pia masuto ya ujane wako hutayakumbuka tena.

5Kwa sababu Muumba wako ni mume wako; BWANA wa majeshi ndilo jina lake; na Mtakatifu wa Israeli ndiye Mkombozi wako; Yeye ataitwa Mungu wa dunia yote.[#Isa 41:14; 44:6; 49:7; Ayu 19:25; Rum 3:29]

6Maana BWANA amekuita kama mke aliyeachwa na kuhuzunishwa rohoni, kama mke wakati wa ujana, atupwapo, asema Mungu wako.

7Kwa kitambo kidogo nimekuacha; lakini kwa rehema nyingi nitakurudisha.[#2 Kor 4:17]

8Kwa ghadhabu ifurikayo nilikuficha uso wangu dakika moja; lakini kwa fadhili za milele nitakurehemu, asema BWANA, Mkombozi wako.[#Yer 31:3]

9Kwa maana jambo hili limekuwa kama maji ya Nuhu kwangu; maana kama nilivyoapa ya kwamba maji ya Nuhu hayatapita juu ya dunia tena, kadhalika nimeapa ya kwamba sitakuonea hasira, wala kukukemea.[#Yer 31:35; Mwa 9:8-17]

10Maana milima itaondoka, na vilima vitaondolewa; bali wema wangu hautaondoka kwako, wala agano langu la amani halitaondolewa; asema BWANA akurehemuye.[#Zab 46:2; 89:33]

11Ewe uliyeteswa, uliyerushwa na tufani, usiyetulizwa, tazama, nitaweka mawe yako kwa rangi nzuri, nitaweka misingi yako kwa yakuti samawi.[#Ufu 21:18-21]

12Nami nitaifanya minara yako ya akiki nyekundu, na malango yako ya almasi, na mipaka yako yote ya mawe yapendezayo.

13Na watoto wako wote watafundishwa na BWANA; na amani ya watoto wako itakuwa nyingi.[#Isa 11:9; 1 Kor 2:10; 1 The 4:9; Flp 4:7; Yn 6:45; 14:27]

14Utathibitika katika haki; utakuwa mbali na kuonewa, kwa maana hutaogopa; na mbali na hofu, kwa maana haitakukaribia.

15Tazama, hakika ikiwa utashambuliwa na yeyote, haitakuwa kwa shauri langu. Yeyote atakayekushambulia ataanguka kwa ajili yako.

16Tazama, nimemwumba mhunzi afukutaye moto wa makaa, akatoa silaha kwa kazi yake; nami nimemwumba mharibu ili aharibu.

17Kila silaha itengenezwayo juu yako haitafanikiwa, na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa BWANA, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema BWANA.[#Mdo 6:10; 2 Kor 2:14; Ufu 12:10; Isa 50:8,9; 45:24]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya