The chat will start when you send the first message.
1BWANA asema hivi, Shikeni hukumu, mkatende haki; kwa maana wokovu wangu uko karibu kuja, na haki yangu kufunuliwa.[#Mt 3:2; Rum 13:11]
2Heri afanyaye haya, na mwanadamu ayashikaye sana; azishikaye sabato asizivunje, auzuiaye mkono wake usifanye uovu wowote.[#Kut 20:11; Isa 58:13]
3Wala mgeni, aambatanaye na BWANA, asiseme hivi, Hakika yake BWANA atanitenga na watu wake; wala towashi asiseme, Mimi ni mti mkavu.[#Kum 23:1; Mdo 8:27; 1 Pet 1:1]
4Kwa maana BWANA awaambia hivi matowashi, wanaozishika sabato zangu, na kuyachagua mambo yanipendezayo, na kulishika sana agano langu;
5Nitawapa hawa nyumbani mwangu, na ndani ya kuta zangu, kumbukumbu na jina, lililo jema kuliko kuwa na watoto wa kiume na wa kike; nitawapa jina lidumulo milele, lisilokatiliwa mbali.[#Efe 2:22; 1 Tim 3:15; Ebr 3:6; Yn 1:12; Ufu 3:12]
6Na wageni, walioandamana na BWANA ili wamhudumu, na kulipenda jina la BWANA, kuwa watumishi wake; kila aishikaye sabato asiivunje, na kulishika sana agano langu;
7Nitawaleta hao nao hadi katika mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabihu zao zitakubaliwa juu ya madhabahu zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote.[#1 Pet 1:1; 2:5; Zab 4:5; Mal 1:11; Rum 12:1; Ebr 13:15; Mt 21:13; Mk 11:17; Lk 19:46]
8Bwana MUNGU, akusanyaye waliofukuzwa katika Israeli asema, Pamoja na hayo nitamkusanyia na wengine, zaidi ya hao walio wake waliokusanywa.[#Mwa 49:10; Isa 43:6; Efe 1:10]
9Enyi wanyama wote wa porini njoni
Mle, enyi wanyama wote wa porini.
10Walinzi wake ni vipofu, wote pia hawana maarifa; wote ni mbwa walio bubu, hawawezi kulia; huota ndoto, hulala, hupenda usingizi.[#Mt 15:14; Flp 3:2]
11Naam, mbwa hao wana uchu sana, hawashibi kamwe; na hao ni wachungaji wasioweza kufahamu neno; wote pia wamegeuka upande, wazifuate njia zao wenyewe, kila mmoja kwa faida yake, toka pande zote.
12Husema,
Njooni, nitaleta divai,
Na tunywe sana kileo;
Na kesho itakuwa kama leo,
Sikukuu kupita kiasi.