Isaya 59

Isaya 59

Uovu na udhalimu kuadhibiwa

1Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia;[#Hes 11:23; Isa 50:2]

2lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia.

3Kwa maana mikono yenu imetiwa unajisi kwa damu, na vidole vyenu vimetiwa unajisi kwa uovu; midomo yenu imenena uongo, ndimi zenu zimenong'ona uovu.[#Isa 1:15,21; Hos 4:2; Mik 3:10; Rum 3:15]

4Hakuna anayeshitaki kwa haki, wala hapana atetaye kwa kweli; hutumainia ubatili, hunena uongo; hupata mimba ya madhara, na kuzaa uovu.[#Ayu 15:35; Zab 7:14]

5Huangua mayai ya fira, na kusuka wavu wa buibui; yeye alaye mayai yao hufa, na hilo livunjwalo hutoka nyoka.[#Ayu 8:14]

6Nyavu zao hazitakuwa mavazi, wala hawatajifunika kwa kazi zao; kazi zao ni kazi za uovu, na vitendo vya udhalimu vimo mikononi mwao.

7Miguu yao hukimbilia mabaya, nao hufanya haraka kumwaga damu isiyo na hatia; mawazo yao ni mawazo ya uovu; ukiwa na uharibifu zaonekana katika njia zao kuu.[#Mit 1:16; Rum 3:15-17]

8Njia ya amani hawaijui; wala hapana hukumu ya haki katika mienendo yao; wamejifanyia njia zilizopotoka; kila apitaye katika njia hizo hajui amani.[#Zab 125:5; Mit 2:15]

9Kwa sababu hiyo hukumu ya haki iko mbali nasi, wala haki haitufikii; twatazamia nuru, na kumbe! Latokea giza; twatazamia mwanga, lakini twaenda katika giza kuu.[#Yer 8:15]

10Twapapasapapasa kutafuta ukuta kama kipofu, naam, twapapasa kama watu wasio na macho; twajikwaa wakati wa adhuhuri, kana kwamba ni wakati wa ukungu wa alfajiri; kati yao walionenepa tumekuwa kama wafu.[#Kum 28:29; Amo 8:9; Sef 1:17]

11Sisi sote twanguruma kama dubu; twaomboleza kama hua; twatazamia hukumu ya haki, lakini hapana; na wokovu, lakini u mbali nasi.

12Maana makosa yetu yamezidi kuwa mengi mbele zako, na dhambi zetu zashuhudia juu yetu; maana makosa yetu tunayo pamoja nasi, na maovu yetu tumeyajua;

13katika kukosa na kumkana BWANA, na katika kugeuka tusimfuate Mungu wetu, tukinena udhalimu na uasi, na kukusudia maneno ya uongo na kuyatoa moyoni.[#Mt 12:34]

14Na hukumu imegeuka ikaenda nyuma, na haki inasimama mbali sana; maana kweli imeanguka katika njia kuu, na unyofu hauwezi kuingia.[#Neh 8:1]

15Naam, kweli imepunguka kabisa, na yeye auachaye uovu ajifanya kuwa mateka; naye BWANA akaona hayo, akachukizwa kwa kuwa hapana hukumu ya haki.

16Akaona ya kuwa hapana mtu, akastaajabu kwa kuwa hapana mwombezi; basi, mkono wake mwenyewe ndio uliomletea wokovu; na haki yake ndiyo iliyomsaidia.[#Yer 5:1; Eze 22:30; Mk 6:6; Isa 63:5]

17Akajivika haki kama deraya kifuani, na chapeo cha wokovu kichwani pake, akajivika mavazi ya kisasi yawe mavazi yake, naye alivikwa wivu kama joho.[#Zab 35:2; 2 Kor 6:7; 1 The 5:8; Ufu 19:11; Efe 6:14,17; 1 The 5:8]

18Kadiri ya matendo yao, kwa kadiri iyo hiyo atawalipa, ukali kwao wampingao, malipo kwa adui zake; naye atavirudishia visiwa malipo.

19Basi, wataliogopa jina la BWANA toka magharibi, na utukufu wake toka maawio ya jua; maana yeye atakuja kama mkondo wa mto ufurikao, uendeshwao kwa pumzi ya BWANA.[#Zab 113:3; Mal 1:11; Ufu 12:15]

20Na Mkombozi atakuja Sayuni, kwa wao wa Yakobo waachao maasi yao, asema BWANA.[#Rum 11:26]

21Tena kuhusu habari zangu, hili ndilo agano langu nao, asema BWANA; roho yangu iliyo juu yako, na maneno yangu niliyoyatia kinywani mwako, hayataondoka kinywani mwako, wala kinywani mwa wana wako, wala kinywani mwa wajukuu wako, asema BWANA, tangu leo na hata milele.[#Ebr 8:10; Isa 61:1; Eze 36:37]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya