The chat will start when you send the first message.
1Ondoka, uangaze; kwa kuwa nuru yako imekuja,[#Mal 4:2]
Na utukufu wa BWANA umekuzukia.
2Maana, tazama, giza litaifunika dunia,
Na giza kuu litazifunika makabila ya watu;
Bali BWANA atakuzukia wewe,
Na utukufu wake utaonekana juu yako.
3Na mataifa wataijia nuru yako,[#Ufu 21:24]
Na wafalme kuujia mwanga wa mapambazuko yako.
4Inua macho yako, utazame pande zote;
Wote wanakusanyana; wanakujia wewe;
Wana wako watakuja kutoka mbali.
Na binti zako watabebwa nyongani.
5Ndipo utakapoona na kutiwa nuru,
Na moyo wako utatetemeka na kukunjuka;
Kwa kuwa wingi wa bahari utageuzwa kukujia,
Utajiri wa mataifa utakuwasilia.
6Wingi wa ngamia utakufunika,[#Mwa 25:4; Zab 72:10; Mt 2:11]
Ngamia vijana wa Midiani na Efa;
Wote watakuja kutoka Sheba;
Wataleta dhahabu na uvumba;
Na kuzitangaza sifa za BWANA.
7Makundi yote ya Kedari yatakusanyika kwako,[#Mwa 25:13; Hag 2:7-9]
Kondoo dume wa Nebayothi watakutumikia;
Watapanda juu ya madhabahu yangu kwa kibali,
Nami nitaitukuza nyumba ya utukufu wangu.
8Ni nani hawa warukao kama wingu,
Na kama njiwa waendao madirishani kwao?
9Hakika yake visiwa vitaningojea,[#Gal 4:26; Zek 14:14; Yer 3:17; Isa 55:5]
Na merikebu za Tarshishi kwanza,
Ili kuleta wana wako kutoka mbali,
Na fedha yao na dhahabu yao pamoja nao,
Kwa ajili ya jina la BWANA, Mungu wako,
Kwa ajili yake Mtakatifu wa Israeli,
Kwa kuwa amekutukuza wewe.
10Na wageni watajenga kuta zako,[#Zek 6:15; Ufu 21:24]
Na wafalme wao watakuhudumu;
Maana katika ghadhabu yangu nilikupiga,
Lakini katika upendeleo wangu nimekurehemu.
11Malango yako nayo yatakuwa wazi daima;[#Ufu 21:25-26]
Hayatafungwa mchana wala usiku;
Ili watu wapate kukuletea utajiri wa mataifa,
Huku wakiwaongoza wafalme wao.
12Kwa maana kila taifa na ufalme wa watu[#Zab 2:12; Zek 14:17; Mt 21:44; Lk 19:27; Ufu 2:26,27]
Wasiotaka kukutumikia wataangamia;
Naam, mataifa hayo wataharibiwa kabisa.
13Utukufu wa Lebanoni utakujia wewe,[#Isa 35:2; 1 Nya 28:2; Ebr 12:22]
Mberoshi na mtidhari na mteashuri pamoja;
Ili kupapamba mahali pangu patakatifu,
Nami nitapatukuza mahali pa miguu yangu.
14Na wana wa watu wale waliokutesa[#Ufu 3:9; 14:1]
Watakuja kwako na kukuinamia;
Nao wote waliokudharau
Watajiinamisha katika nyayo za miguu yako;
Nao watakuita, Mji wa BWANA,
Sayuni wa Mtakatifu wa Israeli.
15Na kwa kuwa umeachwa na kuchukiwa,
Hata ikawa hapana mtu aliyepita ndani yako,
Nitakufanya kuwa fahari ya milele,
Furaha ya vizazi vingi.
16Utanyonya maziwa ya mataifa,[#Zab 98:2; Isa 43:3; Eze 34:30; Ufu 5:9]
Utanyonya matiti ya wafalme;
Nawe utajua ya kuwa mimi, BWANA, ni mwokozi wako,
Na mkombozi wako, Mwenye enzi wa Yakobo.
17Badala ya shaba nitaleta dhahabu,
Na badala; ya chuma nitaleta fedha,
Na badala ya mti, shaba,
Na badala ya mawe, chuma;
Tena nitaifanya amani kuwa kama msimamizi wako,
Na haki kuwa kiongozi wako.
18Jeuri haitasikiwa tena katika nchi yako,[#Isa 26:1]
Ukiwa na uharibifu hazitakuwa mipakani mwako;
Bali utaziita kuta zako, Wokovu,
Na malango yako, Sifa.
19Jua halitakuwa nuru yako tena wakati wa mchana,[#Zek 2:5; Ufu 21:23; 22:5]
Wala mwezi hautakupa nuru kwa mwangaza wake;
Bali BWANA atakuwa nuru ya milele kwako,
Na Mungu wako atakuwa utukufu wako.
20Jua lako halitashuka tena,[#Amo 8:9]
Wala mwezi wako hautajitenga;
Kwa kuwa BWANA mwenyewe atakuwa nuru yako ya milele;
Na siku za kuomboleza kwako zitakoma.
21Watu wako nao watakuwa wenye haki wote,[#Zab 37:11; Efe 2:10; Mt 5:5; 15:13]
Nao watairithi nchi milele;
Wao ni chipukizi nililolipanda mimi mwenyewe,
Kazi ya mikono yangu mwenyewe,
Ili mimi nitukuzwe.
22Aliye mdogo zaidi atakuwa elfu,[#Mt 13:31; Hos 1:10]
Na mnyonge atakuwa taifa hodari;
Mimi, BWANA, nitayahimiza hayo wakati wake.