Isaya 61

Isaya 61

Habari njema ya ukombozi

1Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu BWANA amenitia mafuta niwahubirie wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwatibu waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao.[#Mt 11:5; Lk 7:22; 4:18; Isa 11:2; Yn 1:32; Zab 34:18; Hos 6:1; Zek 9:12; Yn 8:32-36]

2Kutangaza mwaka wa BWANA uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote waliao;[#Mt 5:4; Law 25:9; Mal 4:1-3]

3kuwaagizia hao waliao katika Sayuni, wapewe taji la maua badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya roho nzito; wapate kuitwa miti ya haki, iliyopandwa na BWANA, ili atukuzwe.[#Zab 30:11; Isa 60:21; Yn 15:8]

4Nao watajenga mahali pa kale palipoharibiwa, watapainua mahali palipokuwa ukiwa zamani, watatengeneza miji iliyoharibiwa, mahali palipoachwa kizazi baada ya kizazi.[#Eze 36:33]

5Na wageni watasimama na kulisha makundi yenu, na watu wa kabila nyingine watakuwa wakulima wenu, na watunzaji wa mizabibu yenu.[#Efe 2:12]

6Bali ninyi mtaitwa makuhani wa BWANA; watu watawaiteni wahudumu wa Mungu wetu; mtakula utajiri wa mataifa, na kujisifia utukufu wao.[#Kut 19:6]

7Badala ya aibu yenu mtapata maradufu, na badala ya fedheha wataifurahia sehemu yao; basi katika nchi yao watamiliki maradufu; furaha yao itakuwa ya milele.[#2 Fal 2:9; Isa 40:2; Zek 9:12]

8Maana mimi, BWANA, naipenda hukumu ya haki, nauchukia wizi na uovu; nami nitawalipa malipo katika kweli, nitaagana nao agano la milele.[#Isa 55:3]

9Na kizazi chao kitajulikana katika mataifa, na uzao wao katika makabila ya watu; wote wawaonao watakiri ya kuwa wao ni kizazi kilichobarikiwa na BWANA.

10Nitafurahi sana katika BWANA, nafsi yangu itashangilia katika Mungu wangu; maana amenivika mavazi ya wokovu, amenifunika vazi la haki, kama bwana arusi ajipambavyo kwa kilemba cha maua, na kama bibi arusi ajipambavyo kwa vyombo vya dhahabu.[#Ufu 21:2]

11Maana kama nchi itoavyo machipuko yake, na kama bustani ioteshavyo vitu vilivyopandwa ndani yake; ndivyo Bwana MUNGU atakavyootesha haki na sifa mbele ya mataifa yote.[#Zab 72:3; Isa 60:18]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya