Isaya 63

Isaya 63

Kisasi juu ya Edomu

1Ni nani huyu atokaye Edomu,[#Isa 34:5-17; Yer 49:7-22; Eze 25:12-14; 35:1-15; Amo 1:11-12; Oba 1-14; Mal 1:2-5]

Atokaye Bosra akiwa na mavazi yenye madoa mekundu?

Huyu aliye na nguo za fahari,

Anayekwenda katika ukuu wa uweza wake?

Ndimi nisemaye kwa haki,

Niliye hodari wa kuokoa.

2Kwa nini mavazi yako ni mekundu,[#Ufu 19:13]

Na nguo zako kama za mtu akanyagaye zabibu?

3Nilikanyaga shinikizoni peke yangu;[#Omb 1:15; Mal 4:3; Ufu 14:20; 19:13,15]

Wala katika watu hakuwapo mtu pamoja nami;

Naam, niliwakanyaga kwa hasira yangu,

Niliwaponda kwa ghadhabu yangu;

Na mavazi yangu yametiwa madoa kwa damu yao,

Nami nimezichafua nguo zangu zote.

4Maana siku ya kisasi ilikuwamo moyoni mwangu,

Na mwaka wao niliowakomboa umewadia.

5Nikatazama, wala hapakuwa na wa kunisaidia;[#Yn 16:32; Zab 44:3; 98:1; Isa 40:10; 51:9; Isa 59:16]

Nikashangaa kwa kuwa hakuna mwenye kutegemeza;

Basi, mkono wangu mwenyewe uliniletea wokovu,

Ghadhabu yangu ndiyo iliyonitegemeza.

6Nikayakanyaga makabila ya watu kwa hasira yangu,[#Ufu 16:6]

Nikawalevya kwa ghadhabu yangu,

Nami nikaimwaga damu yao chini.

Rehema za Mungu zakumbukwa

7Nitautaja wema wa BWANA, sifa za BWANA kwa yote aliyotukirimia BWANA; na wingi wa wema wake kwa nyumba ya Israeli, aliowakirimia kwa rehema zake, na kwa wingi wa wema wake.

8Maana alisema, Hakika ndio watu wangu hawa, wana wasio na hila; akawa Mwokozi wao.

9Katika mateso yao yote yeye aliteswa, na malaika wa uso wake akawaokoa; kwa mapenzi yake, na huruma zake, aliwakomboa mwenyewe; akawainua, akawachukua siku zote za kale.[#Mdo 9:4; 12:11; Kut 14:19; Hos 12:4,5; Mal 3:1; Kum 7:7]

10Lakini wakaasi, wakamhuzunisha Roho yake Mtakatifu; kwa hiyo akawageukia, akawa adui, akapigana nao.[#Zab 78:8,40; Mdo 7:51; Efe 4:30; Ebr 10:29]

11Ndipo alipozikumbuka siku za kale, za Musa, na watu wake, akisema, Yuko wapi yeye aliyewapandisha toka baharini pamoja na wachungaji wa kundi lake? Yuko wapi yeye aliyetia kati yao Roho yake Mtakatifu?

12Aliyewaongoza kwa mkono wake mtukufu, kwa mkono wa kulia wa Musa? Aliyeyatenga maji mbele yao, ili ajifanyie jina la milele?[#Kut 14:21]

13Aliyewaongoza vilindini, kama farasi jangwani, wasijikwae?

14Kama ng'ombe washukao bondeni, Roho ya BWANA ikawastarehesha; ndivyo ulivyowaongoza watu wako, ili ujifanyie jina lenye utukufu.

Sala ya toba

15Tazama toka mbinguni, ukaone toka makao ya utukufu wako na fahari yako; uko wapi wivu wako, na uweza wako? Shauku ya moyo wako, na huruma zako zimezuiliwa kwangu.

16Maana wewe ndiwe Baba yetu, ijapokuwa Abrahamu hatujui, wala Israeli hatukiri; wewe, BWANA, ndiwe Baba yetu, mkombozi wetu tangu milele ndilo jina lako.[#Gal 3:28]

17Ee BWANA, mbona umetukosesha njia zako, ukatufanya kuwa na mioyo migumu hata tusikuogope? Urudi kwa ajili ya watumishi wako, makabila ya urithi wako.[#Zab 119:10; Isa 6:10; Mt 13:15]

18Watu wako watakatifu waliumiliki kwa kitambo tu; adui zetu wamepakanyaga patakatifu pako.[#Dan 8:24]

19Tumekuwa kama watu usiowamiliki kamwe; kama watu wasioitwa kwa Jina lako.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya