Isaya 8

Isaya 8

Mwana wa Isaya kuwa ishara ya uvamizi wa Ashuru

1BWANA akaniambia, Ujipatie ubao mkubwa ukaandike juu yake kwa hati ya kawaida, Kwa Maher-shalal-hash-bazi;[#8:1 Kwa maana ya ‘kuteka kasi, kupokonya upesi’.]

2nami nitajipatia mashahidi waaminifu ili kuandika habari, yaani, Uria, kuhani, na Zekaria, mwana wa Yeberekia.[#2 Fal 16:10]

3Nami nikalala na nabii mwanamke, naye akapata mimba, akazaa mtoto wa kiume. Kisha BWANA akaniambia, Mwite jina lake Maher-shalal-hash-bazi.

4Kwa maana kabla mtoto huyo hajaweza kujua kusema, Baba yangu, na Mama yangu, hazina za Dameski na mateka ya Samaria yatachukuliwa mbele ya mfalme wa Ashuru.[#Isa 7:16]

5Kisha BWANA akasema nami mara ya pili, akaniambia,

6Kwa sababu watu hawa wameyakataa maji ya Shiloa yapitayo polepole, na kufurahi kwa ajili ya Resini na huyo mwana wa Remalia,[#Neh 3:15; Yn 9:7]

7basi sasa angalia; Bwana aleta juu yao maji ya huo Mto, yenye nguvu, mengi sana, nayo ni mfalme wa Ashuru na utukufu wake wote; naye atakuja, na kupita juu ya mifereji yake yote, atafurika juu ya kingo zake zote;

8naye atapita, atapita kwa kasi na kuingia Yuda; atafurika na kupita katikati, atafika hadi shingoni; na kule kuyanyosha mabawa yake kutaujaza upana wa nchi yako, Ee Imanueli.[#Isa 7:14; Mt 1:23]

9Ungameni pamoja, enyi makabila ya watu,

Nanyi mtavunjwa vipande vipande;

Tegeni masikio, ninyi nyote wa nchi zilizo mbali;

Jitahidini, nanyi mtavunjwa vipande vipande;

Jitahidini, nanyi mtavunjwa vipande vipande.

10Fanyeni shauri pamoja, nalo litabatilika;[#Ayu 5:12; Kum 20:1; Yos 1:5; Zab 46:7,11; Isa 9:6; Mt 1:23; Rum 8:31]

Semeni neno, lakini halitasimama;

Kwa maana Mungu yu pamoja nasi.

11Maana BWANA aliniambia hivi, kwa mkono hodari, akanifundisha nisiende katika njia ya watu hawa, akisema,

12Msiseme, Ni njama, kuhusu mambo yote ambayo watu hawa watasema, Ni njama; msihofu kwa hofu yao, wala msiogope.[#1 Pet 3:14-15]

13BWANA wa majeshi ndiye mtakayemtakasa; na awe yeye hofu yenu, na awe yeye utisho wenu.[#Hes 20:12; Lk 12:5]

14Naye atakuwa ni mahali patakatifu; bali ni jiwe la kujikwaza na mwamba wa kujikwaa kwa nyumba za Israeli zote mbili, na mtego na tanzi kwa wenyeji wa Yerusalemu.[#Eze 11:16; Lk 2:24; Rum 9:33; 1 Pet 2:8]

15Na wengi watajikwaa juu yake, na kuanguka na kuvunjika, na kunaswa na kukamatwa.[#Lk 20:18]

Wafuasi wa Isaya

16Ufunge huo ushuhuda, ukaitie mhuri sheria kati ya wanafunzi wangu.[#Dan 12:4]

17Nami nitamngojea BWANA, awafichaye uso wake nyumba ya Yakobo, nami nitamtazamia.[#Hab 2:3; Lk 2:25; Ebr 2:13]

18Angalieni, mimi na watoto hawa niliopewa na BWANA tu ishara na ajabu katika Israeli, zitokazo kwa BWANA wa majeshi, yeye akaaye katika mlima Sayuni.[#Zek 3:8; Ebr 2:13]

19Na wakati watakapokuambia, Tafuta habari kwa watu wenye pepo na kwa wachawi; waliao kama ndege na kunong'ona; je! Haiwapasi watu kutafuta habari kwa Mungu wao? Je! Waende kwa watu waliokufa kwa ajili ya watu walio hai?[#Zab 106:28]

20Na waende kwa sheria na ushuhuda; ikiwa hawasemi kulingana na neno hili, bila shaka kwa hao hakuna asubuhi.

21Nao watapita katikati yake, wamedhikika sana na kuwa na njaa; na itakuwa watakapoona njaa, watalalamika na kuapa kwa mfalme wao, na kwa Mungu wao, na kuelekeza nyuso zao juu;

22nao wataiangalia nchi, na, tazama, shida na giza; hapatakuwa changamko kwa sababu ya dhiki; nao watafukuzwa na kuingia katika giza kubwa.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya