Yakobo 5

Yakobo 5

Onyo kwa matajiri wadhalimu

1Haya basi, enyi matajiri! Lieni, mkapige mayowe kwa sababu ya mateso yenu yanayowajia.[#Lk 6:24]

2Mali zenu zimeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo.[#Mt 6:19]

3Dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto. Mmejiwekea akiba katika siku za mwisho.[#Mit 16:27]

4Angalieni, ujira wa wakulima waliovuna mashamba yenu, ninyi mliokosa kuwalipa kwa hila, unapiga kelele, na vilio vyao waliovuna vimeingia masikioni mwa Bwana wa majeshi.[#Kum 24:14-15; Law 19:13; Mal 3:5; Isa 5:9; Ayu 31:38-40]

5Mmefanya anasa katika dunia, na kujifurahisha kwa tamaa; mmejinenepesha mioyo yenu kama kwa siku ya kuchinjwa.[#Lk 16:19,25; Yer 12:3]

6Mmehukumu mwenye haki mkamwua; wala hashindani nanyi.

Uvumilivu katika mateso

7Kwa hiyo ndugu, vumilieni, hata kuja kwake Bwana. Tazama, mkulima hungoja mazao ya nchi yaliyo ya thamani, huvumilia kwa ajili yake hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho.[#Kum 11:14; Yoe 2:23; Zek 10:1; Yer 5:24; Lk 21:19; Ebr 10:36]

8Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia.[#Ebr 10:25; 1 The 2:16; 3:13]

9Ndugu, msinung'unikiane, msije mkahukumiwa. Angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango.

10Ndugu, watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu.[#Mt 5:12]

11Angalieni, twawaita heri wao waliostahimili. Mmesikia habari za kustahimili kwake Ayubu, kuona mwisho Bwana aliyomtendea, jinsi Bwana alivyo mwingi wa rehema na mwenye huruma.[#Ayu 1:21-22; 2:10; Zab 103:8; 111:4; Dan 12:12]

12Lakini zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, wala kwa mbingu wala kwa nchi; wala kwa kiapo kinginecho chote; bali “ndiyo” yenu na iwe ndiyo, na “Hapana” yenu iwe hapana, msije mkaanguka katika hukumu.[#Mt 5:34-37]

Sala ya imani

13Kuna mtu miongoni mwenu anayeteseka? Na aombe. Ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi.[#Zab 50:15; Kol 3:16]

14Mtu wa kwenu amekuwa mgonjwa? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana.[#Mk 6:13]

15Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa.[#Mk 16:18]

16Basi ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, ili mpate kuponywa. Sala yake mwenye haki ina nguvu nyingi, na hutenda mengi.

17Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia sawa na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita.[#1 Fal 17:1; 18:1; Lk 4:25; Mdo 14:15]

18Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake.[#1 Fal 18:42-45]

19Ndugu zangu, mtu yeyote miongoni mwenu akipotoka mbali na kweli, na kurejeshwa na mtu mwingine;[#Gal 6:1]

20jueni ya kuwa yeye amrejeshaye mwenye dhambi hadi akatoka katika njia ya upotevu, ataokoa roho ya mwenye dhambi kutoka mauti, na kufunika wingi wa dhambi.[#Mit 10:12; 1 Pet 4:8; Zab 51:13]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya