The chat will start when you send the first message.
1Samsoni akateremka hadi Timna, akaona mwanamke huko Timna, mmojawapo wa binti za Wafilisti.[#Mwa 38:13; Yos 15:10; Mwa 34:2; Zab 119:37]
2Kisha akapanda, akawaambia baba yake na mama yake, akasema, Nimemuona mwanamke huko Timna, mmojawapo wa binti za Wafilisti; basi mniruhusu, nimuoe.[#Mwa 21:21; 34:4]
3Ndipo baba yake na mama yake wakamwambia, Je! Hapana mwanamke hata mmoja katika ndugu zako, au katika jamaa zangu wote, hata uende kumuoa mwanamke kwa hawa Wafilisti wasiotahiriwa? Samsoni akamwambia baba yake; Mniruhusu nimuoe huyo, kwa maana ananipendeza sana.[#Mwa 24:3,4; Kut 34:16; Kum 7:3]
4Lakini baba yake na mama yake hawakujua ya kuwa jambo hili ni la BWANA; maana alitaka kisa juu ya Wafilisti. Basi wakati ule Wafilisti walikuwa wakiwatawala Israeli.[#Yos 11:20; 2 Nya 10:15]
5Ndipo Samsoni na baba yake na mama yake wakateremka hadi Timna, walipofika katika mashamba ya mizabibu huko Timna; mara, mwanasimba akamngurumia.
6Roho ya BWANA ikamjia kwa nguvu, naye akampasua kana kwamba anampasua mwana-mbuzi, wala hakuwa na kitu chochote mkononi mwake; lakini hakuwaambia baba yake na mama yake aliyoyafanya.[#Amu 3:10; 13:25; 1 Sam 11:6]
7Basi akateremka na kuzungumza na huyo mwanamke; naye akampendeza Samsoni sana.
8Kisha baadaye akarudi ili kumtwaa, naye akaenda kando kuuangalia mzoga wa huyo simba; na tazama, nyuki wengi walikuwamo ndani ya mzoga wa simba, na asali.
9Akatwaa asali mikononi mwake akasonga mbele, huku akila alipokuwa akienda, akawafikia babaye na mamaye, akawapa, nao wakala; lakini hakuwaambia ya kuwa ameitwaa hiyo asali katika mzoga wa simba.
10Basi babaye akamteremkia huyo mwanamke; Samsoni naye akafanya karamu huko; kwa kuwa ndivyo vijana walivyokuwa wakifanya.
11Basi ikawa hapo watu walipomwona, wakamletea wenziwe thelathini, wawe pamoja naye.
12Samsoni akawaambia, Mimi nitawategea ninyi kitendawili; kama mnaweza kunitegulia katika hizo siku saba za karamu, na kukitambua, ndipo nitakapowapa mavazi thelathini ya kitani na mavazi thelathini ya sikukuu;[#1 Fal 10:1; Eze 17:2; Lk 14:7; Mwa 29:27; 45:22; 2 Fal 5:22]
13lakini msipoweza kunitegulia ndipo mtakaponipa mimi mavazi thelathini ya kitani na mavazi thelathini ya sikukuu. Basi wakamwambia, Haya, tega kitendawili chako, ili tupate kukisikia.
14Naye akawaambia,
Kutoka kwa huyo kikatoka chakula,
Kutoka kwa huyo mwenye nguvu kikatoka kitamu.
Nao katika siku tatu hawakuweza kukifumbua hicho kitendawili.
15Ikawa kwa siku ya saba, wakamwambia mkewe Samsoni, Mbembeleze mumeo, ili atutegulie hicho kitendawili, tusije tukakuteketeza moto wewe na nyumba ya baba yako; je! Mmetuita ili mpate kuichukua mali yetu? Je! Sivyo?[#Mwa 3:6; Amu 16:5; Mit 6:26; Mik 7:6; Amu 15:6]
16Basi mkewe Samsoni akalia mbele yake, akasema, Wewe wanichukia tu, wala hunipendi; wewe umewategea kitendawili hao wana wa watu wangu, nawe hukuniambia mimi. Naye akamwambia, Angalia, sikumwambia baba yangu wala mama yangu, mbonai nikuambie wewe?[#Amu 16:15]
17Naye akalia mbele yake hizo siku saba, wakati ulioendelea karamu yao; basi ikawa siku ya saba akamwambia, kwa sababu alikuwa akimsisitiza sana; naye akawaambia wale wana wa watu wake hicho kitendawili.
18Nao watu wa mji wakamwambia siku ya saba kabla ya jua kuchwa,
Ni kitu gani kilicho tamu kuliko asali?
Ni kitu gani kilicho na nguvu kuliko simba?
Naye akawaambia,
Msingelima na mtamba wangu,
Hamngekitegua kitendawili changu.
19Roho ya BWANA ikamjia juu yake kwa nguvu, naye akateremka hadi Ashkeloni, akawaua wanaume thelathini katika watu hao, na kuzitwaa nyara zao, na kuwapa hao waliokitambua kitendawili mavazi hayo ya sikukuu. Hasira zake zikampanda, naye akakwea kwenda nyumbani kwa baba yake.[#Hes 11:17; 27:18; Amu 3:10; 13:25; 1 Sam 10:6; 11:6; 16:13; 1 Kor 12:4,11]
20Lakini huyo mke wa Samsoni aliozwa mwenzake, ambaye alikuwa amemtendea kama rafikiye.[#Amu 15:2; Yn 3:29]