The chat will start when you send the first message.
1Basi watu wa Efraimu wakamwambia, Kwa nini umetutendea haya? Hata usituite hapo ulipokwenda kupigana na Wamidiani? Nao wakamshutumu vikali.[#Amu 12:1; 2 Sam 19:41]
2Lakini akawaambia, Je! Niliyoyafanya ni nini yakilinganishwa na yale mliyofanya ninyi? Hayo masazo ya zabibu za Efraimu si mema kuliko mavuno ya Abiezeri?
3Mungu amewatia hao wakuu wa Midiani, Orebu na Zeebu, mikononi mwenu; na mimi nilipata kufanya nini kama mlivyofanya ninyi? Ndipo hasira zao walizokuwa nazo juu yake zikatulia aliposema maneno hayo.[#Zab 83:11; Amu 7:24; Zab 44:3; Mit 15:1; Rum 12:3,6]
4Basi Gideoni akafika Yordani, akauvuka, yeye na hao watu mia tatu waliokuwa pamoja naye, walikuwa wamechoka, lakini waliendelea kuwafuatilia adui.
5Naye akawaambia watu wa Sukothi, Tafadhali wapeni mikate hao watu waniandamao; kwa maana wameishiwa na nguvu, nami ni katika kuwafuatia Zeba na Salmuna, wafalme wa Midiani.[#Mwa 33:17; Zab 60:6]
6Hao wakuu wa Sukothi wakasema, Je! Mikono ya Zeba na Salmuna iko mkononi mwako sasa, hata sisi tukawape jeshi lako mikate?[#1 Fal 20:11; 1 Sam 25:11]
7Ndipo Gideoni akasema, Kwa sababu hii, hapo BWANA atakapokuwa amewatia Zeba na Salmuna mkononi mwangu, ndipo nitaipura miili yenu kwa miiba ya nyikani, na kwa michongoma.
8Basi kutoka hapo alikwea kwenda Penieli, akasema na watu wa mahali hapo maneno kama hayo; watu wa Penieli nao wakamjibu kama vile watu wa Sukothi walivyomjibu.[#Mwa 32:30; 1 Fal 12:25]
9Naye akawaambia hao watu wa Penieli nao, akisema, Nitakapokuja tena kwa amani, nitaubomoa mnara huu.[#1 Fal 22:27; Lk 12:45; 1 The 5:2,3; #8:9 au salama.]
10Basi hao kina Zebu na Salmuna walikuwa katika Karkori, na majeshi yao walikuwa pamoja nao, watu kama elfu kumi na tano hesabu yao, ni wote waliobaki wa hilo jeshi lote la hao wana wa mashariki; kwa sababu walianguka wapiganaji elfu mia moja na ishirini waliokuwa wakitumia upanga.[#Amu 7:12; 2 Fal 3:26]
11Basi Gideoni alikwea kwa njia iliyotumiwa na misafara, ambayo ilikuwa mashariki mwa Noba na Yogbeha, akalishambulia hilo jeshi; kwa maana lile jeshi halikuwa na hadhari.[#Hes 32:35; Amu 18:27; Mit 17:18; 1 The 5:3]
12Zeba na Salmuna walikimbia; naye akawaandamia; akawakamata hao wafalme wawili wa Midiani Zeba na Salmuna, akalitapanyatapanya hilo jeshi lote.[#Zab 83:11]
13Kisha huyo Gideoni mwana wa Yoashi akarudi kutoka vitani, kutoka kwenye makweleo ya Heresi.
14Ndipo akamshika kijana mmoja mwanamume katika watu wa Sukothi, akamwuliza; naye akamwandikia majina ya hao wakuu wa Sukothi, na wazee wa mji, watu sabini na saba.
15Kisha akaufikia wale watu wa Sukothi, akawaambia, Tazama, Zeba na Salmuna, ambao ninyi mlinisimanga kwa ajili yao, mliposema, Je! Mikono ya Zeba na Salmuna iko sasa mikononi mwako wewe, hata tuwape watu wako waliochoka mikate?
16Basi akawatwaa hao wazee wa mji, na miiba ya nyikani na michongoma, akawafunza hao watu wa Sukothi kwayo.
17Kisha akaubomoa mnara wa Penieli, na kuwaua watu wa mji huo.[#1 Fal 12:25]
18Ndipo akawaambia hao Zeba na Salmuna, Hao watu mliowaua huko Tabori walikuwa watu wa namna gani? Wakamjibu, Walikuwa kama wewe ulivyo; kila mmoja alikuwa anafanana na wana wa mfalme.[#Amu 4:6; Zab 89:12]
19Naye akasema, Watu hao walikuwa ndugu zangu, wana wa mama yangu; kama yeye BWANA aishivyo, kama mngaliwaokoa hai watu hao, nami nisingewaua ninyi.
20Kisha akamwambia Yetheri mwanawe mzaliwa wa kwanza, Haya, simama, uwaue hawa. Lakini huyo kijana hakutoa upanga wake; maana, akaogopa, kwa sababu alikuwa ni kijana tu.
21Ndipo hapo Zeba na Salmuna wakasema, Simama wewe utuue sisi; kwa maana kama mtu alivyo, ndivyo zilivyo nguvu zake. Basi Gideoni akasimama, akawaua Zeba na Salmuna, akazitwaa koja zilizokuwa katika shingo za ngamia wao.[#Zab 83:11]
22Ndipo watu wa Israeli wakamwambia Gideoni, Tawala wewe juu yetu, wewe, na mwanao, na mjukuu wako pia; kwa kuwa wewe umetuokoa na mikono ya Midiani.
23Gideoni akawaambia, Mimi sitatawala juu yenu wala mwanangu hatatawala juu yenu; yeye BWANA atatawala juu yenu.[#1 Sam 8:7; 10:19; Zab 10:16; 29:10; Isa 26:13; 33:22; Hos 13:10]
24Kisha Gideoni akawaambia, Mimi nina haja yangu niitakayo kwenu, ni ya kila mtu kunipa hizo herini za mateka wake. (Kwa maana walikuwa na herini za dhahabu, kwa sababu walikuwa ni Waishmaeli.)[#Mwa 16:10; 25:13]
25Wakajibu, Tutakupa kwa moyo mweupe. Basi wakatandika nguo chini, wakatia humo kila mtu herini za mateka yake.
26Na uzani wa hizo herini za dhahabu alizozitaka ulipata shekeli za dhahabu elfu moja na mia saba; mbali na makoja na vidani, na mavazi ya rangi ya zambarau waliyokuwa wameyavaa hao wafalme wa Midiani, tena mbali na mikufu iliyokuwa katika shingo za ngamia wao.
27Basi Gideoni akafanya naivera kwa vitu vile, akaiweka katika mji wake, mji huo wa Ofra; nao Israeli wote wakaenda na kuiandama kwa ukahaba huko; nayo ilikuwa ni tanzi kwa Gideoni na kwa nyumba yake.[#Amu 17:5; 18:14,17; 6:24; Kut 23:33; Zab 73:27; 106:39; Kum 7:16]
28Ndipo Midiani walishindwa mbele ya wana wa Israeli, wala hawakuinua vichwa vyao tena. Nayo nchi ilipata kuwa na amani muda wa miaka arubaini katika siku za Gideoni.
29Kisha huyo Yerubaali, mwana wa Yoashi, akaenda kukaa katika nyumba yake mwenyewe.
30Gideoni alikuwa na wana sabini waliozawa na mwili wake; kwa maana alikuwa na wake wengi.[#Amu 9:2,5; 10:4; 12:9,14]
31Na suria yake aliyekuwako Shekemu, yeye naye akamzalia mwana, naye akamwita jina lake Abimeleki.
32Basi Gideoni mwana wa Yoashi akafa mwenye umri wa uzee mwema, akazikwa katika kaburi la Yoashi baba yake, katika Ofra ya Waabiezeri.[#Amu 6:24]
33Kisha ikawa, mara alipokufa Gideoni, wana wa Israeli wakakengeuka tena, wakawaandama Mabaali kwa ukahaba, wakamfanya Baal-berithi kuwa ni mungu wao.[#Amu 2:19; 9:4]
34Kwani wana wa Israeli hawakumkumbuka BWANA, Mungu wao, ambaye ndiye aliyewaokoa na mikono ya adui zao wote pande zote;[#Zab 78:11,42; 106:13-21; Mhu 12:1; Yer 2:32]
35wala hawakuifanyia mema nyumba ya Yerubaali, yaani Gideoni, licha ya hayo mema yote aliyowafanyia Waisraeli.[#Amu 9:16; Mhu 9:14,15]