Yudithi 1

Yudithi 1

VITA VYA AMIRI JESHI HOLOFENE

Afaksadi aimarisha Ekbatana

1Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wake, Nebukadreza, aliyewatawala Waashuri katika ule mji mkubwa Ninawi, alifanya vita na mfalme Afaksadi katika uwanda mkubwa ulioko mpakani mwa Ragae.

2Siku zile Afaksadi alikuwa akiwatawala Wamedi katika Ekbatana; ndiye aliyeujenga ukuta huko Ekbatana na kandokando yake, wa mawe yaliyochongwa yenye upana wa dhiraa tatu na urefu wa dhiraa sita, akafanya kimo cha ukuta dhiraa sabini, na upana wake dhiraa hamsini;

3akafanya minara penye milango yake, kimo chake dhiraa mia moja

4na upana wake msingini dhiraa arubaini, ili kutokezea majeshi yake mkubwa na vikosi vya askari wake.

5-6Wote waliokaa milimani walimwendea Nebukadreza, nao waliokaa kando ya mito Frati na Tigri na Hidaspe, na katika uwanda wa Arioko, mfalme wa Waelima; na kabila nyingi za wana wa Chelodi walikusanyika kwenye vita.

Nebukadreza atoa makataa

7Ndipo Nebukadreza, mfalme wa Waashuri, alipeleka ujumbe kwa wote waliokaa Uajemi, na kwa wote waliokaa upande wa magharibi, na kwao waliokaa Kilikia na Dameski na Libano na Antilibano, na kwa wote waliokaa pwani ya bahari,

8na kwa watu wa mataifa wa Karmeli na Gileadi, na kwa Galilaya ya juu, na uwanda mkubwa wa Esdreloni,

9na kwa wote waliokuwako Samaria na katika miji yake, na ng'ambo ya Yordani mpaka Yerusalemu na Betane na Chelusi na Kadeshi, na mto wa Misri, na Tapanesi na Ramesesi, na nchi yote ya Gosheni

10hata kufika juu ya Tanisi na Nofu, na kwa wote wakao Misri hadi kwenye mipaka ya Ethiopia.

11Lakini wote waliokaa katika nchi hii yote waliidharau amri ya Nebukadreza mfalme wa Waashuri, kwa kuwa hawakumwogopa, ila alionekana machoni pao kama mtu tu. Wakawarudisha wajumbe wake bila kuwasikiliza, wakawatia aibu.

12Basi, Nebukadreza akaighadhabikia nchi hiyo yote, akaapa kwa kiti chake cha enzi, na kwa miliki yake, ya kwamba hakika atajilipiza kisasi juu ya milki zote za Kilikia na Dameski na Shamu, na kuua kwa upanga wenyeji wote wa nchi ya Moabu, na Bani Amoni, na Yuda yote, na wote waliokuwako Misri hata kufika mipaka ya bahari mbili.

Afaksadi kushindwa

13Akaleta vita, akayapanga majeshi yake juu ya mfalme Afaksadi katika mwaka wa kumi na saba, akashinda vitani, akawakimbiza majeshi yote ya Afaksadi, na wapanda farasi wake wote, na magari yake;

14akajitwalia miji yake, akafika mpaka Ekbatana akaitwaa minara yake, akaziharibu njia zake, akaugeuza uzuri wake kuwa aibu.

15Akamtwaa Afaksadi katika milima ya Ragae, akamchoma kwa mishale yake, akamwangamiza kabisa hata leo.

16Akarudi na mateka yake Ninawi, yeye na jeshi lake lote la mataifa mbalimbali, mkutano mkubwa sana wa watu wa vita, na huko akastarehe na kula karamu, yeye na jeshi lake lote, muda wa siku mia moja na ishirini.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya