Yudithi 11

Yudithi 11

Yudithi na Holofene waonana kwa mara ya kwanza

1Holofene akamwambia, Bibi, jipe moyo, usiwe na hofu moyoni mwako; maana mimi sijamtenda mabaya mtu yeyote aliyekubali kumtumikia Nebukadreza, mfalme wa dunia yote.

2Na kama watu wenyeji wa nchi yenye milima wasingalinidharau nisingaliinua mkuki wangu juu yao; lakini wamejipatia mambo haya wao wenyewe.

3Sasa niambie kwa nini uliwatoroka ukaja kwetu – nawe umekuja kujiokoa. Jipe moyo; utaishi usiku huu, na siku zijazo,

4wala hakuna atakayekutenda mabaya; sisi sote tutakutendea mema, kama watendewavyo watumishi wa Mfalme Nebukadreza, bwana wangu.

Yudithi aelezea kuwapo kwake

5Yudithi akamwambia, Uyapokee maneno ya mtumishi wako, mjakazi wako na aseme mbele yako; nami sitamwambia BWANA wangu uongo usiku huu.

6Na kama ukiyafuata maneno ya mjakazi wako, Mungu atakufikilizia kila jambo sawasawa, wala bwana wangu hatakosa makusudi yake.

7Kama Nebukadreza, mfalme wa dunia yote, aishivyo, na kama enzi yake iishivyo, aliyekupeleka kumlindia viumbe vyote, si wanadamu tu wanaomtumikia kwako, ila hayawani na wanyama wafugwao na ndege wa angani wataishi kwa nguvu zako, katika zamani za Nebukadreza na nyumba yake yote.[#Yer 27:6; Dan 2:38]

8Maana tumesikia habari za hekima yako na busara ya roho yako, hata imejulikana katika nchi yote ya kuwa wewe peke yako u jemadari hodari katika ufalme wote, mwenye maarifa mengi, na wa ajabu katika matendo ya vita.

9Basi, juu ya habari ile aliyoisema Akioro barazani pako, tumeyasikia maneno yake; maana watu wa Bethulia walimwokoa, akawaeleza yote aliyoyasema mbele yako.

10Kwa hiyo, Ee bwana wangu, usilidharau neno lake, bali liweke moyoni mwako, maana ni kweli; yaani, taifa letu halitaadhibiwa, wala upanga hautalishinda, isipokuwa wakimkosa Mungu wao.

11Na sasa, kusudi bwana wangu asishindwe na kuukosa mpango wake, mauti itawaangukia. Maana dhambi yao, ambayo kwayo watamkasirisha Mungu imekwisha kuwapata wakati watakapokosa.

12Tangu chakula chao kilipowaishia, na maji yao yote yaliwatindikia, wamefanya mashauri juu ya wanyama wao, kwamba wale vyakula vile vyote ambavyo Mungu aliwaagiza wasile.

13Wamekata shauri pia kutumia malimbuko ya ngano, na sehemu za kumi za divai na mafuta walizozitakasa na kuziweka kwa matumizi ya makuhani wasimamao usoni pa Mungu Yerusalemu – vitu ambavyo haiwapasi watu wengine hata kuvigusa kwa mikono yao.[#Kut 23:19; Law 27:30]

14Nao wamepeleka watu Yerusalemu, kwa sababu huko pia walitenda hivyo, kuwaletea idhini kutoka barazani.

15Basi, itakuwa, watakapoletewa jibu, na kulitimiza jambo hilo, siku iyo hiyo watatolewa kuangamizwa.

16Kwa hiyo, mimi mtumishi wako, nikiyajua hayo yote, nilikimbia kutoka mbele yao; naye Mungu amenituma kutenda pamoja nawe mambo yatakayoushangaza ulimwengu wote, yaani wote watakaoyasikia.

17Maana mtumishi wako ni mcha Mungu, anamtumikia Mungu wa mbinguni mchana na usku. Na sasa, bwana wangu, nitakaa nanyi, nami mtumishi wako nitatoka usiku kwenda bondeni kumwomba Mungu, naye ataniarifu watakapotenda dhambi zao,

18ndipo nitakapokuja kukupa habari, nawe utatoka na jeshi lako lote, wala hatakuwapo hata mmoja atakayekupinga.

19Nami nitakuongoza katikati ya Yuda hataa ufike Yerusalemu; nitakuwekea kiti katikati ya mji, nawe utawasaka kama kondoo wasio na mchungaji, wala hakuna hata mbwa atakayefunulia kinywa chake. Maana niliambiwa mambo hayo kwa kufunuliwa, yakatangazwa kwangu, nikatumwa kukupa habari.

20Maneno yake yakapendeza usoni pa Holofene na watumishi wake wote, wakaistaajabia hekima yake, wakasema,

21Toka mwisho mmoja wa dunia hata mwisho mwingine hakuna mwanamke kama huyu kwa uzuri wa uso na busara ya maneno.

22Holofene akamwambia, Mungu alifanya vema kukupeleka mbele ya watu, ili nguvu iwe mikononi mwetu, na maangamizo kwao waliomdharau bwana wangu.

23Nawe u mzuri wa sura na hodari wa maneno, na kama utafanya kama ulivyosema Mungu wako atakuwa Mungu wangu, nawe utakaa nyumbani mwa Mfalme Nebukadreza na kusifiwa duniani kote.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya