The chat will start when you send the first message.
1Ikawa, jua liliposhuka, watumishi wake walifanya haraka kuondoka. Bagoa akalifunga hema kwa nje, akawapa ruhusa wale waliokuwa wakimhudumia bwana wake, wakaenda kulala kitandani, maana wote walikuwa wamechoka, kwa kuwa karamu ilichukua wakati mwingi.
2Yudithi akabaki peke yake hemani pamoja na Holofene, naye amelala kitandani, yu hoi kwa ulevi.
3Naye Yudithi alikuwa amemwagiza mjakazi wake asimame nje ya chumba chake cha kulala amngojee hata atoke, kama kawaida yake ya kila siku, maana atakwenda kusali. Na Bagoa naye, alikuwa amemwambia vivi hivi.
4Basi, watu wote waliondoka kwake, hakuna aliyebaki hemani, mdogo wala mkubwa. Yudithi akasimama kitandani pake akaomba moyoni mwake, Ee Bwana Mungu Mwenye uweza wote, iangalie sasa kazi ya mikono yangu kwa utukufu wa Yerusalemu.
5Sasa ndio wakati wa kuusaidia urithi wako, na kufanya yale niliyokusudia kwa mavunjiko ya adui waliotuinukia.
6Akauendea ubao juu ya kitanda, upande wa kichwa cha Holofene, akaitungua jambia yake humo,
7akasogea kitandani akazishika nywele za kichwa chake, akasema, Ee Bwana Mungu wa Israeli, nipe nguvu leo.
8Akampiga shingo mara mbili kwa nguvu zake zote, akamkata kichwa;
9akaukokota mwili wake toka kitandani na kuuangusha chini; akatungua chandarua katika nguzo zake; na baada ya muda kidogo akatoka.
10Akampa mjakazi wake kichwa cha Holofene akakitia katika mfuko wake wa chakula. Wakatoka wao wawili kama kawaida yao, kwenda kusali. Wakapitia kambini, wakazunguka mle bondeni, wakapanda mlima hata Bethulia, wakafika milangoni pa mji.
11Yudithi akawaambia walinzi wa milango Fungua! Fungua mlango sasa! Mungu, Mungu wetu, yu pamoja nasi, ili aoneshe hata sasa uweza wake katika Israeli na nguvu zake juu ya adui alivyoidhihirisha leo.
12Ikawa watu wa mjini walipoisikia sauti yake waliiendea milango ya mji upesi, wakawaita wazee wa mji waje.
13Wote wakakusanyika, wakubwa kwa wadogo, maana kurudi kwake hakukutazamiwa, wakafungua mlango wakawakaribisha. Wakawasha moto wapate nuru, wakawazunguka pande zote.
14Akawaambia kwa sauti kubwa, Msifuni Mungu, Msifuni! Msifuni Mungu asiyeiondolea nyumba ya Israeli fadhili zake, bali amewavunja adui zetu kwa mkono wangu usiku huu.
15Akakitoa kichwa mfukoni akawaonesha, akawaambia, Kitazameni kichwa cha Holofene, jemadari mkuu wa jeshi la Ashuru! Kitazameni chandarua chake alimolala katika ulevi wake, hata Mungu kampiga kwa mkono wa mwanamke!
16Kama Bwana aishivyo aliyenilinda katika njia niliyokwenda, sura yangu ndiyo iliyomvuta kwenye maangamizo yake, wala hakutenda dhambi nami, kunitia unajisi na aibu.
17Watu wote wakashangaa kabisa, wakainama wakamwabudu Mungu, wakisema wote, Umehimidiwa, Ee Mungu wetu, uliyewaangamiza maadui wa watu wako leo.
18Uzia akamwambia, Umebarikiwa, binti yangu, usoni pa Mungu Aliye Juu, kuliko wanawake wote duniani. Na ahimidiwe BWANA Mungu, Muumba mbingu na nchi, aliyekuongoza hata ukampiga kichwa mkuu wa adui zetu.[#Amu 5:24; Lk 1:28,42]
19Imani yako haitatoka mioyoni mwa watu wanaoukumbuka uweza wa Mungu milele.
20Mungu afanye mambo hayo yawe kwako sifa ya daima, akujaze mema; kwa kuwa hukuiachilia maisha yako kwa ajili ya mateso ya taifa letu, bali uligeuzia mbali maangamizo yetu, ukashika njia iliyonyoka mbele ya Mungu wetu. Watu wote wakasema, Amin, Amin.