Yudithi 14

Yudithi 14

USHINDI

Mawaidha ya Yudithi

1Yudithi akawaambia, Nisikilizeni sasa, ndugu zangu. Kichukueni kichwa hiki, kitundikeni katika ukuta wa boma lenu.

2Na itakuwa, kunapopambazuka asubuhi, na jua linachomoza, mtashika kila mtu silaha zake za vita, na kila mtu hodari miongoni mwenu atatoka mjini, nanyi mtaweka jemadari juu yao, kana kwamba mnataka kuushukia uwanda wa chini kwenye walinzi wa wana wa Ashuru; lakini msishuke.

3Nao watachukua mavazi yao ya vita na kwenda kambini kuwaamsha wakuu wa jeshi la Ashuru; nao wote watakwenda mbio hemani kwa Holofene, wasimwone. Ndipo hofu itawaangukia, nao watakimbia mbele yenu.

4Basi, ninyi na wote wanaokaa katika mitaa ya Israeli mtawafuata na kuwaangusha njiani.

5Lakini kabla ya kufanya hayo, niitieni Akioro Mwamoni, ili amwone akamjue yeye aliyeidharau nyumba ya Israeli na kumpeleka kwetu kusudi afe.

6Wakamwita Akioro katika nyumba ya Uzia. Naye alipokuja akakiona kichwa cha Holofene mkononi mwa mtu mmoja katika mkutano wa watu, alianguka kifudifudi na moyo wake ulizimia.

7Hata walipomwinua alianguka miguuni pa Yudithi akamsujudia, akasema, Umebarikiwa wewe katika kila hema ya Yuda, na katika kila taifa, nao wanapolisikia jina lako watafadhaika.

8Sasa nieleze yote uliyoyatenda siku hizi. Yudithi akamweleza katikati ya watu mambo yote aliyoyafanya tangu siku alipotoka hata wakati huo anaposema nao.

9Naye akiisha maneno yake watu wote wakapaza sauti zao wakashangilia wakapiga vigelegele vya furaha mjini mwao.

10Naye Akioro alipoyaona mambo aliyoyafanya Mungu wa Israeli alimwamini Mungu kabisa, akatahiriwa, akaungwa na nyumba ya Israeli hata leo.

Kifo cha Holofene kutangazwa

11Basi, mara kulipokucha, walikitungika kichwa cha Holofene ukutani, kila mtu akatwaa silaha zake, wakatoka vikosi vikosi kwenye njia za milimani.

12Nao wana wa Ashuru walipowaona walipeleka habari huku na huko kwa maakida wao, nao wakaenda kwa majemadari wao na maamiri wao na wakuu wao wote.

13Wakaja hemani kwa Holofene, wakamwambia yule aliyesimamia nyumba yake yote, Mwamshe bwana wetu sasa, maana wale watumwa wamethubutu kutushukia kupigana nasi kwa maangamizi yao.

14Bagoa akaenda, akapiga hodi nje ya hema, maana alidhani yumo amelala na Yudithi.

15Hata asipopata jibu alifungua, akaingia katika chumba cha kulalia, akamwona yupo chini karibu na kitanda, ameondolewa kichwa.

16Akalia kwa sauti kuu, akiomboleza na kuugua na kupiga kelele na kurarua nguo zake.

17Akaingia hemani alimolala Yudithi asimwone. Akawaendea watu mbio, akapaza sauti yake akasema,

18Wale watumwa wametudanganya. Mwanamke mmoja wa Kiebrania ametahayarisha nyumba ya Mfalme Nebukadreza, maana kumbe, Holofene amelala chini, hana kichwa!

19Nao wakuu wa jeshi la Ashuru waliposikia maneno hayo walirarua nguo zao wakifadhaika mno. Kulikuwa na maombolezo na kilio kikubwa kambini.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya