The chat will start when you send the first message.
1Mwimbieni Mungu wangu kwa matari;
Mwimbieni Bwana wangu kwa matoazi;
Mwimbieni zaburi na nyimbo za shangwe;
Mtukuzeni, mliitieni jina lake.
2Maana BWANA ndiye Mungu azivunjaye silaha za vita;
Alipokaa kambini miongoni mwa watu
Aliniokoa mkononi mwao walionitesa.
3Ashuru alitoka katika milima ya kaskazini;
Alikuja na askari zake makumi elfu.
Kwa wingi wao waliiziba mito,
Na wapanda farasi wao waliifunika milima.
4Alisema ataziteketeza nchi zangu
Na kuwaua vijana wangu kwa upanga;
Atawatupa chini watoto wangu wanyonyao,
Na kuwatoa wana wangu wawe mateka,
Na wanawali wangu wawe nyara.
5BWANA Mwenyezi aliwaangamiza
Kwa mkono wa mwanamke.
6Shujaa wao hakuanguka kwa pigo la vijana,
Wala kuuawa na wana wa majitu,
Wala kushambuliwa na majitu ya juu.
Ila Yudithi binti Merari alimdhoofisha
Kwa uzuri wa sura yake.
7Alivua nguo zake za ujane
Ili walioteswa katika Israeli wainuliwe;
Alijipaka marhamu usoni.
8Akasuka nywele zake kwa mapambo,
Akavaa nguo ya kitani ambembeleze.
9Kiatu chake kilimfurahisha jicho lake;
Uzuri wake ukaiteka nyara roho yake;
Jambia likamchoma shingoni.
10Waajemi waliutetemekea ujasiri wake;
Wamedi walitishwa na ushupavu wake.
11Ndipo wanyenyekevu wangu walipiga kelele za shangwe,
Wanyonge wangu walilia kwa sauti kuu.
Adui walijikunyata kwa hofu,
Walilalamika wakakimbia.
12Wana wa wajakazi wakawachoma,
Waliwajeruhi kama wana wa watoro,
Wakauawa na jeshi la BWANA wangu.
13Nitamwimbia Mungu wangu wimbo mpya.[#Zab 144:9]
Ee BWANA, Wewe ndiwe mkuu, mwenye fahari;
Wa ajabu katika uweza wako, hakuna kama Wewe.
14Viumbe vyako vyote vikutumikie,
Maana ulisema vikafanyika,
Ulitoa Roho yako vikaumbwa,
Wala hakuna atakayeshindana na sauti yako.
15Milima husukasuka katika misingi yake kama maji
Miamba huyeyuka kama nta mbele yako;
Lakini u mwenye rehema kwao wanaokucha.
16Dhabihu zote hazitoshi kwa harufu ya manukato;[#1 Sam 15:22; Zab 51:16-17; Hos 6:6]
Wala shahamu yote kwa sadaka ya kuteketezwa kwako.
Lakini yeye amchaye BWANA ni mkuu daima.
17Ole wa mataifa wainukao juu ya taifa langu,
BWANA Mwenyezi atawapatiliza siku ya hukumu,
Akitia nyama yao moto na funza,
Nao watalia na kuumia daima.
18Ikawa walipofika Yerusalemu walimwabudu Mungu; watu wakatakaswa, wakatoa sadaka nzima za kuteketezwa, na sadaka za hiari, na matoleo yao.
19Yudithi akaiweka wakfu mali yote ya Holofene aliyopewa na watu, akakitoa na chandarua alichokitwaa mwenyewe katika chumba chake cha kulalia, kiwe sadaka kwa BWANA.
20Watu wakazidi kula karamu Yerusalemu kwa muda wa miezi mitatu mbele ya patakatifu, naye Yudithi akakaa nao.
21Na baada ya siku hizo kila mtu alikwenda kwao, na Yudithi alikwenda Bethulia akakaa shambani mwake, akastahiwa katika zamani zake katika nchi yote.
22Wengi walimtamani, lakini hakuna aliyemjua siku zote za maisha yake tangu siku aliyokufa mumewe Manase akakusanywa kwa watu wake.
23Sifa yake ikazidi sana. Akazeeka katika nyumba ya mumewe hata kupata umri wa miaka mia moja na mitano. Akamweka mjakazi wake huru. Akafa Bethulia, wakamzika katika pango la mumewe Manase.
24Waisraeli wakamwomboleza siku saba. Naye, kabla ya kufa kwake, aligawa mali yake kwa jamaa za karibu wa mumewe Manase, na kwa jamaa zake wa karibu.
25Ikawa hakuna aliyewatia wana wa Israeli hofu tena katika siku zake Yudithi, wala kwa siku nyingi baada ya kufa kwake.