The chat will start when you send the first message.
1Na wana wa Israeli waliokaa Yuda walisikia habari za Holofene, jemadari mkuu wa Nebukadreza, mfalme wa Waashuri, jinsi alivyowatenda mataifa, na jinsi alivyoyaharibu mahekalu yao yote na kuyaangamiza kabisa;
2wakaona hofu nyingi juu yake, na kufadhaika sana kwa ajili ya Yerusalemu na hekalu la BWANA Mungu wao.
3Maana ilikuwa ndiyo kwanza warudi kwao baada ya uhamisho wa Babeli, na watu wa Yuda kukusanyika pamoja, na vyombo na madhabahu na nyumba yenyewe kutakaswa baada ya kule kutiwa unajisi.
4Wakapeleka kwenye kila mtaa wa Samaria, na Kone, na Beth-horoni, na Belmaimu, na Yeruko, na Choba, na Esoro, na bonde la Salemu,
5wakavishika upesi vilele vya milima mirefu, wakaitia nguvu miji yake na kuweka akiba ya chakula kwa matumizi ya vita, maana wakati huo mashamba yalikuwa yamekwisha vunwa.
6Naye Yoakimu, kuhani mkuu, aliyekuwako Yerusalemu siku zile, aliwaandikia watu waliokaa Bethulia na Betomesthaimu, karibu na Esdreloni penye uwanda ulio karibu na Dothaimu,
7kuwaagiza wazishike njia za kupandia katika nchi ya milima. Maana njia hizo ni mlango wa kuingilia Yuda, tena ni rahisi kuzuia watu wasipite kwa sababu njia hizo ni nyembamba, za kupitisha mtu mmoja mmoja tu, au mwisho wawili.
8Nao wana wa Israeli walifanya kama Yoakimu, kuhani mkuu, alivyowaagiza, yeye na baraza ya Waisraeli waliokaa Yerusalemu.
9Na Waisraeli wote walimlilia Mungu kwa bidii sana, na kujinyenyekeza mbele zake kwa bidii.
10Wao, pamoja na wake zao na watoto, na wanyama wao, na kila mgeni aliyekuwako kwao, na kila mtu wa mshahara, na kila mtumwa aliyenunuliwa kwa fedha, walijivika magunia viunoni.[#Yon 3:7-8; Est 4:1-3]
11Na Waisraeli wote, wanaume kwa wanawake, hata watoto wadogo, pamoja na wenyeji wa Yerusalemu, walianguka kifudifudi mbele ya hekalu, wakajitia majivu vichwani na kunyosha mavazi yao ya magunia mbele za Mungu.
12Wakatanda magunia juu ya madhabahu. Na wote kwa sauti moja walimsihi Mungu wa Israeli kwa bidii asiwatoe watoto wao wawe mateka, na wake zao wawe nyara, wala wasiitoe miji ya urithi wao iharibiwe, na patakatifu pake patiwe unajisi na aibu na kudhihakiwa na mataifa.
13BWANA akaisikia sauti yao akaiangalia dhiki yao, na watu wakaendelea katika kufunga muda wa siku nyingi, katika Yuda yote na Yerusalemu, mbele ya patakatifu pa BWANA Mwenyezi.[#Est 4:16]
14Na Yoakimu, kuhani mkuu, na makuhani wote waliosimama mbele za BWANA, nao waliomhudumia BWANA, walikuwa wamejifunga magunia viunoni; wakatoa sadaka za kuteketezwa za kila siku, pamoja na nadhiri na sadaka za hiari, nao walikuwa wamejitia majivu juu ya kofia zao.[#Yoe 2:17]
15Wakamlilia BWANA kwa nguvu zao zote apate kuiangalia nyumba ya Israeli kwa wema.