The chat will start when you send the first message.
1Basi, Holofene, jemadari mkuu wa jeshi la Ashuru, alipata habari ya kuwa wana wa Israeli wamejiweka tayari kwa vita, tena wamezifunga njia za milimani na kuvitia nguvu vilele vya milima mirefu na kuweka mapingamizi uwandani.
2Naye akakasirika mno, akawaita wakuu wote wa Moabu, na maakida wa Amoni, na viongozi wa pwani ya bahari,
3akawaambia: Enyi, wana wa Kanaani, niambieni: Watu hawa wanaokaa katika nchi yenye milima ni nani, na miji yao ni ya namna gani? Watu wa jeshi lao ni wangapi, na nini asili ya uwezo wao na nguvu zao? Mfalme awatawalaye na kuliongoza jeshi lao yu nani?
4Na kwa nini wamenipa kisogo wasije kunilaki kama wote wengine wakaao pande za magharibi?
5Ndipo Akioro, mkuu wa Bani Amoni, akamwambia: BWANA wangu na alisikie neno litokalo katika kinywa changu mimi mtumishi wako, nami nitakueleza yaliyo kweli juu ya watu hawa wakaao katika nchi hii yenye milima, karibu na mahali unapokaa; wala hakuna uongo utakaotoka kinywani mwangu, mimi mtumishi wako.
6Watu hao ni wa ukoo wa Wakaldayo,
7lakini zamani walifanya makazi yao Mesopotamia, kwa sababu hawakutaka kuifuata miungu ya baba zao katika nchi ya Wakaldayo,
8bali waliiacha njia ya wazee wao wakamwabudu Mungu wa mbinguni, Mungu waliyemjua. Nao waliwafukuza katika nchi ya miungu yao, wakakimbilia Mesopotamia, wakakaa huko siku nyingi.
9Kisha, Mungu wao aliwaamuru waondoke pale walipokuwa wakikaa, waende katika nchi ya Kanaani. Wakakaa huko, wakaongezewa dhahabu na fedha na wanyama wengi mno.[#Mwa 11:31—12:5]
10Wakashukia Misri kwa sababu njaa kubwa iliiangukia nchi yote ya Kanaani, wakafanya makao yao huko walikopata chakula, wakaongezeka kuwa wengi sana, hata hakuna awezaye kulihesabu taifa lao.[#Mwa 42:1-5; Kut 1:7]
11Mfalme wa Misri akawainukia akawafanyia hila, akawadhilisha akiwatumikisha kazi ya matofali, akawafanya watumwa.[#Kut 1:8-14]
12Wakamlilia Mungu wao, naye akaipiga nchi yote ya Misri kwa mapigo yasiyoponyeka, hata Wamisri walipowaondoa machoni pao.[#Kut 7:1-12; 29:46]
13Mungu akaikausha Bahari ya Shamu mbele yao,[#Kut 14:21-22]
14akawaongoza katika njia ya Sinai na Kadesh-barnea, wakawaondoa wote waliokuwa wakikaa jangwani.
15Wakafanya makao yao katika nchi ya Waamoni, wakawaharibu watu wote wa Heshboni kwa nguvu yao. Wakavuka Yordani wakaimiliki nchi yote yenye milima,
16wakafuwakuza mbele yao Wakanaani na Waperizi na Wayebusi na Washekemu na Wagirgashi wote, wakakaa katika nchi yenye milima siku nyingi.
17Hata muda wote walioishi bila dhambi mbele ya Mungu wao walistawi, maana Mungu achukiaye maovu alikuwa pamoja nao.[#Kum 28:1-68]
18Lakini walipoiacha njia aliyowaagiza waliangamizwa katika vita vingi vikali mno, wakachukuliwa mateka katika nchi ya kigeni. Nalo hekalu la Mungu wao liliangushwa hata nchi, na miji yao ilishikwa na adui zao.
19Na sasa wamemrudia Mungu wao na kutoka katika nchi ya uhamisho wao walipotawanywa; wamerudi Yerusalemu, palipo patakatifu pao, na kuikalia nchi yenye milima, maana ilikuwa haina watu.
20Basi, sasa, bwana wangu na mkuu wangu, kama likiwapo kosa katika watu hao, wakitenda dhambi juu ya Mungu wao, tuliangalie jambo hili lililowakwaza, tukapande na kuwashinda.
21Lakini kama hakuna maasi katika taifa lao, basi, bwana wangu na awaambae, isiwe kama BWANA wao atawalinda, na Mungu wao awe upande wao, nasi tutakuwa dhihaka mbele ya ulimwengu wote.
22Ikawa, Akioro akiisha kusema maneno hayo, watu wote waliolizunguka lile hema na kusimama kandokando yake walinung'unika, na wakuu wa Holofene na wote waliokaa pwani ya bahari na katika nchi ya Moabu walitoa shauri auawe.
23Wakasema, Sisi hatuwezi kuwaogopa wana wa Israeli, maana, tazameni! Ni taifa lisilo na uwezo wala nguvu ya kufanya vita vikali.
24Kwa hiyo tutapanda, nao watakuwa nyara ya kutekwa na jeshi lako lote, Ee Bwana Holofene.