Yudithi 7

Yudithi 7

BETHULIA UNAZINGWA

Juhudi na mipango juu ya Bethulia

1Asubuhi yake, Holofene alitoa amri kwa jeshi lake lote, na kwa watu wote waliokuja kujiunga naye, wahamishe kambi lao kuendea Bethulia, wakashike upesi njia za kupandia katika nchi yenye milima na kupigana na wana wa Israeli.

2Basi, siku ile, kila mtu hodari aliondoka, hata hesabu ya watu wa vita ilikuwa askari wa miguu elfu mia moja na sabini, na wapanda farasi elfu kumi na mbili, licha ya wenye mizigo na watu waliofuatana nao kwa miguu, watu wengi mno.

3Wakapiga kambi bondeni karibu na Bethulia, karibu na kisima, wakajieneza katika nchi ya Dothaimu hata Belmaimu kwa upana, na toka Bethulia hata Kiamoni, karibu na Esdreloni, kwa urefu.

4Nao wana wa Israeli, walipoona wingi wao, walifadhaika mno, wakasemezana kila mtu na jirani yake, Sasa watu hawa wataulamba uso wote wa ardhi; milima mirefu na mabonde na vilima havitaweza kustahimili uzito wao.

5Kila mtu akatwaa silaha zake, wakawasha mioto juu ya minara yao, wakakaa tayari, wakikesha usiku kucha.[#1 Mak 12:28-29]

6Basi, siku ya pili, Holofene aliwatoa askari zake wapanda farasi wote machoni pa wana wa Israeli waliokuwako Bethulia,

7akazipeleleza njia za kuupandia mji wao; akavivumbua visima vya maji akavishika, akaweka vikosi vya askari kuvilinda; akaondoka yeye akarudi kwake.

8Wakamjia wakuu wa Bani Esau, na viongozi wote wa watu wa Moabu, na viongozi wa nchi ya pwani, wakasema:

9Bwana wetu na asikilize neno moja, kusudi jeshi lako lisipatwe na hasara.

10Watu hawa, wana wa Israeli, hawaitumainii mikuki yao, ila huutumainia urefu wa milima wanakokaa, maana si rahisi kuvifikia vilele vyake.

11Basi sasa, bwana wangu, usipigane nao kama watu wapiganavyo wakifungana vita; hivyo hakuna hata mmoja wa watu wako atakayekufa.

12Kaeni kambini, watu wote wa jeshi lako wawe salama, uwaagize watumsihi wako waikamate chemchemi ya maji yatokayo chini ya milima,

13maana wote wakaao Bethulia hupata maji huko. Hivyo watakufa kwa kiu, na kuutoa mji wao. Nasi, pamoja na watu wetu, tutapanda juu ya milima iliyo karibu, na kufanya kambi letu huko, tuwavizie, asitoke mjini hata mtu mmoja.

14Watadhoofu kwa njaa, wao na wake zao na watoto wao hata kabla upanga haujawapata wataanguka katika njia za mji wao.

15Nawe utajilipiza kisasi juu yao kwa sababu walikuasi, wala hawakuja kukulaki kwa amani.

16Maneno yao yakapendeza machoni pa Holofene, na machoni pa watumishi wake wote, akatoa amri ifanywe kama walivyosema.

17Basi, jeshi la wana wa Amoni likaondoka, na pamoja nao watu elfu tano wa wana wa Ashuru, wakapiga kambi bondeni, wakazishika chechemi za maji ya wana wa Israeli.

18Wana wa Esau wakapanda pamoja na wana wa Amoni, wakafanya kambi katika nchi ya milima karibu na Dothaimu. Wakapeleka wengine upande wa kusini, na wengine upande wa mashariki, kuelekea Ekrebeli, karibu na Chusi, kando ya kijito Mokmuri. Na waliobaki wa jeshi la Waashuri wakatua uwandani, wakaenda katika uso wa nchi, hata mahema yao na mizigo yao ilisongana sana kotekote, nao walikuwa watu wengi mno.

Udhia wa Israeli

19Wana wa Israeli wakamlilia BWANA Mungu wao, maana roho zao zilizimia kwa sababu ya adui zao waliowazunguka pande zote hata hakuna njia ya kutoka katikati yao.

20Jeshi lote la Ashuru likawazunguka hivi, askari wao na magari yao na wapanda farasi wao, muda wa siku thelathini na nne,

21hata maji yalikwisha katika vyombo vyote vya watu wa Bethulia. Mabirika yakapungua maji, wala hawakushiba maji hata siku moja, ila walipewa kwa kipimo.

22Watoto wadogo wakalegea, na wanawake na vijana walizimia kwa kiu, wakaanguka katika njia za mji na penye milango, wala haikuwamo tena nguvu ndani yao.

23Watu wote wakajikusanya juu ya Uzia, na juu ya wakuu wa mji, vijana, wanawake na watoto, wakalia kwa sauti kubwa, wakasema mbele ya wakuu wote:

24Mungu aamue kati ya ninyi na sisi, maana mmetudhulumu sana kwa kutowapa wana wa Ashuru maneno ya amani.

25Sasa hatuna msaidizi, ila Mungu ametuuza mikononi mwao kuangushwa mbele yao kwa kiu na maangamizo makubwa.

26Basi, waiteni, mtoe mji wote mateka kwa watu wa Holofene na jeshi lake lote.

27Maana ni afadhali kwetu tuwe mateka yao, kwa kuwa hivi tutakuwa watumwa na roho zetu zitaishi; wala hatutaona watoto wetu wachanga wakifa machoni petu, wala wake zetu na wana wetu wakizimia kufani.

28Twawashuhudiza mbingu na nchi, na Mungu wetu, BWANA wa baba zetu, anayetupatiliza dhambi zetu na dhambi za baba zetu, asifanye kama tulivyosema leo.

29Kukatokea kilio kikuu katika mkutano, watu wote wakiomboleza pamoja; wakamlilia BWANA kwa sauti kubwa.

30Uzia akawaambia, Ndugu zangu, jipeni moyo. Tustahimili siku tano tena, ili kwa muda huo BWANA Mungu wetu atuoneshe rehema zake, kwa maana yeye hatatutupa kabisa.

31Na kama siku hizi zikipita, wala hatuletewi msaada, basi, nitafanya kama mlivyosema.

32Akawapa watu ruhusa, kila mtu aende mahali pake, wakaenda kwenye makuta na minara ya mji wao. Akawapeleka wanawake na watoto nyumbani kwao, na wote wa mjini walidhilika kabisa.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya