The chat will start when you send the first message.
1Ikawa siku zile habari zilimfikia Yudithi binti Merari, mwana wa Uzi, mwana wa Yusufu, mwana wa Ozieli, mwana wa Elkia, mwana wa Hanania, mwana wa Gideoni, mwana wa Rafaimu, mwana wa Ahitubu, mwana wa Elihu, mwana wa Eliabu, mwana wa Nathanaeli, mwana wa Samalieli, mwana wa Salasadai, mwana wa Israeli.
2Mumewe alikuwa Manase, mtu wa kabila yake na ukoo wake, naye alikufa wakati wa mavuno ya shayiri.
3Maana aliwasimamia wafunga miganda shambani, akapigwa na jua kichwani, akaanguka kitandani pake akafa katika mji wake Bethulia. Wakamzika pamoja na baba zake katika konde lililopo kati ya Dothaimu na Balamoni.
4Yudithi akakaa ujane nyumbani kwake muda wa miaka mitatu na miezi minne.
5Akajitengenezea hema juu ya dari ya nyumba yake, akajifunga magunia kiunoni na kuvaa nguo za matanga.[#Amu 3:20; 2 Fal 4:10]
6Akafunga siku zote za ujane wake ila makesha ya sabato tu, na sabato zenyewe, na siku za mwandamo wa mwezi na mikesha yake, na sikukuu na siku za furaha za nyumba ya Israeli.
7Naye sura yake ilikuwa nzuri mno, ya kupendeza macho sana; tena mumewe Manase alikuwa amemwachia dhahabu na fedha na watumwa na wajakazi wa wanyama na mashamba, naye alikaa pale penye mashamba yake.
8Wala hakuna aliyemsingizia neno lolote, kwa kuwa alimcha Mungu sana.
9Yudithi aliyasikia maneno mabaya ya watu waliyomwambia mkuu wa mji walipokuwa wakizimia kwa kiu, akayasikia maneno yote ya Uzia aliyowajibu, jinsi alivyowaapia ya kuwa atautoa mji kwa Waashuri baada ya siku tano.
10Akamtuma mjakazi wake kuwaita Uzia na Chabrisi, na Charmisi, na wakuu wa mji wake.
11Wakafika kwake, akawaambia; Nisikilizeni sasa, enyi wakuu wa wenyeji wa Bethulia, maana neno lenu mlolisema leo mbele ya watu silo jema, nanyi mmeuweka uapo mliouapa kati ya Mungu na ninyi, na kuahidi kuutoa mji kwa adui zetu, isipokuwa katika siku hizi Mungu awageukieni na kuwasaidia.
12Basi, ninyi ni nani mliomjaribu Mungu leo, na kusimama mahali pa Mungu katikati ya watu?[#Kum 6:16; Ayu 38:2]
13Mkimjaribu Mungu hamtajua kitu.
14Ninyi hamwezi kuupima moyo wa binadamu wala kuyajua mawazo yake; mtawezaje, basi, kumchungua Mungu aliyeviumba hivi vyote, mjue nia yake na kuyafahamu mawazo yake? Hasha, ndugu zangu, msimkasirishe BWANA![#Rum 11:33-34; 1 Kor 2:11]
15Maana, kama hana nia ya kutusaidia katika siku tano hizi, ana uweza wa kutulinda wakati apendao, au kutuharibu usoni pa adui zetu.
16Basi, msiyafunge mashauri ya BWANA Mungu wetu kwa ahadi; maana Mungu si kama binadamu atishwe, wala kama mwanadamu ageuzwe kwa maombi.
17Kwa hiyo tuungojee wokovu utokao kwake, na tumwite Mungu atusaidie, naye ataisikia sauti yetu kama akioana vema.
18Kwa sababu hakutokea mtu katika zamani zetu, wala hakuna wa kwetu leo, katika kabila yetu au ukoo wetu au jamaa yetu au mji wetu, amwabuduye mungu aliyefanyizwa kwa mikono, kama ilivyotendeka katika zamani zilizopita.
19Ilikuwa kwa sababu hiyo baba zetu walitolewa kwa upanga na kutekwa, wakaanguka kwa maangamizo mbele ya adui zetu.
20Lakini sisi hatujui mungu mwingine ila Yeye; kwa hiyo twatumaini kwamba hatatudharau sisi, wala mtu yeyote wa taifa letu.
21Bali sisi tukiwafuata hao, Yuda yote itakaa ukiwa, na patakatifu petu patatekwa, naye atatupatiliza unajisi uliopapata.
22Hata mauaji ya ndugu zetu, na utumwa wa nchi, na ukiwa wa urithi wetu, ataurudisha juu ya vichwa vyetu katikati ya mataifa tutakapokaa utumwani.
23Nasi tutakuwa chukizo na lawama machoni pao wanaotumiliki, kwa kuwa utumwa wetu hautakuwa na manufaa, bali Mungu ataufanya kuwa fedheha.
24Basi sasa, ndugu, tuwe mfano mwema kwa ndugu zetu, maana roho yao inatuinamia na patakatifu, na nyumba, na madhabahu vinatutegemea.
25Zaidi ya hayo, tumshukuru BWANA Mungu wetu anayetujaribu kama alivyowajaribu baba zetu pia.
26Yakumbukeni yote aliyomtendea Abrahamu, na majaribu yote aliyomjaribia Isaka, na yote yaliyompata Yakobo katika Mesopotamia ya Shamu alipowachunga kondoo za mjomba wake Labani.[#Mwa 22:1-18; 29:1—31:55]
27Maana hakutujaribu sisi kwa moto kama alivyowajaribu wao ili kuichungua mioyo yao; wala hakulipiza kisasi juu yetu; ila BWANA huwapiga wale wanaomkaribia kusudi awaadilishe.
28Uzia akamwambia, Yote uliyoyasema umesema kwa moyo mwema, wala hakuna awezaye kuyakana maneno yako.
29Wala leo si siku ya kwanza ya kudhihirika busara yako, ila tangu mwanzo wa siku zako watu wote wamejua maarifa yako, kwa kuwa welekevu wa moyo wako ni mwema.
30Lakini watu walikuwa wanaumia sana kwa kiu, nao walitushurutisha kufanya kama tulivyosema, na kujifunga kwa uapo ambao hatutauvunja.
31Basi sasa utuombee, maana u mwanamke mwema, na BWANA atatuletea mvua kuyajaza mabirika yetu, tusizidi kuzimia.
32Yudithi akawaambia, Nisikilizeni, nami nitafanya jambo litakalokumbukwa katika taifa letu kwa vizazi vyote.
33Mtasimama mlangoni leo usiku, nami nitatoka na mjakazi wangu; na katika zile siku, ambazo mlisema baada yake mtautoa mji kwa adui zetu, BWANA atamsaidia Israeli kwa mkono wangu.
34Lakini msiniulize nitakavyofanya, kwa sababu sitawaambieni hata yote nitakayofanya yatimizwe.
35Uzia na viongozi wakamwambia, Nenda zako kwa amani, na BWANA Mungu awe pamoja nawe alipize kisasi juu ya adui zetu.
36Wakaondoka hemani wakarudi kwao.