The chat will start when you send the first message.
1Naye Yudithi alianguka kifudifudi akajitia majivu kichwani, akalifunua gunia alilovikwa; na wakati huo uvumba wa jioni ulikuwa ukifukizwa Yerusalemu katika nyumba ya Mungu. Yudithi akamlilia BWANA kwa sauti kuu, akisema:
2Ee BWANA, Mungu wa baba yangu Simeoni, ulitia upanga mkononi mwake ili alipize kisasi wale wageni walioulegeza mshipi wa msichana kumharibu, na kulifunua paja lake kumwaibisha, na kulinajisi tumbo lake kumlaumu; maana wewe uliamuru lisitendeke, nao wakalitenda.[#Mwa 34:1-31]
3Kwa hiyo uliwatoa wakuu wao wauawe, na kitanda chao kiwe chekundu kwa damu, kile kitanda kilichofedheheka kwa ajili yake aliyedanganywa. Ukapiga watumwa pamoja na mabwana zao, na mabwana pamoja na viti vyao vya enzi;
4ukatoa wake zao kuwa mateka na binti zao kuwa watumwa, na mali yao yote kugawanywa katikati ya wana wako wapendwa, ambao walifanya ari kwa ajili yako, wakichukizwa kwa unajisi wa damu yao, wakaomba msaada kwako. Ee Mungu, Mungu wangu, nisikilize mimi pia, niliye mjane.
5Maana yaliyoyatangulia hayo uliyatenda Wewe, na hayo pia, na mambo yaliyofuata; umeyaazimia mambo yaliyopo sasa, na yatakayokuja; na yale uliyoyaazimia yakatendeka.
6Naam, mambo uliyoyakusudia yalisimama usoni pako yakasema, Tazama, sisi hapa. Maana njia zako zote zimeandaliwa, na hukumu zako hutolewa kwa kujua yote.
7Basi, tazama, Waashuri wameongezewa nguvu; wamejitukuza kwa farasi na wapanda farasi, na kujisifia wingi wa askari wao; wameweka tumaini lao kwa ngao na mkuki na upinde na kombeo; wala hawajui ya kuwa Wewe u BWANA uzivunjaye zana za vita;
8BWANA ndilo jina lako. Ziangushe nguvu zao kwa uweza wako, ulishushe jeuri lao katika ghadhabu yako; maana wamekaza nia yao kupanajisi patakatifu pako na kulitia uchafu hema linamokaa jina lako tukufu, na kuivunja kwa upanga pembe ya madhabahu yako.
9Uangalie kiburi chao; uwamwagie hasira yako kichwani; tia mkononi mwangu, mimi mjane, uwezo wa kutimiza azimio langu.
10Kwa hila ya midomo yangu, mpige mtumwa pamoja na mkuu, na mkuu pamoja na mtumwa wake; shusha fahari yao kwa mkono wa mwanamke.
11Maana uweza wako haumo katika wingi wa watu, wala nguvu yako katika mashujaa; ila Wewe u Mungu wao waliotaabika; msaidizi wao walioonewa.
12U tegemeo lao walio dhaifu; mlinzi wao walioachwa; mwokozi wao wasio na tumaini. Naam, Mungu wa baba yangu, Mungu wa urithi wa Israeli, BWANA wa mbingu na nchi, Muumba wa maji yote, Mfalme wa kila kiumbe, isikilize sala yangu.
13Fanya maneno yangu na hila yangu kuwa jeraha lao na pigo lao waliokusudia mabaya juu ya agano lako na nyumba yako takatifu, na juu ya mlima Sayuni na nyumba ya urithi wa watoto wako.[#Estk 4:17s-17t]
14Ulijulishe taifa lako na kila kabila kwamba wewe ndiwe Mungu, Mungu wa uweza wote na nguvu zote, wala hakuna alilindaye taifa la Israeli ila Wewe tu.