Yeremia 1

Yeremia 1

1Maneno ya Yeremia, mwana wa Hilkia, mmoja wa makuhani waliokuwa katika Anathothi, katika nchi ya Benyamini;[#Yos 21:18]

2ambaye neno la BWANA lilimjia katika siku za Yosia, mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda, katika mwaka wa kumi na tatu wa kutawala kwake.[#2 Pet 1:21; Yer 25:3; 2 Fal 22:3—23:27; 2 Nya 34:8—35:19]

3Tena lilikuja siku za Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, hadi mwisho wa mwaka wa kumi na mmoja wa Sedekia, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda; hata wakati ulipochukuliwa mateka Yerusalemu, katika mwezi wa tano.[#Yer 39:2; 52:12; 2 Fal 25:8; 2 Fal 23:36—24:7; 24:18—25:21; 2 Nya 36:5-8,11-21]

Kuitwa na kutumwa kwa Yeremia

4Neno la BWANA lilinijia, kusema,

5Kabla sijakuumba katika tumbo nilikujua, na kabla hujatoka tumboni, nilikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.[#Lk 1:15]

6Ndipo niliposema, Aa, Bwana MUNGU! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto.[#Kut 4:10]

7Lakini BWANA akaniambia, Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru.[#Kut 7:1,2; Eze 2:3,4; Mt 28:20; Mk 16:15,16; Hes 22:20; 1 Fal 22:14]

8Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema BWANA.[#Kut 3:12; Kum 31:6; Mdo 26:17]

9Ndipo BWANA akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa changu; BWANA akaniambia, Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako;[#Isa 6:7; 51:16]

10angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.[#1 Fal 17:1; Yer 25:15; Ufu 11:3-6; 2 Kor 10:4]

11Tena neno la BWANA likanijia, kusema, Yeremia, waona nini? Nikasema, Naona ufito wa mlozi.

12Ndipo BWANA akaniambia, Umeona vema, kwa maana ninaliangalia neno langu, ili nilitimize.[#Kum 32:35]

13Neno la BWANA likanijia mara ya pili, kusema, Waona nini? Nikasema, Naona sufuria lenye maji yatokotayo, na mdomo wake unaelekea toka upande wa kaskazini.

14Ndipo BWANA akaniambia, Toka kaskazini mabaya yatatokea, na kuwapata watu wote wakaao katika nchi hii.

15Kwa kuwa, tazama, nitaziita jamaa zote za falme za kaskazini, asema BWANA; nao watakuja, na kuweka kila mtu kiti chake cha enzi mbele ya mahali pa kuingilia malango ya Yerusalemu, na kuzielekea kuta zake pande zote, na kuielekea miji yote ya Yuda.[#Yer 39:3]

16Nami nitatamka hukumu zangu juu yao kutokana na uovu wao wote; kwa kuwa wameniacha mimi, wakaifukizia uvumba miungu mingine, wakaziabudu kazi za mikono yao wenyewe.[#Law 26:15; Yer 4:12; Kum 28:20]

17Haya basi, wewe jifunge viuno, ukaondoke ukawaambie maneno yote niliyokuamuru; usifadhaike kwa ajili yao, nisije nikakufadhaisha wewe mbele yao.[#1 Fal 18:46; Kut 3:12]

18Maana, tazama, nimekufanya leo kuwa mji wenye boma, na nguzo ya chuma, na kuta za shaba, juu ya nchi yote; juu ya wafalme wa Yuda, na juu ya wakuu wake, na juu ya makuhani wake, na juu ya watu wa nchi hii.

19Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, asema BWANA, ili nikuokoe.[#Hes 14:9; Zab 27:1; Rum 8:31]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya