The chat will start when you send the first message.
1Basi Pashuri, mwana wa Imeri, kuhani, aliyekuwa msimamizi mkuu katika nyumba ya BWANA, alimsikia Yeremia alipokuwa akitoa unabii huo.[#1 Nya 24:14]
2Ndipo Pashuri akampiga Yeremia, nabii, akamtia katika mkatale, uliokuwa pale penye lango la juu la Benyamini, lililokuwa katika nyumba ya BWANA.
3Hata ikawa, asubuhi, Pashuri huyo akamtoa Yeremia katika mkatale. Ndipo Yeremia akamwambia, BWANA hakukuita jina lako Pashuri, bali Magor-misabibu.[#20:3 tafsiri yake ni Hofu iko pande zote.]
4Maana BWANA asema hivi, Tazama, nitakufanya kuwa hofu kuu kwa nafsi yako, na kwa rafiki zako wote; nao wataanguka kwa upanga wa adui zao, na macho yako yataona hayo; nami nitatia Yuda yote katika mikono ya mfalme wa Babeli, naye atawachukua mateka mpaka Babeli, na kuwaua kwa upanga.[#Ayu 18:11; Yer 6:25; 46:5]
5Tena mali zote za mji huu, na mapato yake yote, na vitu vyake vya thamani vyote pia, naam, hazina zote za wafalme wa Yuda, nitavitia katika mikono ya adui zao, watakaowateka nyara, na kuwakamata, na kuwachukua mpaka Babeli.[#2 Fal 20:17; Yer 3:24]
6Na wewe, Pashuri, na watu wote wanaokaa katika nyumba yako, mtakwenda utumwani; nawe utafika Babeli, na huko utakufa, na huko utazikwa, wewe, na rafiki zako wote, uliwatolea unabii wa uongo.[#Yer 14:13,14; 28:15]
7Ee BWANA, umenihadaa, nami nimehadaika; wewe una nguvu kuliko mimi, ukashinda; nimekuwa kitu cha kuchekesha, mchana kutwa; kila mtu hunidhihaki.[#Yer 1:6,7; Ayu 12:4; Omb 3:14]
8Maana kila ninenapo napiga kelele, nalia, Dhuluma na uharibifu! Kwa kuwa neno la BWANA limefanywa shutumu kwangu, na dhihaka, mchana kutwa.[#Yer 6:7]
9Nami nikisema, Sitamtaja, wala sitasema tena kwa jina lake; basi, ndipo moyoni mwangu kumekuwamo kama moto uwakao, uliofungwa ndani ya mifupa yangu, nami nimechoka kwa kustahimili, wala siwezi kujizuia.[#1 Fal 19:10; Zab 39:3; Ayu 32:18,19,20; Mdo 18:5]
10Maana nimesikia shutuma za watu wengi; hofu ziko pande zote. Rafiki zangu wote, wanaonivizia nisite, husema, Mshitaki, nasi tutamshitaki, huenda akahadaika, nasi tutamshinda, tutajilipiza kisasi kwake.[#Zab 31:13]
11Lakini BWANA yuko pamoja nami, mfano wa shujaa mwenye kutisha; kwa hiyo hao wanaonionea watajikwaa, wala hawatashinda; watatahayarika sana. Kwa sababu hawatafaulu wataona aibu ya milele, ambayo haitasahauliwa kamwe.[#Isa 41:13; Rum 8:31; Yer 1:8; 15:20; 17:18]
12Lakini, Ee BWANA wa majeshi, wewe wawajaribu wenye haki, waona fikira na mioyo, nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu.[#Yer 11:20; 17:10; Zab 54:7; 50:10; 109:6-20; Yer 12:3; 17:18]
13Mwimbieni BWANA; msifuni BWANA;[#Zab 35:9; Yak 2:5,6]
Kwa maana ameiponya roho ya mhitaji
Katika mikono ya watu watendao maovu.
14Na ilaaniwe siku niliyozaliwa, isibarikiwe siku ile aliyonizaa mama yangu.[#Yer 15:10; Ayu 3:1-19]
15Na alaaniwe mtu yule aliyemletea baba yangu habari, akisema, Umezaliwa mtoto wa kiume; na kumfurahisha sana.
16Mtu huyo na awe kama miji ile, ambayo BWANA aliiangamiza, asijute; na asikie kilio asubuhi, na kelele za fujo adhuhuri;[#Mwa 19:25; Yer 18:22]
17kwa sababu hakuniua nilipotoka tumboni, na hivyo mama yangu angekuwa kaburi langu, na mimba yake sikuzote nzito.[#Ayu 3:10]
18Nilitoka tumboni kwa sababu gani, kuona taabu na huzuni, hata siku zangu ziharibike katika aibu?[#Ayu 3:20; Omb 3:1]