Ayubu 19

Ayubu 19

Ayubu ajibu: Najua mkombozi wangu yu hai

1Ndipo Ayubu akajibu, na kusema,

2Je! Mtanichukiza nafsi yangu hata lini,[#1 Sam 1:6; Zab 6:2,3]

Na kunivunjavunja kwa maneno?

3Mara kumi hizi mmenishutumu;

Hamwoni haya kunifanyia mambo magumu.

4Ingawaje nimekosa,[#Zab 19:12; Eze 18:4]

Kosa langu hukaa kwangu mwenyewe.

5Ikiwa mtajitukuza juu yangu,[#Zab 38:16; Mik 7:8]

Na kufanya aibu yangu kuwa hoja juu yangu;

6Jueni basi kuwa Mungu amenipotosha,[#Omb 1:13]

Na kunizingira kwa wavu wake.

7Tazama, nalia, Udhalimu, lakini sisikiwi;

Naulilia msaada, wala hapana hukumu.

8Yeye ameiziba njia yangu nisipate kupita,[#Omb 3:7,8]

Na kutia giza katika mapito yangu.

9Amenivua utukufu wangu,

Na kuiondoa taji kichwani mwangu.

10Amenibomoa pande zote, nami nimetoweka;

Na tumaini langu ameling'oa kama mti.

11Tena ameziwasha ghadhabu zake juu yangu,[#Kum 32:22]

Akanihesabia kuwa mmoja katika watesi wake.

12Majeshi yake husongea pamoja, na kunipandishia njia yao,[#Zab 34:19]

Na kupiga kambi kuizunguka hema yangu.

13Amewaweka ndugu zangu mbali nami,[#Zab 31:11; Mt 26:56; 2 Tim 4:16]

Na wanijuao wametengwa nami kabisa.

14Watu wa ukoo wangu wamekoma,

Na marafiki zangu niwapendao wamenisahau.

15Wakaao nyumbani mwangu, na vijakazi vyangu, wanihesabu kuwa mgeni;

Wageni nyumbani mwangu, na vijakazi wangu, wanihesabu kuwa mgeni.

16Namwita mtumishi wangu, wala haniitikii,

Ingawa namsihi kwa kinywa changu.

17Pumzi zangu zimekuwa kinyaa kwa mke wangu,

Nami ni machukizo kwa ndugu zangu.

18Hata watoto wadogo hunidharau;

Nikiondoka, huninena.

19Marafiki zangu wote wa dhati wanichukia;

Na hao niliowapenda wamenigeukia.

20Mfupa wangu unagandamana na ngozi yangu na nyama yangu,

Nami nimeokoka na ngozi ya meno yangu tu.

21Nihurumieni, nihurumieni, enyi rafiki zangu,

Kwa maana mkono wa Mungu umenigusa.

22Mbona ninyi mnaniudhi kama Mungu,

Wala hamkutosheka na nyama yangu?

23Laiti maneno yangu yangeandikwa sasa!

Laiti yangeandikwa kitabuni!

24Yakachorwa katika mwamba milele,

Kwa kalamu ya chuma na risasi.

25Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai,

Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi.

26Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi,

Lakini, pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu;

27Nami nitamwona mimi nafsi yangu,

Na macho yangu yatamtazama, wala si mwingine.

Mtima wangu unazimia ndani yangu!

28Kama mkisema, Jinsi tutakavyomwudhi!

Kwa kuwa shina la jambo hili limeonekana kwake;

29Uogopeni upanga;

Kwa maana adhabu za upanga zina ghadhabu,

Mpate kujua ya kwamba hukumu iko.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya