The chat will start when you send the first message.
1Tena ilitukia siku moja hao wana wa Mungu walipokwenda kujiweka mbele za BWANA, Shetani naye akaenda kati yao, ili kujiweka mbele za BWANA.
2BWANA akamwuliza Shetani, Umetoka wapi? Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Natoka katika kuzungukazunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo.
3BWANA akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hakuna hata mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu; naye hata sasa anashikamana na utimilifu wake, ijapokuwa ulinichochea juu yake, ili nimwangamize pasipokuwa na sababu.[#Ayu 27:5,6; Yak 1:12; 1 Pet 1:7; Mwa 22:1; Mt 7:11; Yn 9:2]
4Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Ngozi kwa ngozi, naam, yote aliyo nayo mtu atayatoa kwa ajili ya uhai wake.
5Lakini sasa nyosha mkono wako, uuguse mfupa wake na nyama yake, naye atakukufuru mbele za uso wako.[#Ayu 19:20; Zab 32:3,4]
6BWANA akamwambia Shetani, Tazama, yeye yumo mkononi mwako; lakini tunza tu uhai wake.
7Basi Shetani akatoka mbele za uso wa BWANA, akampiga Ayubu na majipu mabaya tangu wayo wa mguu hadi utosi wa kichwa.
8Naye akashika kigae cha kujikunia; akaketi majivuni.[#2 Sam 13:19; Ayu 42:6; Mt 11:21]
9Ndipo mkewe akamwambia, Je! Wewe hata sasa washikamana na utimilifu wako? Mkufuru Mungu, ufe.[#Mwa 3:6; 2 Fal 6:33; Mal 3:14; Ayu 21:15]
10Lakini yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! Tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya? Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake.[#2 Sam 19:28; Ayu 1:21; Omb 3:38-41; Yn 18:11; Rum 12:12; Ebr 12:9-11; Zab 39:1; Yak 1:12]
11Basi ikawa hao marafiki watatu wa Ayubu walipopata habari ya mabaya hayo yote yaliyomfikia, wakaja kila mtu kutoka mahali pake; nao ni Elifazi Mtemani, na Bildadi Mshuhi, na Sofari Mnaamathi; wakapatana pamoja ili waende kumfariji Ayubu na kumtuliza moyo.[#Mwa 36:11; Yer 49:7; Mwa 25:2; Ayu 42:11; Rum 12:15]
12Basi walipoinua macho yao, wakiwa bado kwa mbali, wasimtambue, wakainua sauti zao na kulia; kila mmoja akararua joho lake, wakarusha mavumbi juu ya vichwa vyao kuelekea mbinguni.[#Neh 9:1; Omb 2:10]
13Kisha wakaketi ardhini pamoja naye muda wa siku saba, mchana na usiku, wala hapana mmoja aliyenena naye neno lolote; kwa maana waliona ya kuwa mashaka yake aliyo nayo ni makuu mno.[#Mwa 50:12]