Ayubu 28

Ayubu 28

Hekima inapopatikana

1Hakika kuna shimo wachimbako fedha,

Na mahali wapatapo dhahabu waisafishayo.

2Chuma hufukuliwa katika ardhi,

Na shaba huyeyushwa katika mawe.

3Binadamu hukomesha giza;[#Mit 2:4; Mhu 1:13]

Huyatafutatafuta hata katika maeneo ya mbali,

Mawe ya madini katika giza, giza kuu.

4Hufukua shimo mbali na makao ya watu;

Husahauliwa na nyayo zipitazo;

Huning'inia mbali na watu, huyumbayumba huku na huko.

5Katika ardhi ndimo kitokeamo chakula;

Na chini yake hupinduliwa kama kwa moto.

6Mawe yake ni mahali zipatikanapo yakuti;

Nayo ina mchanga wa dhahabu.

7Njia ile hapana ndege mkali aijuaye,

Wala jicho la tai halijaiona;

8Wanyama wakali wajivunao hawajaikanyaga,

Wala simba mkali hajaipita.

9Huunyoshea mwamba wa gumegume mkono wake;

Huipindua milima hata misingi yake.

10Hukata mifereji kati ya majabali;

Na jicho lake huona kila kito cha thamani.

11Hufunga vijito visichuruzike;

Na kitu kilichositirika hukifunua.

12Bali hekima itapatikana wapi?[#Ayu 11:7,8; Zab 139:6; Mhu 7:24]

Na mahali pa ufahamu ni wapi?

13Mwanadamu hajui thamani yake,[#Mit 3:15]

Wala haionekani katika nchi ya walio hai.

14Vilindi vyasema, Haimo ndani yangu;[#Rum 11:33]

Na bahari yasema, Haiko kwangu.

15Haipatikani kwa dhahabu,[#Mit 3:13,14]

Wala fedha haitapimwa iwe thamani yake.

16Haiwezi kutiwa thamani kwa dhahabu ya Ofiri,

Wala kwa shohamu ya thamani nyingi, wala kwa yakuti samawi.

17Dhahabu na vioo haviwezi kulinganishwa nayo;

Wala kubadili kwake hakutakuwa kwa vyombo vya dhahabu safi.

18Havitatajwa fedhaluka wala bilauri;

Naam, kima cha hekima chapita marijani.

19Yakuti ya rangi ya manjano ya Kushi haitasawazishwa nayo,

Wala haitatiwa kima kwa dhahabu safi.

20Basi hekima yatoka wapi?

Na mahali pa ufahamu ni wapi?

21Kwa kuwa imefichwa mbali na macho ya wote walio hai,

Na kusitirika na ndege wa angani.

22Uharibifu na Mauti husema,

Tumesikia habari zake kwa masikio yetu.

23Mungu ndiye aijuaye njia yake,[#Mdo 15:18; Ebr 4:13]

Naye anajua mahali pake.

24Maana anatazama hata miisho ya nchi,[#Mit 15:3]

Na kuona chini ya mbingu nzima.

25Apate kuufanyia upepo uzito wake;[#Zab 135:7]

Naam, anayapima maji kwa kipimo.

26Hapo alipoiwekea mvua amri,[#Ayu 38:25; Zab 148:8; Yer 14:22]

Na njia kwa umeme wa radi.

27Ndipo alipoiona na kuitangaza;

Aliithibitisha, naam, na kuichunguza.

28Kisha akamwambia mwanadamu,[#Zab 111:10; Mit 1:7; 9:10; Kum 29:29; 4:6]

Tazama, kumcha Bwana ndiyo hekima,

Na kujitenga na uovu ndio ufahamu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya