Ayubu 32

Ayubu 32

Elihu awakemea marafiki wa Ayubu

1Basi hao watu watatu wakaacha kumjibu Ayubu, kwa sababu alikuwa mwenye haki machoni pake mwenyewe.

2Ndipo zikawaka hasira za huyo Elihu mwana wa Barakeli, Mbuzi, katika jamaa ya Ramu, juu ya Ayubu, kwa sababu alikuwa amejipa haki mwenyewe zaidi ya Mungu.[#Mwa 22:21]

3Tena hasira zake ziliwaka juu ya hao rafiki zake watatu kwa sababu hawakupata jawabu, lakini wamemhukumia Ayubu makosa.

4Basi huyo Elihu alikuwa anangoja ili anene na Ayubu, kwa sababu hao wengine walikuwa wazee kuliko yeye.

5Hata Elihu alipoona kuwa hapana jawabu katika vinywa vya watu hao watatu, hasira zake ziliwaka.

6Basi Elihu mwana wa Barakeli, Mbuzi, akajibu, na kusema,

Mimi ni kijana, na ninyi ni wazee sana;

Kwa hiyo nilijizuia, nisithubutu kuwaonesha nionavyo.

7Nilisema, Yafaa siku ziseme,[#Ayu 8:8,9]

Na wingi wa miaka ufundishe hekima.

8Lakini hakika imo roho ndani ya mwanadamu,[#1 Fal 3:9]

Na pumzi ya Mwenyezi ndiyo impayo ufahamu.

9Sio wakuu walio wenye hekima,[#1 Kor 1:21]

Wala sio wazee watambuao haki.

10Basi nilisema, Nisikilizeni mimi;

Mimi nami nitawaonesha nionavyo.

11Tazama, niliyangojea maneno yenu,

Nilizisikiliza nisikie hoja zenu,

Hapo mlipokitafuta mtakalonena.

12Naam, niliwasikiza ninyi,[#Mit 18:13]

Na tazama, hapana mmoja aliyemshinda Ayubu,

Wala kumjibu maneno yake, kati yenu.

13Jitunzeni msiseme, Sisi tumepata hekima;[#Yer 9:23]

Mungu huenda akamshinda, si mtu;

14Kwa kuwa yeye hajayaelekeza maneno yake kwangu;

Wala sitamjibu mimi kwa maneno yenu.

15Wameshangaa, hawajibu tena;

Hawana neno la kusema.

16Na mimi, je! Ningoje, kwa sababu hawaneni,

Kwa sababu wasimama kimya, wala wasijibu tena;

17Mimi nami nitajibu sehemu yangu,

Mimi nami nitaonesha nionavyo.

18Kwa kuwa nimejaa maneno;

Roho iliyo ndani yangu hunihimiza.

19Tazama, tumbo langu ni kama divai iliyozibwa;

Kama viriba vipya liko karibu kupasuka.

20Nitanena, ili nipate kutulia;

Nitafunua midomo yangu na kujibu.

21Tafadhali, nisiupendelee uso wa mtu;

Wala sitajipendekeza kwa mtu yeyote.

22Kwa kuwa mimi sijui kujipendekeza;[#Mdo 12:22,23]

Au Muumba wangu angeniondoa kwa upesi.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya