Ayubu 34

Ayubu 34

Elihu atangaza haki ya Mungu

1Tena Elihu akajibu na kusema,

2Sikilizeni maneno yangu, enyi wenye hekima;

Tegeni masikio kwangu, ninyi mlio na maarifa.

3Kwa kuwa sikio huyajaribu maneno,

Kama vile kaakaa lionjavyo chakula.

4Na tujichagulie yaliyo ya uelekevu;

Na tujue wenyewe yaliyo mema.

5Kwani Ayubu amesema, Mimi ni mwenye haki,[#Ayu 33:9; 27:2]

Naye Mungu ameniondolea haki yangu;

6Nijapokuwa mwenye haki, nimehesabiwa kuwa mwongo;[#Ayu 9:17]

Jeraha langu haliponyeki, nijapokuwa sina makosa.

7Je! Ni mtu gani mfano wa Ayubu,

Anywaye mzaha kama maji?

8Atembeaye na hao watendao uovu,

Na kwenda pamoja na watu wabaya.

9Kwa kuwa amenena, Haimfai mtu lolote[#Ayu 9:22]

Kujifurahisha na Mungu.

10Kwa hiyo nisikilizeni, enyi wenye fahamu;[#Mwa 18:25; Kum 32:4]

Mungu asidhaniwe kutenda udhalimu;

Wala Mwenyezi kufanya uovu.

11Kwani atamlipa binadamu kwa kazi yake,[#Zab 62:12; Mit 24:12; Mt 16:27; Ufu 22:12]

Naye atamfanya kila mtu kuona kulingana na njia zake.

12Naam, hakika, Mungu hatatenda mabaya,

Wala Mwenyezi hatapotosha hukumu.

13Ni nani aliyemwagiza kuiangalia dunia?

Au ni nani aliyemwekea ulimwengu huu wote?

14Kama akimwekea mtu moyo wake,[#Mhu 12:7]

Akijikusanyia roho yake na pumzi zake;

15Wenye mwili wote wangeangamia pamoja,

Nao wanadamu watarejea tena kuwa mavumbi.

16Ikiwa una ufahamu, sikia neno hili;

Isikilize sauti ya maneno yangu.

17Je! Atatawala mtu aichukiaye haki hata mmoja?[#Mwa 18:25]

Nawe, je! Utamhukumia mkosa aliye na haki na mwenye nguvu?

18Je! Inafaa kumwambia mfalme, Wewe u mwovu?

Au kuwaambia wakuu, Ninyi ni wabaya?

19Sembuse yeye huwajali nyuso za wakuu,[#Kum 10:17]

Wala hawajali matajiri kuliko maskini?

Kwani wote ni kazi ya mikono yake,

20Hufa ghafla, hata usiku wa manane;

Watu hutikisika na kwenda zao,

Nao mashujaa huondolewa pasipo mkono wa mtu.

21Kwani macho yake yako juu ya njia za mtu,

Naye huziona hatua zake zote.

22Hapana hofu ya giza kuu,

mahali wawezapo kujificha watendao udhalimu.

23Kwani yeye hana haja ya kumfikiria mtu zaidi,[#Ezr 9:13]

ili aende mbele za Mungu ahukumiwe.

24Yeye huwavunjavunja mashujaa pasipo kuwachunguza,

Na kuwaweka wengine mahali pao.

25Kwa sababu hiyo yeye huyatafiti matendo yao;

Naye huwapindua usiku, wakaangamia.

26Yeye huwapiga kwa sababu ya uovu wao,

Waziwazi mbele ya macho ya wengine;

27Kwa sababu walikengeuka, wasimfuate yeye,

Wasikubali kuzishika njia zake hata moja;

28Hata wakafanya kilio cha maskini kumfikia,[#Mhu 5:8; Yak 5:4; Kut 22:23; Zab 34:17; Mhu 3:16,17]

Naye akasikia kilio cha hao wateswao.

29Akitoa utulivu yeye, ni nani awezaye kuhukumia makosa?

Akificha uso wake, ni nani awezaye kumtazama?

Kama hufanyiwa taifa, au mtu mmoja, ni sawasawa;

30Ili huyo mpotovu asitawale,[#Mit 29:2-12; 1 Fal 12:28-30]

Wala pasiwe na wa kuwatega watu.

31Kwani kuna mtu aliyemwambia Mungu,

Mimi nimevumilia kurudiwa, ingawa sikukosa;

32Nisiyoyaona nifundishe wewe;

Kama nimefanya uovu sitafanya tena?

33Je! Malipo yake yatakuwa kama upendavyo wewe, hata ukayakataa?

Kwani yakupasa wewe kuchagua, si mimi;

Kwa sababu hiyo sema uyajuayo.

34Watu walio na akili wataniambia,

Naam, kila mtu mwenye hekima anisikiaye;

35Huyo Ayubu amesema pasipo maarifa,[#Ayu 38:2]

Na maneno yake hayana hekima.

36Laiti Ayubu angejaribiwa hadi mwisho,

Kwa kuwa amejibu kama watu waovu.

37Maana huongeza uasi juu ya dhambi zake,

Apiga makofi kati yetu,

Na kuongeza maneno yake kinyume cha Mungu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya