Ayubu 9

Ayubu 9

Ayubu ajibu: Hakuna mpatanishi

1Ndipo Ayubu akajibu, na kusema,

2Kweli najua kuwa ndivyo hivyo;[#Ayu 4:17; Zab 143:2; Rum 3:20]

Lakini mtu huwaje mwenye haki mbele za Mungu?

3Kama akipenda kushindana naye,

Hawezi kumjibu neno moja katika elfu.

4Yeye ni mwenye hekima moyoni, na mwenye uwezo katika nguvu;

Ni nani aliyejifanya kuwa mgumu juu yake, naye akafanikiwa?

5Aiondoaye milima, nayo haina habari,

Akiipindua katika hasira zake.

6Aitikisaye dunia itoke mahali pake,[#Isa 2:19-21; Hag 2:6,21; Ebr 12:26]

Na nguzo zake hutetemeka.

7Aliamuruye jua, nalo halichomozi;

Nazo nyota huzipiga mhuri.

8Ambaye peke yake ni mwenye kuzitandika mbingu,

Na kuyakanyaga mawimbi ya bahari.

9Yeye afanyaye hizo nyota za Dubu, na Orioni, na hicho Kilimia,[#Ayu 38:31; Amo 5:8; Mwa 1:16]

Na makundi ya nyota ya kusini.

10Atendaye mambo makuu yasiyochunguzika;

Naam, mambo ya ajabu yasiyohesabika.

11Tazama, yuaenda karibu nami, nisimwone;[#Ayu 23:8]

Tena yuapita kwenda mbele, nisimtambue.

12Tazama, yuanyakua, ni nani awezaye kumzuia?[#Isa 45:9; Yer 18:6]

Ni nani awezaye kumwuliza, Wafanya nini?

13Mungu haondoi hasira zake;

Hao wamsaidiao Rahabu huinama chini yake.

14Je! Mimi nitamjibuje,

Na kuyachagua maneno yangu kuhojiana naye?

15Ambaye, nijapokuwa mimi ni mwenye haki, siwezi kumjibu;[#Ayu 10:15]

Ni lazima nimwombe mshitaki wangu anihurumie.

16Kama ningemwita, naye akaniitikia;

Hata hivyo singeamini kuwa amesikiza sauti yangu.

17Yeye anipondaye kwa dhoruba,[#Ayu 2:3; Zab 25:3; Yn 9:3]

Na kuyaongeza majeraha yangu pasipokuwa na sababu.

18Haniachi nipate kuvuta pumzi,

Lakini hunijaza uchungu.

19Kama tukitaja nguvu za mashujaa, tazama yupo hapo!

Kama tukitaja hukumu, ni nani atakayemwita mahakamani?

20Ingawa mimi ni mwenye haki, kinywa changu mwenyewe kitanihukumu;

Ingawa mimi ni mkamilifu, kitanishuhudia kuwa mimi ni mpotovu.

21Mimi ni mkamilifu; siangalii nafsi yangu;

Naudharau uhai wangu.

22Hayo yote ni mamoja; kwa hiyo nasema,[#Mhu 9:1,2; Eze 21:3; Lk 13:2-4]

Yeye huangamiza wakamilifu na waovu pia.

23Kama hilo pigo likiua ghafla,

Atayadhihaki majaribu yake asiye na kosa.

24Dunia imetiwa mkononi mwa waovu;[#2 Sam 15:30; Yer 14:4]

Yeye hufunika nyuso za waamuzi wake;

Kama si yeye, ni nani basi?

25Basi siku zangu zina mbio kuliko tarishi;

Zakimbia, wala hazioni mema.

26Zimepita kama merikebu ziendazo mbio;

Mfano wa tai ayashukiaye mawindo.

27Nikisema, Mimi nitasahau kuugua kwangu,

Nitaacha kununa uso nikachangamke moyo;

28Mimi ninayaogopa mateso yangu yote,[#Kut 20:7; Zab 130:3]

Najua kuwa hutanihesabu kuwa sina hatia.

29Nitahukumiwa kuwa ni mkosa;

Ya nini basi nitaabike bure?

30Ingawaje najiosha kwa maji ya theluji,

Na kuitakasa mikono yangu kwa sabuni;

31Lakini utanitupa shimoni,

Nami hata nguo zangu zitanichukia.

32Maana yeye si mtu, kama mimi, hata nimjibu,[#Mhu 6:10; Isa 45:9; Yer 49:19]

Hata tuwe mahakamani pamoja.

33Hapana mwenye kuamua katikati yetu,[#1 Sam 2:25]

Awezaye kutuwekea mkono sote wawili.

34Na aniondolee fimbo yake,

Na utisho wake usinitie hofu;

35Hapo Ndipo ningeweza kusema, pasipo kumwogopa;

Maana najua sivyo nilivyo nafsini mwangu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya