Yoeli 2

Yoeli 2

1Pigeni tarumbeta katika Sayuni,[#Hes 10:5; Zab 87:1; Oba 1:15; Sef 1:14]

Pigeni na kelele katika mlima wangu mtakatifu;

Wenyeji wote wa nchi na watetemeke;

Kwa maana siku ya BWANA inakuja.

Kwa sababu inakaribia;

2siku ya giza na huzuni, siku ya mawingu na giza kuu. Kama mapambazuko yakitandazwa juu ya milima, hao ni wakuu, tena wenye nguvu, mfano wao haukuwako kamwe, wala hautakuwako baada ya hao, hata katika miaka ya vizazi vingi.[#Amo 5:18; Yoe 1:6; Kut 10:14]

3Moto unaunguza vikali mbele yao; na nyuma yao miali ya moto inateketeza; hiyo nchi inafanana na bustani ya Edeni mbele yao, na nyuma yao imekuwa jangwa tupu; naam, hakuna aliyeokoka asipatikane nao.[#Zek 7:14]

4Kuonekana kwao ni kama kuonekana kwa farasi; na kama wapanda farasi ndivyo wanavyopiga mbio.[#Ufu 9:7-9]

5Kama mshindo wa magari ya vita juu ya vilele vya milima, ndivyo warukavyo; kama mshindo wa miali ya moto iunguzapo mabua makavu, kama mashujaa waliopangwa tayari kwa vita.

6Mbele yao watu wanahangaika; nyuso zote zimegeuka kuwa nyeupe kwa hofu.[#Yer 8:21]

7Hupiga mbio kama mashujaa; huupanda ukuta kama watu wa vita; nao huendelea mbele kila mmoja katika njia zake, wala hawapotoshi safu zao.

8Wala hapana mmoja amsukumaye mwenzake; huendelea mbele kila mmoja katika njia yake; hujifanyia njia kwa nguvu kati ya silaha, wala hawaachi kuifuata njia yao.

9Huurukia mji; hupiga mbio juu ya ukuta; hupanda na kuingia ndani ya nyumba; huingia madirishani kama aingiavyo mwizi.

10Nchi inatetemeka mbele yao; mbingu zinatetemeka; jua na mwezi hutiwa giza, na nyota huacha kuangaza;[#Ufu 8:12]

11naye BWANA anatoa sauti yake mbele ya jeshi lake; maana matuo yake ni makubwa sana; kwa maana yeye ni hodari atekelezaye neno lake; kwa kuwa siku ya BWANA ni kuu, yenye kitisho sana; naye ni nani awezaye kuistahimili?[#Yer 50:34; Hes 24:23; Mal 3:2; Ufu 6:17]

12Lakini hata sasa, asema BWANA, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuomboleza;[#Yer 4:1; Hos 12:6]

13rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie BWANA, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi kuadhibu.[#2 Fal 22:19; Zab 34:18; Isa 57:15; Mt 5:3,4; Kut 34:6; Yon 4:2]

14Ni nani ajuaye kwamba hatarudi na kugeuka, na kutuachia baraka nyuma yake, naam, sadaka ya unga, na sadaka ya kinywaji, kwa BWANA, Mungu wenu?[#Yos 14:12; Sef 2:3; Isa 65:8; Hag 2:19]

15Pigeni tarumbeta katika Sayuni,

Takaseni saumu, kusanyeni kusanyiko kuu;

16Kusanyeni watu, litakaseni kusanyiko,[#Kut 19:10; 2 Nya 20:13; 1 Kor 7:5]

Kusanyeni wazee, kusanyeni watoto,

Na hao wanyonyao maziwa;

Bwana arusi na atoke chumbani mwake,

Na bibi arusi katika hema yake.

17Hao makuhani, wahudumu wa BWANA, na walie[#Mt 23:35; Kut 32:11; Isa 37:20]

Kati ya patakatifu na madhabahu,

Na waseme, Uwaachilie watu wako, Ee BWANA,

Wala usiutoe urithi wako upate aibu,

Hata mataifa watawale juu yao;

Kwa nini waseme kati ya watu, Yuko wapi Mungu wao?

Majibu ya Mungu na ahadi yake

18Hapo ndipo BWANA alipoona wivu kwa ajili ya nchi yake, akawahurumia watu wake.[#Isa 42:13; Zek 1:14; Kum 32:36; Zab 103:13]

19BWANA akajibu, akawaambia watu wake; Tazameni, nitawaletea nafaka, na divai, na mafuta, nanyi mtashiba kwa vitu hivyo; wala sitawafanya tena kuwa aibu kati ya mataifa;[#Mal 3:10]

20lakini jeshi lililotoka kaskazini nitaliondolea mbali nanyi, nami nitalifukuza mpaka nchi ya ukame na ukiwa; sehemu yake iliyo mbele itaingia katika bahari ya mashariki, na sehemu yake iliyo nyuma itaingia katika bahari ya magharibi; na uvundo wake utapanda juu, na harufu yake mbaya itapanda juu, kwa sababu ametenda mambo makubwa.[#Kut 10:19; Kum 11:24]

21Ee nchi, usiogope; furahi na kushangilia; kwa kuwa BWANA ametenda mambo makuu.[#1 Yoh 4:18]

22Msiogope, enyi wanyama wa porini; maana malisho ya jangwani yanatoa miche, na huo mti unazaa matunda yake, mtini na mzabibu inatoa nguvu zake.[#Zek 8:12]

23Furahini, basi, enyi wana wa Sayuni, mkamfurahie BWANA, Mungu wenu; kwa kuwa yeye huwapa ninyi mvua ya masika, kwa kipimo cha haki, naye huwanyeshea mvua, mvua ya masika, na mvua ya vuli, kama awali.[#Zab 28:7; Isa 12:2-6; Hab 3:17,18; Zek 10:7; Law 26:4; Yak 5:7]

24Na sakafu za kupepetea zitajaa ngano, na mashinikizo yatafurika kwa divai na mafuta.

25Nami nitawarudishia hiyo miaka iliyoliwa na nzige, na parare, na madumadu, na tunutu, jeshi langu kubwa nililotuma kati yenu.

26Nanyi mtakula chakula tele na kushiba, na kulihimidi jina la BWANA, Mungu wenu, aliyewatendea mambo ya ajabu; na watu wangu hawatatahayari kamwe.[#Mik 6:14]

27Nanyi mtajua ya kuwa mimi ni katikati ya Israeli, na ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu, wala hakuna mwingine; na watu wangu hawatatahayari kamwe.[#Law 26:11; Isa 45:5]

Roho wa Mungu amiminiwa

28Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, wa kiume na wa kike, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono;[#Isa 44:3; Yn 7:39; Isa 54:13; Mdo 2:17-21; 21:9; #2:28 Katika Kiebrania ni Sura 3:1.]

29tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu.[#1 Kor 12:13; Gal 3:28]

30Nami nitaonesha mambo ya ajabu katika mbingu na katika dunia, damu, na moto, na minara ya moshi.[#Mk 13:24]

31Jua litageuzwa kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla haijaja hiyo siku ya BWANA iliyo kuu na itishayo.[#Mt 24:29; Mk 13:24-25; Lk 21:25; Ufu 6:12-13]

32Na itakuwa ya kwamba mtu awaye yote atakayeliita jina la BWANA ataponywa; kwa kuwa katika mlima Sayuni na katika Yerusalemu watakuwako watu watakaookoka, kama BWANA alivyosema; na katika mabaki, hao awaitao BWANA.[#Zab 50:15; Yer 33:3; Mdo 2:21; 1 Kor 1:2; Isa 46:13; 11:11; Oba 1:17; Rum 10:13; 9:27]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya