The chat will start when you send the first message.
1Basi ikawa hapo Adoni-sedeki, mfalme wa Yerusalemu, aliposikia jinsi Yoshua alivyouteka mji wa Ai na kuuharibu kabisa; kama alivyoufanyia mji wa Yeriko na mfalme wake, akaufanya hivyo Ai na mfalme wake; na jinsi wenyeji waliokaa Gibeoni walivyofanya amani na Israeli, na ya kwamba walikuwa kati yao;[#Yos 6:21; 8:22; 9:15]
2ndipo wakaogopa mno, kwa sababu Gibeoni ulikuwa ni mji mkubwa, kama ilivyo miji ya kifalme mmojawapo, tena kwa sababu ulikuwa ni mji mkubwa kupita Ai, tena watu wake wote walikuwa ni mashujaa.[#Kut 15:14-16; Kum 11:25; 28:10; Zab 48:4-6; Mit 1:26,27; Ebr 10:27,31; Ufu 6:15-17]
3Basi kwa hiyo Adoni-sedeki, mfalme wa Yerusalemu, akatuma ujumbe kwa Hohamu, mfalme wa Hebroni, na kwa Piramu, mfalme wa Yarmuthi, na kwa Yafia, mfalme wa Lakishi, na kwa Debiri, mfalme wa Egloni, akiwaambia,[#Mwa 23:2; Hes 13:22]
4Haya, kweeni mje kwangu, mnisaidie, tuupige Gibeoni; kwa sababu umefanya mapatano ya amani pamoja na Yoshua na wana wa Israeli.[#Yos 9:15]
5Ndipo hao wafalme watano wa Waamori, mfalme wa Yerusalemu, na mfalme wa Hebroni na mfalme wa Yarmuthi na mfalme wa Lakishi, na mfalme wa Egloni, wakakutana pamoja, kisha wakakwea, wao na majeshi yao yote, na kupiga kambi yao kinyume cha Gibeoni, na kuupiga vita.[#Yos 9:2]
6Ndipo watu wa Gibeoni wakatuma wajumbe kwenda kwa Yoshua huko Gilgali kambini, wakamwambia, Usiulegeze mkono wako hata ukatuacha sisi watumishi wako; njoo kwetu upesi, utuokoe, na kutusaidia; kwa sababu wafalme wote wa Waamori wakaao katika nchi ya vilima wamekutana pamoja juu yetu.[#Yos 5:10]
7Basi Yoshua akakwea kutoka Gilgali, yeye, na watu wa vita wote pamoja naye, na mashujaa wote wenye uwezo.[#Yos 8:1]
8BWANA akamwambia Yoshua, Usiwaogope watu hao; kwa kuwa mimi nimekwisha kuwatia mikononi mwako; hapana mtu awaye yote miongoni mwao atakayesimama mbele yako.[#Kum 7:24; 11:25; Yos 11:6; 23:9; Amu 4:14; Yos 1:5]
9Basi Yoshua akawatokea ghafla; kwani alikwea kutoka Gilgali kwenda usiku kucha.
10BWANA naye akawatapanya mbele ya Israeli, naye Israeli akawaua uuaji ulio mkuu hapo Gibeoni, akawafukuza waikimbilie hiyo njia ya kukwelea kwenda Beth-horoni, na kuwapiga hadi kufikia Azeka, tena hadi kufikia Makeda.[#Amu 4:15; 1 Sam 7:10; Zab 18:14; Isa 28:21; 2 Nya 14:12; Yos 16:3,5; 15:35]
11Kisha ikawa, hapo walipokuwa wakikimbia mbele ya Israeli, hapo walipokuwa wakiteremka Beth-horoni, ndipo BWANA alipowatupia mawe makubwa kutoka mbinguni juu yao hadi kufikia Azeka, nao wakafa; hao waliokufa kwa kuuawa na hayo mawe ya barafu walikuwa ni wengi kuliko hao waliouawa na wana wa Israeli kwa upanga.[#Zab 18:13,14; 77:17; Isa 28:2; 30:30; Ufu 16:21]
12Ndipo Yoshua akanena na BWANA katika siku hiyo ambayo BWANA aliwatoa Waamori mbele ya wana wa Israeli; akasema mbele ya macho ya Israeli,[#Kum 4:19; 17:3; Zab 19:4; Isa 28:21; 38:8; Hab 3:11; Amu 12:12]
Wewe Jua, simama kimya juu ya Gibeoni;
Na wewe Mwezi, simama katika bonde la Aiyaloni.
13Ndipo jua likasimama, na mwezi ukatulia,[#2 Sam 1:18]
Hadi hilo taifa lilipokuwa limekwisha jilipiza kisasi juu ya adui zao.
Hayo, je! Hayakuandikwa ndani ya kitabu cha Yashari? Basi jua likasimama kimya katikati ya mbingu, wala halikufanya haraka kuchwa kama muda wa siku nzima.
14Haikuwapo siku nyingine mfano wa siku hiyo katika siku zilizotangulia mbele yake wala katika hizo zilizofuata baada yake, hata ikawa yeye BWANA kuisikia sauti ya binadamu; kwa kuwa BWANA alipiga vita kwa ajili ya Israeli.[#Isa 38:8; Kut 14:14; Kum 1:30; 3:22; 20:4; 33:26-29; Yos 23:3,10; Amu 1:19,22; 2 Nya 20:29; Neh 4:20; Zab 33:8-20; Isa 31:4; 42:13; Zek 14:3]
15Basi Yoshua akarudi, na Israeli wote wakarudi pamoja naye, mpaka kambini hapo Gilgali.
16Na hawa wafalme watano wakakimbia, wakajificha ndani ya pango la Makeda.
17Kisha Yoshua aliambiwa habari hiyo, ya kwamba, Hao wafalme watano wameonekana, nao wamejificha ndani ya pango ya Makeda
18Basi Yoshua akasema, Haya, vingirisheni mawe makubwa mdomoni mwa lile pango, kisha wekeni watu hapo ili kuwalinda;
19lakini msikae ninyi; wafuatieni adui zenu, mwapige hao walio nyuma; msiwaache wakaingia ndani ya miji yao; kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, amewatia mikononi mwenu.
20Kisha ikawa, hapo Yoshua, na wana wa Israeli, walipokuwa wamekwisha kuwaua watu wengi mno, hata wakaangamizwa, na hayo mabaki yao yaliyowasalia walipokuwa wamekwisha ingia katika miji yao yenye boma,
21ndipo hao watu wote wakamrudia Yoshua kambini huko Makeda salama; hakuna mtu awaye yote aliyetoa ulimi kinyume cha hao wana wa Israeli hata mmojawapo.[#Kut 11:7; Isa 54:17]
22Kisha Yoshua akasema, Haya, funua mdomo wa pango, mniletee hao wafalme watano hapa nje ya pango.
23Nao wakafanya hivyo, wakamletea hao wafalme watano hapo nje ya pango, yaani, mfalme wa Yerusalemu, na mfalme wa Hebroni, na mfalme wa Yarmuthi, na mfalme wa Lakishi, na mfalme wa Egloni.
24Kisha ikawa hapo walipomletea Yoshua hao wafalme watano hapo nje, Yoshua akawaita wanaume wote wa Israeli, akawaambia majemadari wa watu wa vita waliokwenda naye, Haya, jongeeni karibu, mweke nyayo za miguu yenu katika shingo za wafalme hawa. Nao wakajongea karibu, wakatia nyayo zao katika shingo zao.[#Kum 33:29; Zab 2:8-12; 91:13; Isa 26:5,6; Mal 4:3; Ufu 2:26,27]
25Yoshua akawaambia, Msiogope, wala msifadhaike; iweni hodari na wa mioyo ya ushujaa; kwa kuwa ndivyo BWANA atakavyowafanyia adui zenu wote ambao mnapigana nao.[#Kum 31:6,8; Yos 1:9; 1 Sam 17:37; Zab 63:9; 2 Kor 1:10; 2 Tim 4:17; Kum 3:21; 7:19]
26Baadaye Yoshua akawapiga, na kuwaua, akawatundika katika miti mitano; nao wakawa wametundikwa katika hiyo miti hadi jioni.[#Hes 25:14; Yos 8:29; 2 Sam 21:6,9; Est 2:23; 7:9,10; Zab 149:7,9]
27Kisha wakati wa kuchwa jua, Yoshua akatoa amri, nao wakawateremsha katika hiyo miti, na kuwatupa katika lile pango ambamo walikuwa walijificha kisha wakatia mawe makubwa mdomoni mwa pango, hata hivi leo.[#Kum 21:23; Yos 8:29]
28Siku hiyo Yoshua akautwaa mji wa Makeda, akaupiga kwa makali ya upanga, na mfalme wake; akawaangamiza kabisa na wote pia waliokuwamo ndani yake, hakumwacha hata mmoja aliyesalia; naye akamfanyia huyo mfalme wa Makeda kama alivyomfanyia huyo mfalme wa Yeriko.[#Yos 6:21]
29Kisha Yoshua akapita kutoka hapo Makeda, mpaka Libna, na Israeli wote pamoja naye, nao wakapiga Libna;[#Yos 15:42; 21:13; 2 Fal 8:22; 19:8]
30BWANA akautia na mji huo pia pamoja na mfalme wake mkononi mwa Israeli; naye akaupiga kwa makali ya upanga, na wote pia waliokuwamo ndani yake; hakumwacha hata mmoja aliyesalia ndani yake; naye akamtenda mfalme wake kama alivyomtenda huyo mfalme wa Yeriko.
31Kisha Yoshua akapita kutoka hapo Libna, na Israeli wote pamoja naye, wakafika Lakishi, wakapiga kambi mbele yake na kupigana nao;[#2 Fal 14:19; Mik 1:13]
32BWANA akautia huo mji wa Lakishi mkononi mwa Israeli, naye akautwaa siku ya pili, akaupiga kwa makali ya upanga, na wote pia waliokuwamo ndani yake, sawasawa na hayo yote aliyoutenda Libna.
33Wakati huo Horamu, mfalme wa Gezeri, akakwea ili kuusaidia Lakishi, lakini Yoshua akampiga yeye na watu wake, hata asimsazie hata mtu mmoja.[#Yos 16:3,10; Amu 1:29; 1 Fal 9:16,17; 1 Nya 20:4]
34Kisha Yoshua akapita kutoka hapo Lakishi, na Israeli wote pamoja naye, hadi wakafika Egloni; nao wakauzingira na kuushambulia;
35siku iyo hiyo wakautwaa, nao wakaupiga kwa makali ya upanga, na wote pia waliokuwamo ndani yake akawaangamiza kabisa siku hiyo, sawasawa na hayo yote aliyoufanyia mji wa Lakishi.
36Kisha Yoshua akakwea kutoka hapo Egloni, na Israeli wote pamoja naye, hadi wakafika Hebroni; nao wakapigana nao;[#Hes 13:22; Yos 14:13; 15:13; Amu 1:10; 2 Sam 5:1,4]
37wakautwaa, na kuupiga kwa makali ya upanga, na mfalme wake, na miji yake yote, na wote waliokuwamo ndani yake; hakumwacha aliyesalia hata mtu mmoja, sawasawa na hayo yote aliyoufanyia huo mji wa Egloni; lakini akauangamiza kabisa, na wote pia waliokuwamo ndani yake.
38Kisha Yoshua akarudi, na Israeli wote pamoja naye, hata Debiri; nao wakapigana nao;[#Yos 15:15; 21:15; Amu 1:11,15]
39kisha akautwaa, na mfalme wake, na miji yake yote; nao wakawapiga kwa makali ya upanga, wakawaangamiza kabisa wote pia waliokuwamo ndani yake; hakumwacha hata mmoja aliyesalia; kama alivyoufanyia Hebroni aliufanyia na Debiri vivyo hivyo, na mfalme wake; kama alivyoufanyia Libna, na mfalme wake.
40Basi Yoshua akaipiga nchi hiyo yote, nchi ya vilima, na nchi ya Negebu, na nchi ya Shefela, na nchi ya materemko, na wafalme wake wote; hakumwacha aliyesalia hata mmoja; lakini akawaharibu kabisa wote waliokuwa hai, kama BWANA, Mungu wa Israeli, alivyoamuru.[#Yos 15:21-63; 19:1-8; Kut 23:31-33; 34:12; Kum 7:2; 20:16,17]
41Yoshua akawapiga kutoka Kadesh-barnea mpaka Gaza, na nchi yote ya Gosheni, hata Gibeoni.[#Hes 13:17,26; 32:8; Mwa 10:19; Kum 2:23; Amu 16:1; Amo 1:6; Sef 2:4; Zek 9:5; Mdo 8:26; Yos 11:16]
42Na wafalme hao wote na nchi zao Yoshua akatwaa kwa wakati mmoja, kwa sababu yeye BWANA, Mungu wa Israeli, alipigana kwa ajili ya Israeli,[#Zab 44:2; 80:8; Isa 43:4]
43Kisha Yoshua akarudi, na Israeli wote pamoja naye, hata kambi yao huko Gilgali.