The chat will start when you send the first message.
1Ikawa, wafalme wa Waamori, waliokaa ng'ambo ya Yordani pande za magharibi, na wafalme wote wa Wakanaani, waliokuwa karibu na bahari, waliposikia jinsi BWANA alivyoyakausha maji ya Yordani mbele ya wana wa Israeli, hadi tulipokwisha kuvuka, basi mioyo yao iliyeyuka, wala haikuwamo roho ya nguvu ndani yao tena; kwa ajili ya wana wa Israeli.[#Hes 13:29; Kut 15:14; Zab 48:6; Eze 21:7; 1 Fal 10:5]
2Wakati huo BWANA akamwambia Yoshua, Haya, jifanyie visu vya mawe ya gumegume, watahiri tena wana wa Israeli mara ya pili.[#Kut 4:25]
3Basi Yoshua akajifanyia visu vya mawe ya gumegume, akawatahiri wana wa Israeli huko Gibea-haaralothi.[#5:3 Maana yake ni ‘mlima wa Magovi’.]
4Na sababu ya Yoshua kutahiri ni hii; watu wote wanaume waliotoka Misri, waliokuwa wapiganaji vita wote walifariki katika safari jangwani baada ya kutoka Misri.[#Hes 14:29; 26:64; Kum 2:16]
5Kwa kuwa watu wote waliotoka walikuwa wamekwisha kutahiriwa; lakini watu wote waliozaliwa katika safari jangwani walipokwisha kutoka Misri, hao hawakutahiriwa.
6Kwa kuwa wana wa Israeli walitembea muda wa miaka arubaini barani, hadi hilo taifa zima, yaani, watu wanaume wapiganaji vita, waliotoka Misri, walipokuwa wameangamia; kwa sababu hawakuisikiza sauti ya BWANA; nao ndio BWANA aliowaapia ya kwamba hatawaacha waione hiyo nchi, ambayo BWANA aliwaapia baba zao kwamba atatupa sisi; nchi itiririkayo maziwa na asali.[#Hes 14:28-35; Kum 1:3; Zab 95:10; Ebr 3:11]
7Na watoto wao, aliowainua badala yao ndio hao aliowatahiri Yoshua; kwa kuwa wao walikuwa hawajatahiriwa, kwa maana hawakuwatahiri njiani.[#Hes 14:31]
8Ilikuwa walipokwisha kutahiriwa taifa zima, wakakaa kila mtu mahali pake kambini, hadi walipopoa.[#Mwa 34:25]
9BWANA akamwambia Yoshua, Siku hii ya leo nimeivingirisha hiyo aibu ya Misri iondoke juu yenu. Kwa hiyo jina la mahali pale likaitwa Gilgali, hata hivi leo.[#1 Sam 14:6; Law 18:3; Yos 24:14; Eze 20:7; 23:3,8; #5:9 Kwa maana ya kuvingirisha.]
10Basi wana wa Israeli wakapanga hema zao huko Gilgali; nao wakala sikukuu ya Pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi, jioni, katika nchi tambarare za Yeriko.[#Kut 12:1-13; Hes 9:5]
11Nao wakala katika mazao ya nchi siku ya pili ya kuiandama hiyo sikukuu ya Pasaka, mikate isiyotiwa chachu, na bisi, siku iyo hiyo.
12Ndipo ile mana ikakoma siku ya pili yake, baada ya wao kuyala hayo mazao ya nchi; na hao wana wa Israeli hawakuwa na mana tena; lakini wakala mazao ya nchi ya Kanaani mwaka huo.[#Kut 16:35]
13Ikawa hapo Yoshua alipokuwa karibu na mji wa Yeriko, akainua macho yake na kuangalia juu, akaona ghafla mtu mmoja, mwanamume amesimama amemkabili naye alikuwa na upanga uliofutwa mkononi mwake; Yoshua akamwendea, na kumwambia, Je! Wewe u upande wetu, au upande wa adui zetu?[#Mwa 18:2; Kut 23:23; Zek 1:8; Mdo 1:10]
14Akasema, La, lakini mimi ni kamanda wa jeshi la BWANA, nimekuja sasa. Yoshua akainama chini hadi nchi, akasujudu, akamwuliza, Bwana wangu aniambia nini mimi mtumishi wake?[#Dan 10:13; 12:1; Ufu 12:7; Mwa 17:3; Law 9:24; Hes 16:22,45]
15Huyo kamanda wa jeshi la BWANA akamwambia Yoshua, Vua viatu vyako miguuni mwako; kwa kuwa mahali hapo usimamapo ni patakatifu. Yoshua akafanya hivyo.[#Kut 3:5; 19:10,13; Law 19:2; 1 Sam 2:2; 1 Nya 16:25,29; Zab 22:3; 29:2; Isa 6:3; Mdo 7:33; Ufu 4:8; 15:4]