The chat will start when you send the first message.
1Jinsi dhahabu ilivyoacha kung'aa,
Na dhahabu iliyo safi ilivyobadilika!
Mawe ya patakatifu yametupwa
Mwanzo wa kila njia.
2Wana wa Sayuni wenye thamani,[#2 Kor 4:7]
Walinganao na dhahabu safi,
Jinsi wanavyodhaniwa kuwa vyombo vya udongo,
Kazi ya mikono ya mfinyanzi!
3Hata mbwamwitu hutoa matiti,[#Ayu 39:14]
Huwanyonyesha watoto wao;
Binti ya watu wangu amekuwa mkali,
Mfano wa mbuni jangwani.
4Ulimi wa mtoto anyonyaye[#Zab 22:15]
Wagandamana na kinywa chake kwa kiu;
Watoto wachanga waomba chakula,
Wala hakuna hata mmoja awamegeaye.
5Wale waliokula vitu vya anasa[#Ayu 24:8; Lk 15:16]
Wameachwa peke yao njiani;
Wale waliokuzwa kuvaa nguo nyekundu
Wakumbatia jaa.
6Maana uovu wa binti ya watu wangu ni mkubwa[#Mwa 19:24]
Kuliko dhambi ya Sodoma,
Uliopinduliwa kama katika dakika moja,
Wala mikono haikuwekwa juu yake.
7Wakuu wake walikuwa safi kuliko theluji,
Walikuwa weupe kuliko maziwa;
Miili yao, walikuwa wekundu kuliko marijani,
Na umbo lao kama yakuti samawi.
8Nyuso zao ni nyeusi kuliko makaa;[#Zab 102:5]
Hawajulikani katika njia kuu;
Ngozi yao yagandamana na mifupa yao
Imekauka, imekuwa kama mti.
9Heri wale waliouawa kwa upanga
Kuliko wao waliouawa kwa njaa;
Maana hao husinyaa, wakichomwa
Kwa kukosa matunda ya mashamba.
10Mikono ya wanawake wenye huruma[#Omb 2:20; Kum 28:57; Eze 5:10]
Imewatokosa watoto wao wenyewe;
Walikuwa ndio chakula chao
Katika uharibifu wa binti ya watu wangu.
11BWANA ameitimiza ghadhabu yake,[#Kum 32:22]
Ameimimina hasira yake kali;
Naye amewasha moto katika Sayuni
Ulioiteketeza misingi yake.
12Wafalme wa dunia hawakusadiki,[#Kum 29:24]
Wala wote wakaao duniani,
Ya kwamba mtesi na adui wangeingia
Katika malango ya Yerusalemu.
13Ni kwa sababu ya dhambi za manabii wake[#Yer 5:31; Mt 23:31]
Na maovu ya makuhani wake,
Walioimwaga damu ya wenye haki
Katikati yake.
14Hutangatanga njiani kama vipofu,[#Yer 2:34]
Wametiwa unajisi kwa damu;
Hata ikawa hakuna aliyeweza
Kuyagusa mavazi yao.
15Watu waliwapigia kelele, Ondokeni, Uchafu,
Ondokeni, ondokeni, msiguse;
Walipokimbia na kutangatanga, watu walisema kati ya mataifa,
Hawatakaa hapa tena.
16Hasira ya BWANA imewatenga,[#Omb 5:12]
Yeye hatawaangalia tena;
Hawakujali nafsi za wale makuhani,
Hawakuwaheshimu wazee wao.
17Macho yetu yamechoka[#2 Fal 24:7; Isa 20:5,6]
Kwa kuutazamia bure msaada wetu;
Katika kungoja kwetu tumengojea taifa
Lisiloweza kutuokoa.
18Wanatuvizia hatua zetu,[#2 Fal 25:4; Yer 51:33]
Hata hatuwezi kwenda katika njia zetu;
Mwisho wetu umekaribia, siku zetu zimetimia;
Maana mwisho wetu umefika.
19Waliotufuatia ni wepesi
Kuliko tai za mbinguni;
Hao walitufuatia milimani,
Nao walituotea jangwani.
20Pumzi ya mianzi ya pua zetu, masihi wa BWANA,[#Mwa 2:7; Yer 52:9; #4:20 Au, mtiwa mafuta (tazama 1 Sam 2:10).]
Alikamatwa katika marima yao;
Ambaye kwa habari zake tulisema,
Chini ya kivuli chake tutakaa kati ya mataifa.
21Furahi, ushangilie, Ee binti Edomu,
Ukaaye katika nchi ya Usi;
Hata kwako kikombe kitapita,
Utalewa, na kujifanya uchi.
22Adhabu ya uovu wako imetimia, Ee binti Sayuni;
Hatakuhamisha tena;
Atapatiliza uovu wako, Ee binti Edomu;
Atazivumbua dhambi zako.