The chat will start when you send the first message.
1Ee BWANA, kumbuka yaliyotupata;
Utazame na kuiona aibu yetu.
2Urithi wetu umegeuka kuwa mali ya wageni;
Na nyumba zetu kuwa mali ya mataifa.
3Tumekuwa yatima waliofiwa na baba;
Mama zetu wamekuwa kama wajane.
4Tumekunywa maji yetu kwa fedha;
Kuni zetu twauziwa.
5Watufuatiao wako juu ya shingo zetu;
Tumechoka, tusipate pumziko lolote.
6Tumewapa hao Wamisri mkono;[#Mwa 24:2; Yer 50:15; Hos 12:1]
Na Waashuri nao, ili tushibe chakula.
7Baba zetu walitenda dhambi hata hawako;[#Yer 16:12; Eze 18:2; Mt 23:32]
Na sisi tumeyachukua maovu yao.
8Watumwa wanatutawala;
Hakuna mtu wa kutuokoa na mikono yao.
9Twapata chakula kwa kujihatarisha nafsi zetu;
Kwa sababu ya upanga wa nyikani.
10Ngozi yetu ni nyeusi kama tanuri;
Kwa sababu ya joto ya njaa ituteketezayo.
11Wanawake katika Sayuni wanashikwa kwa nguvu;[#Isa 13:16]
Na mabikira katika miji ya Yuda.
12Wakuu hutundikwa kwa mikono yao;
Nyuso za wazee hazipewi heshima.
13Vijana huyachukua mawe ya kusagia;[#Amu 16:21]
Na watoto hujikwaa chini ya kuni.
14Wazee wameacha kwenda langoni;[#2 Fal 25:18]
Na vijana kwenda ngomani.
15Furaha ya mioyo yetu imekoma;
Machezo yetu yamegeuka maombolezo.
16Taji ya kichwa chetu imeanguka;
Ole wetu! Kwa kuwa tumetenda dhambi.
17Kwa sababu hiyo mioyo yetu imezimia;[#Ayu 17:7; Zab 6:7]
Kwa ajili ya hayo macho yetu hayaoni vema.
18Kwa ajili ya mlima Sayuni ulio ukiwa,
Mbweha hutembea juu yake.
19Wewe, BWANA, unadumu milele;
Kiti chako cha enzi ni tangu kizazi hata kizazi.
20Mbona watusahau sikuzote;
Na kutuacha muda huu mwingi?
21Ee BWANA, utugeuze kwako, nasi tutageuka; Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale.
22Ingawa wewe umetukataa kabisa;
Nawe una hasira nyingi sana juu yetu.