Mambo ya Walawi 11

Mambo ya Walawi 11

Vyakula halali na haramu

1BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,

2Neneni na wana wa Israeli, mkiwaambia, Wanyama hawa ndio wanyama wenye uhai mtakaowala, katika hayawani wote walio juu ya nchi.[#Kum 14:4; Eze 4:4; Dan 1:8; Mt 15:11; Mdo 10:12; Rum 14:2; 1 Kor 8:8; Kol 2:16; Ebr 9:10]

3Kila mnyama mwenye kwato katika miguu yake, mwenye miguu iliyopasuka kati, mwenye kucheua, katika hayawani, hao ndio mtakaowala.

4Pamoja na hayo, wanyama hawa hamtawala katika wale wenye kucheua, na katika wale walio na kwato; ngamia, kwa sababu yuacheua lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu.

5Na wibari, kwa sababu yeye hucheua lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu.

6Na sungura, kwa sababu hucheua, lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu.[#1 Tim 4:4,5]

7Na nguruwe, kwa sababu yeye anazo kwato, ni mwenye miguu iliyopasuka kati, lakini hacheui, yeye ni najisi kwenu.[#Isa 65:4; 66:3,17]

8Msiile nyama yao, wala msiiguse mizoga yao; hao ni najisi kwenu.[#Isa 52:11; Mt 15:11,20; Mk 7:2,15,18; Mdo 10:14,15; 15:29; Rum 14:14,17; 1 Kor 8:8; Kol 2:16,21; Ebr 9:10]

9Katika hao wote walio ndani ya maji mtakula hawa; kila aliye na mapezi na magamba, ndani ya hayo maji, na ndani ya bahari, na ndani ya mito, mtakula hao.[#Kum 14:9,10]

10Na hao wote wasio na mapezi na magamba, ndani ya bahari, na ndani ya mito, katika hao waendao majini, na katika wote wenye uhai, waliomo majini, hao ni machukizo kwenu,[#Law 7:18; Kum 14:3]

11watakuwa machukizo kwenu; msiile nyama yao, na mizoga yao itakuwa machukizo kwenu.

12Kila asiye na mapezi wala magamba aliye ndani ya maji ni machukizo kwenu.

13Kisha katika ndege hawa watakuwa ni machukizo kwenu; hawataliwa, ndio machukizo; tai, na furukombe, na kipungu;[#Kum 14:12; Rum 14:1-23]

14na mwewe, na kozi kwa aina zake,

15na kila kunguru kwa aina zake;

16na mbuni, na kirukanjia, na dudumizi, na kipanga kwa aina zake;

17na bundi, na mnandi, na bundi mkubwa;

18na mumbi, na mwari, na mderi;[#Zab 102:6; Sef 2:14]

19na korongo, na koikoi kwa aina zake, na hudihudi, na popo.

20Tena vyote vitambaavyo vyenye mabawa viendavyo kwa miguu minne, hivi ni machukizo kwenu.

21Pamoja na hayo, hivi vitambaavyo vyenye mabawa viendavyo kwa miguu minne ni halali kula, hao walio na miguu mirefu, ya kurukia juu ya nchi;

22katika hao mna ruhusa kuwala; nzige kwa aina zake, na nzige kuu kwa aina zake, na panzi kwa aina zake, na parare kwa aina zake.[#Mt 3:4; Mk 1:6; Amu 6:5; Yer 46:23; Nah 3:17]

23Lakini vyote vitambaavyo vyenye mabawa, vilivyo na miguu minne, ni machukizo kwenu.

Wanyama walio haramu

24Nanyi mtakuwa najisi kwa wanyama hao; kila atakayegusa mzoga wao atakuwa ni najisi hata jioni;

25na mtu awaye yote atakayechukua chochote cha mizoga yao atafua nguo zake, naye atakuwa najisi hata jioni.[#Law 14:8; 15:5; Hes 19:10,22; 31:24]

26Kila mnyama aliyepasuliwa ukwato, naye hana kwato mbili, wala hacheui, huyo ni najisi kwenu; kila agusaye wanyama hao atakuwa ni najisi.

27Tena kila mnyama aendaye kwa vitanga vyake, katika hao wanyama wote waendao kwa miguu minne, hao ni najisi kwenu; awaye yote atakayegusa mizoga yao, atakuwa ni najisi hata jioni.

28Na huyo atakayechukua mzoga wa wanyama hao atafua nguo zake, naye atakuwa ni najisi hata jioni; hao ni najisi kwenu.

29Miongoni mwa viumbe watambaao juu ya nchi, hawa ni najisi kwenu; kicheche, panya na mjombakaka kwa aina zake,[#Ebr 9:10; Isa 66:17]

30na guruguru kenge, mjusi, goromoe na lumbwi.[#Zab 58:8; Isa 2:20]

31Wanyama hao ndio walio najisi kwenu katika hao watambaao; yeyote atakayewagusa, wakiisha kuwa mgoza, atakuwa ni najisi hata jioni.

32Tena kitu chochote, wanyama hao mmojawapo atakachokiangukia, wakiisha kufa, kitakuwa ni najisi; cha mti, nguo, ngozi, gunia, chombo chochote cha kufanyia kazi yoyote, lazima kitiwe ndani ya maji, nacho kitakuwa ni najisi hadi jioni; ndipo kitakapokuwa ni safi.[#Law 15:12]

33Na kila chombo cha udongo, wanyama hao mmojawapo atakachokiangukia, kila kilichomo ndani yake kitakuwa ni najisi, na hicho chombo kitavunjwa.[#Law 6:28]

34Chakula chochote cha kuliwa kitakuwa najisi kikitiwa maji ya chombo hicho; na kila kinyweo ambacho ni cha kunywewa, kilichomo katika chombo kama hicho, kitakuwa ni najisi.

35Na kila kitu kitakachoangukiwa na kipande chochote cha mizoga yao kitakuwa najisi; iwe ni tanuri, au meko ya vyungu, kitavunjwa vipande vipande; ni najisi vitu hivyo, navyo vitakuwa najisi kwenu.

36Pamoja na hayo, chemchemi, au shimo, ambamo maji yakusanyika, vitakuwa ni safi; lakini hicho kitakachogusa mizoga yao kitakuwa ni najisi.

37Na kipande chochote cha mzoga kikiwa kimeangukia mbegu za kupandwa, zitakazopandwa zitakuwa safi.

38Lakini ikiwa hizo mbegu zilitiwa maji na chochote cha mizoga yao kuziangukia, ni najisi kwenu.

39Mnyama yeyote ambaye mna ruhusa kumla akifa, yeye anayeugusa mzoga wake atakuwa najisi hadi jioni.

40Na yeye atakayekula nyama ya mzoga wake atafua nguo zake, naye atakuwa najisi hata jioni; yeye atakayeuchukua mzoga wake atafua nguo zake, naye atakuwa ni najisi hadi jioni.[#Law 17:5; 22:8; Kum 14:21; Eze 4:14; 44:31]

41Na kila kiumbe kitambaacho juu ya nchi ni machukizo; hakitaliwa.

42Kila aendaye kwa tumbo lake, na kila aendaye kwa miguu minne, na kila aendaye kwa miguu mingi, maana, ni vyote vyenye kutambaa vitambaavyo juu ya nchi, hamtavila, kwa kuwa ni machukizo.

43Msifanye nafsi zenu kuwa ni chukizo kwa kitu chochote chenye kutambaa, kitambaacho, wala msifanye nafsi zenu kuwa ni najisi kwa vitu hivyo, mkajipatia uchafu kwa hivyo.[#Law 20:25]

44Kwa kuwa mimi ni BWANA, Mungu wenu; takaseni nafsi zenu basi; iweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni Mtakatifu; wala msitie uchafu nafsi zenu kwa kitu kitambaacho cha aina yoyote, kiendacho juu ya nchi.[#Law 19:2; 1 Pet 1:15,16; Isa 51:15; 43:3; Kut 19:6; 1 The 4:7]

45Kwa kuwa mimi ni BWANA niliyewaleta kutoka nchi ya Misri, ili kwamba niwe Mungu wenu; basi mtakuwa watakatifu, kwa kuwa mimi ni Mtakatifu.[#Mwa 35:1,2; Kut 6:7; 20:2; Rum 14:17; 12:1; 1 Kor 6:11]

46Hii ndiyo sheria katika hao wanyama, na ndege, na kila kiumbe kilicho hai, kiendacho ndani ya maji, na kila kiumbe kitambaacho juu ya nchi;

47ili kupambanua kati ya hao walio najisi na hao walio safi, na kati ya kiumbe kilicho hai ambacho chaliwa, na hicho kilicho hai ambacho hakiliwi.[#Law 10:10; Yer 15:19; Eze 22:26; 44:23]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya