Mambo ya Walawi 17

Mambo ya Walawi 17

Uchinjaji wa wanyama

1BWANA akamwambia Musa

2Sema na Haruni, na wanawe, na wana wote wa Israeli, uwaambie; Neno hili ndilo aliloamuru BWANA,

3Mtu yeyote wa nyumba ya Israeli atakayechinja ng'ombe, mwana-kondoo, au mbuzi, ndani au nje ya kambi,

4wala hamleti mlangoni pa hema ya kukutania, kama matoleo kwa BWANA mbele ya hema ya BWANA; mtu huyo atahesabiwa kuwa ana hatia ya damu; amemwaga damu; na atatupiliwa mbali na watu wake;[#Kum 12:5; Zab 32:2; Rum 4:6; 5:13; Mwa 17:14]

5ili wana wa Israeli walete sadaka zao, wazichinjazo mashambani, wazilete kwa BWANA, mpaka mlango wa hema ya kukutania, kwa huyo kuhani, ili wazichinje ziwe sadaka za amani kwa BWANA.[#Mwa 21:33; 22:2; Kum 12:2; 1 Fal 14:22,23; 2 Fal 17:10; Eze 20:28; 22:9]

6Naye kuhani atainyunyiza damu yake juu ya madhabahu ya BWANA, mlangoni pa hema ya kukutania, na kuyateketeza mafuta yake, yawe harufu njema mbele za BWANA.[#Kut 29:18; Law 4:31; Hes 18:17]

7Wala hawatatoa tena sadaka zao kwa wale majini, ambao huwafuata ili wafanye uasherati nao. Sheria hii itakuwa sheria ya milele kwao, kizazi baada ya kizazi.[#Kum 32:17; 2 Nya 11:15; Zab 106:37; Mdo 7:42,43; 1 Kor 10:20; Kut 34:15; Kum 31:16]

8Nawe utawaambia, Mtu yeyote katika nyumba ya Israeli, au miongoni mwa wageni, wanaokaa nao, atoaye sadaka ya kuteketezwa au dhabihu,

9wala haileti mlangoni pa hema ya kukutania, ili aisongeze kwa BWANA basi mtu huyo atatengwa na watu wake.

Katazo la kula damu

10Kisha mtu yeyote wa nyumba ya Israeli, au miongoni mwa hao wageni wakaao kati yao, atakayekula damu, ya aina yoyote, nitamkataa mtu huyo alaye damu, na nitamtenga na watu wake.[#Mwa 9:4; Law 7:26-27; 19:26; Kum 12:16,23; 15:23; 1 Sam 14:33; Law 26:17; Yer 44:11; Eze 15:7]

11Kwa kuwa uhai wa mwili uko katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi.[#Ebr 9:22; Mk 14:24; Rum 5:9; Efe 1:7; Kol 1:14; 1 Pet 1:2; 1 Yoh 1:7]

12Kwa hiyo niliwaambia wana wa Israeli, Hapana mtu miongoni mwenu aliye na ruhusa kula damu, wala mgeni aishiye kati yenu asile damu.

13Mtu yeyote aliye wa wana wa Israeli, au wa hao wageni wakaao kati yenu, ambaye amemshika mnyama, au ndege ambaye huliwa, katika kuwinda kwake; atamwaga damu yake, na kuifunikia mchangani.[#Kum 12:16; 15:23; 1 Sam 14:32-34; Eze 24:7]

14Kwa kuwa uhai wa kila kiumbe uko katika damu yake; ndio nikawaagiza wana wa Israeli, Msiile damu ya mnyama wa aina yoyote; kwa kuwa uhai wa kila kiumbe ni damu yake; yeyote atakayeila atatengwa.[#Mwa 9:4]

15Tena kila mtu atakayekula nyamafu, au nyama ya mnyama aliyeraruliwa na wanyama, awe ni mzalia au mgeni, atafua nguo zake, na kuoga majini naye atakuwa najisi hadi jioni; ndipo atakapokuwa safi.[#Kut 22:31; Kum 14:21; Eze 4:14]

16Lakini iwapo hazifui, wala haogi mwili, ndipo atakapolipizwa uovu wake.[#Hes 19:20; Ebr 9:28]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya