The chat will start when you send the first message.
1Kisha BWANA akamwambia Musa, Nena na hao makuhani, wana wa Haruni, uwaambie, Mtu asijinajisi kwa ajili ya wafu katika watu wake;[#Law 5:2; Eze 44:25]
2isipokuwa ni kwa ajili ya jamaa yake wa karibu, kwa ajili ya mama yake, na kwa ajili baba yake, na kwa ajili ya mwanawe, na kwa ajili ya binti yake, na kwa ajili ya nduguye mwanamume;
3na kwa ajili ya dada yake aliye mwanamwali, aliye wa udugu kwake, ambaye hajaolewa na mwanamume; ana ruhusa kujitia unajisi kwa ajili yake huyo.
4Asijitie unajisi, ijapokuwa ni mkubwa katika watu wake, hata akajinajisi.
5Wasijifanyie upara kichwani, wala wasinyoe pembe za ndevu zao, wala wasichanje tojo katika miili yao.[#Law 19:27-28; Kum 14:1; Eze 44:20]
6Watakuwa watakatifu kwa Mungu wao, wala wasilinajisi jina la Mungu wao; kwa kuwa wao ndio wasongezao sadaka za BWANA kwa njia ya moto, chakula cha Mungu wao; kwa ajili ya hayo watakuwa watakatifu.[#Kut 20:7; Law 18:21; 19:12; Kum 5:11; Zab 15:4; Mt 5:33-37; Yak 5:12; Law 3:11]
7Wasimwoe mwanamke aliye kahaba, au huyo aliye mwenye unajisi; wala wasimwoe mwanamke aliyeachwa na mumewe; kwa kuwa yeye kuhani ni mtakatifu kwa Mungu wake.[#Eze 44:22; Kum 24:1,2]
8Kwa hiyo basi utamtakasa; kwa kuwa yeye husongeza chakula cha Mungu wako; atakuwa mtakatifu kwako wewe; kwa kuwa mimi BWANA niwatakasaye ninyi ni mtakatifu.[#Law 20:7,8; Isa 43:15]
9Na binti ya kuhani yeyote atakapojitia unajisi kwa ukahaba, amemtia unajisi baba yake; atachomwa hadi afe.[#Mwa 38:24]
10Na yeye aliye kuhani mkuu katika nduguze, ambaye mafuta ya kutiwa yamemiminwa kichwani mwake, naye akawekwa wakfu ili ayavae hayo mavazi, yeye hataziacha wazi nywele za kichwa chake, wala hatazirarua nguo zake;[#Kut 29:29; Hes 35:25; Kut 28:2; Law 10:6]
11wala hataingia penye maiti, wala asijitie unajisi kwa ajili ya baba yake wala mama yake;[#Hes 19:14]
12wala asitoke katika mahali patakatifu, wala asipatie unajisi mahali patakatifu pa Mungu wake; kwa kuwa utakaso wa hayo mafuta ya kutiwa ya Mungu wake uko juu yake; mimi ndimi BWANA.[#Law 10:7; Kut 28:36; Law 8:9,12,30]
13Naye atamwoa mwanamke katika ubikira wake.[#Eze 44:22]
14Asitwae mjane, wala mwanamke aliyeachwa na mumewe, wala mwanamke mwenye unajisi, wala kahaba; lakini atamwoa mwanamwali katika watu wake mwenyewe.
15Naye asiwatie unajisi wazawa wake katika watu wake; kwa kuwa mimi ndimi BWANA nimtakasaye.[#Rum 12:1; 1 Kor 3:16,17; Efe 5:17; 1 The 4:1-8]
16Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
17Nena na Haruni, umwambie, Mtu yeyote wa vizazi vyenu vyote aliye na kilema asikaribie kutoa chakula cha Mungu wake.[#Hes 16:5; Zab 64:4]
18Kwa kuwa mtu aliye na kasoro ya kimwili hatakaribia, asiyeoana, aliyelemaa mguu au mtu aliyejeruhika uso, au kiungo kilichozidi vimpasavyo mwili,[#Law 22:23]
19au mtu aliyevunjika mguu, au aliyevunjika mkono,
20au aliye na kibyongo, au aliyedumaa, au aliye na kilema cha jichoni, au aliye na upele, au mwenye buba, au aliyevunjika mapumbu;[#Kum 23:1]
21mtu yeyote wa wazawa wa Haruni kuhani aliye na kilema asikaribie kuzisongeza sadaka za BWANA kwa njia ya moto; ana kilema huyo asikaribie kusongeza chakula cha Mungu wake.
22Atakula chakula cha Mungu wake, katika hicho kilicho kitakatifu sana, na hicho kilicho kitakatifu.[#Law 2:3,10; 22:10; Hes 18:19]
23Lakini hataingia ndani ya pazia, wala asikaribie madhabahu, kwa sababu ana kilema; ili kwamba asipanajisi patakatifu pangu; kwa kuwa mimi ndimi BWANA niwatakasaye.
24Basi Musa akanena na Haruni na wanawe, na wana wa Israeli wote.