The chat will start when you send the first message.
1Na mtu yeyote akifanya dhambi, kwa kuwa ameisikia sauti yenye kuapisha, naye akawa ni shahidi, kwamba aliona au kujua, asipolifunua neno lile, ndipo atakapochukua uovu wake mwenyewe;[#1 Fal 8:31; Mit 29:24; Mt 26:63; Mwa 17:14; Law 7:18; 17:16; Hes 9:13]
2au kama mtu akigusa kitu kilicho najisi, iwe ni mzoga wa mnyama nyikani aliye najisi, au ni mzoga wa mnyama wa mfugo aliye najisi, au ni mzoga wa mdudu aliye najisi, bila kujua, akapata kuwa najisi, ndipo atakapochukua uovu wake;[#Law 11:24-39; Hes 19:11-16]
3au kama akiugusa uchafu wa binadamu, uchafu wowote ambao kwao amepata unajisi, bila kujua, hapo apatapo kulijua, ndipo atakapokuwa na hatia;[#Law 12:1; 13:1; 15:1]
4au, kama mtu akijiapisha, kwa kutamka haraka kwa midomo yake, kutenda uovu, au kutenda mema, neno lolote mtu atakalolitamka kwa kiapo pasipo kufikiri, bila kujua; hapo atakapolijua, ndipo atakapokuwa na hatia katika mambo hayo mojawapo;[#1 Sam 14:24; 25:22; Mal 3:5; Mdo 23:12; Mk 6:23]
5kisha itakuwa, hapo atakapokuwa na hatia katika mambo hayo mojawapo, ndipo atakapoliungama jambo hilo alilolikosa;[#Law 26:40; Hes 5:7; Ezr 10:11]
6naye atamletea BWANA sadaka yake ya hatia kwa ajili ya hiyo dhambi yake aliyoifanya, mwana-kondoo wa kike, au mbuzi mke, kutoka katika kundi lake, kuwa ni sadaka ya dhambi; kisha kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya hiyo dhambi yake.
7Lakini asipomweza mwana-kondoo, ndipo atakapomletea BWANA hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, kuwa ni sadaka yake ya hatia ya jambo hilo alilolikosa; mmoja wa hao ndege kwa sadaka ya dhambi, na wa pili kwa sadaka ya kuteketezwa.[#Law 14:21]
8Naye atawaleta kwa kuhani, atakayemsongeza kwanza yule wa sadaka ya dhambi, naye atamvunja shingo kichwa shingoni mwake, lakini asimpasue vipande viwili;
9kisha baadhi ya damu ya hiyo sadaka ya dhambi atainyunyiza katika ubavu wa madhabahu; na damu iliyosalia itachuruzishwa hapo chini ya madhabahu; ni sadaka ya dhambi.
10Kisha huyo ndege wa pili atamsongeza kuwa sadaka ya kuteketezwa, sawasawa na sheria; na kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya hiyo dhambi yake aliyoifanya, naye atasamehewa.[#Law 1:14]
11Lakini asipowaweza hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, ndipo hapo atakapoleta matoleo yake kwa ajili ya neno hilo alilolikosa, sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba, kuwa sadaka yake ya dhambi; asitie mafuta juu yake, wala ubani usitiwe juu yake; maana, ni sadaka ya dhambi.[#Hes 5:15]
12Naye atamletea kuhani, na kuhani atatwaa konzi yake ya huo unga kuwa ukumbusho wake, na kuuteketeza juu ya madhabahu, juu ya sadaka zilizosongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto; ni sadaka ya dhambi.[#Law 4:35]
13Na huyo kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya dhambi yake ambayo katika mambo hayo mojawapo amefanya dhambi, naye atasamehewa; na unga uliosalia utakuwa wa kuhani, kama hiyo sadaka ya unga ilivyokuwa.
14Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
15Mtu awaye yote akiasi na kufanya dhambi naye hakukusudia, katika mambo matakatifu ya BWANA; ndipo atakapomletea BWANA sadaka yake ya hatia, kondoo dume mkamilifu katika kundi lake; sawasawa na hesabu utakayomwandikia katika shekeli za fedha, kwa shekeli ya mahali patakatifu, kuwa sadaka ya hatia;[#Law 22:14; Ezr 10:19; Kut 30:13; Law 27:25]
16naye atalipa kwa ajili ya hilo alilolikosa katika kitu kile kitakatifu, kisha ataongeza na sehemu ya tano, na kumpa kuhani; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa huyo kondoo dume wa sadaka ya hatia, naye atasamehewa.[#Law 6:5; 22:14; Hes 5:7; Law 4:26; Ebr 9:13,14]
17Na kama mtu akifanya dhambi, na kutenda mambo hayo mojawapo ambayo BWANA alizuilia yasifanywe, ajapokuwa hakuyajua, ni mwenye hatia pia, naye atachukua uovu wake.[#Zab 19:12; Lk 12:48; Ebr 5:2]
18Naye ataleta kondoo dume wa kundi lake, mkamilifu, sawasawa na hesabu utakayomwandikia, kuwa sadaka ya hatia, amsongeze kwa huyo kuhani; na kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya jambo hilo alilolikosa pasipo kukusudia, asilijue, naye atasamehewa.
19Ni sadaka ya hatia; hakika yake ni mwenye hatia mbele za BWANA.[#Isa 53:10; Ezr 10:2]