The chat will start when you send the first message.
1Tena, aliwaambia wanafunzi wake, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyekuwa na wakili wake; huyu alishitakiwa kwake kuwa anatapanya mali zake.
2Akamwita, akamwambia, Ni habari gani hii ninayosikia juu yako? Toa hesabu ya uwakili wako, kwa kuwa huwezi kuwa wakili tena.
3Yule wakili akasema moyoni mwake, Nifanyeje? Maana, bwana wangu ananiondolea uwakili. Kulima, siwezi; kuomba, naona haya.
4Najua nitakalotenda, ili nitakapotolewa katika uwakili, wanikaribishe nyumbani mwao.
5Akawaita wadeni wa bwana wake, kila mmoja; akamwambia wa kwanza, Unadaiwa nini na bwana wangu?
6Akasema, Vipimo mia vya mafuta. Akamwambia, Twaa hati yako, keti upesi, andika hamsini.
7Kisha akamwambia mwingine, Na wewe unadaiwa nini? Akasema, Makanda mia ya ngano. Akamwambia, Twaa hati yako, andika themanini.
8Yule bwana akamsifu wakili asiyemwaminifu kwa vile alivyotenda kwa busara; kwa kuwa wana wa ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru.[#Efe 5:8; 1 The 5:5]
9Nami nawaambia, Jifanyieni rafiki kwa mali ya duniani, ili itakapokosekana wawakaribishe katika makao ya milele.[#Lk 14:14; Mt 6:20; 10:40; 19:21]
10Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na asiyeaminika katika lililo dogo, huwa haaminiki pia katika lililo kubwa.[#Lk 19:17]
11Basi, kama ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya duniani, ni nani atakayewapa amana mali ya kweli?
12Na kama hamkuwa waaminifu katika mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe?
13Hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana, ama atamchukia huyu na kumpenda huyu, ama atashikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali.[#Mt 6:24]
14Basi Mafarisayo, ambao wenyewe ni wapenda fedha, waliyasikia hayo yote, wakamdhihaki.[#Mt 23:14]
15Akawaambia, Ninyi ndinyi mnaojidai haki mbele ya wanadamu, lakini Mungu awajua mioyo yenu; kwa kuwa lililotukuka kwa wanadamu huwa chukizo mbele za Mungu.[#Lk 18:9-14; Mt 23:28; Zab 7:9; Mit 6:16,17]
16Torati na Manabii vilikuwapo mpaka Yohana; tangu wakati huo Habari Njema ya ufalme wa Mungu hutangazwa, na kila mtu hujiingiza kwa nguvu.[#Mt 11:12-13]
17Lakini ni rahisi zaidi mbingu na nchi vitoweke, kuliko itanguke nukta moja ya torati.[#Mt 5:18]
18Kila amwachaye mkewe na kumwoa mke mwingine azini; naye amwoaye yeye aliyeachwa na mumewe azini.[#Mt 5:32; 19:9; 1 Kor 7:10-11]
19Akasema, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula sikuzote kwa anasa.
20Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi,
21naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri; hata mbwa walikuwa wakija na kumramba vidonda vyake.[#Mt 15:27]
22Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Abrahamu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa.
23Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Abrahamu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake.
24Akalia, akasema, Ee baba Abrahamu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, aupoze ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu.
25Abrahamu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo yako mema katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unateseka.
26Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu.
27Akasema, Basi, baba, nakuomba, umtume nyumbani kwa baba yangu,
28kwa kuwa ninao ndugu watano, ili awashuhudie, wasije wao pia wakafika mahali hapa pa mateso.
29Abrahamu akasema, Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao.[#2 Tim 3:16]
30Akasema, La, baba Abrahamu, lakini kama akiwaendea mtu atokaye kwa wafu, watatubu.
31Akamwambia, Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishika hata mtu akifufuka katika wafu.[#Yn 11:45-53]