The chat will start when you send the first message.
1Akawaambia wanafunzi wake, Vikwazo havina budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye vinakuja kwa sababu yake!
2Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusagia lifungwe shingoni mwake, akatupwe baharini, kuliko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa.[#Mt 18:6,7]
3Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe.[#Mt 18:15]
4Na kama akikukosea mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe.[#Mt 18:21,22]
5Mitume wakamwambia Bwana, Tuongezee imani.[#Mk 9:24]
6Bwana akasema, Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng'oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii.[#Mt 17:20; 21:21]
7Lakini, ni nani kwenu mwenye mtumwa alimaye au achungaye ng'ombe, atakayemwambia mara arudipo kutoka shambani, Njoo upesi, keti, ule chakula?
8Je! Hatamwambia, Nitayarishie chakula, nile; jifunge unitumikie, hata niishe kula na kunywa, ndipo nawe utakapokula na kunywa?
9Je! Atampa asante yule mtumwa, kwa sababu ameyafanya aliyoagizwa?
10Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya.
11Ikawa walipokuwa njiani kwenda Yerusalemu, alikuwa akipita katikati ya Samaria na Galilaya.[#Lk 9:51; 13:22]
12Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali,[#Law 13:45,46]
13wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu!
14Alipowaona aliwaambia, Nendeni, mkajioneshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika.[#Law 13:49; 14:1-32; Lk 5:14]
15Na mmoja wao alipoona kwamba amepona, alirudi, huku akimtukuza Mungu kwa sauti kuu;
16akaanguka kifudifudi miguuni pake, akamshukuru; naye alikuwa Msamaria.
17Yesu akajibu, akanena, Hawakutakaswa wote kumi? Wale tisa wako wapi?
18Je! Hawakuonekana waliorudi kumpa Mungu utukufu ila mgeni huyu?
19Akamwambia, Inuka, nenda zako, imani yako imekuokoa.[#Lk 7:50]
20Na alipoulizwa na Mafarisayo, Ufalme wa Mungu utakuja lini? Aliwajibu akawaambia, ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza;[#Yn 18:36; 3:3]
21wala hawatasema, Tazama, upo huku, au, kule, kwa maana, tazama, ufalme wa Mungu umo ndani yenu.[#Mt 24:23; Yn 1:26; 12:35]
22Akawaambia wanafunzi, Siku zitakuja mtakapotamani kuona siku moja katika siku zake Mwana wa Adamu, msiione.
23Tena watawaambia, Tazama, kule! Tazama, huku! Msiondoke mahali mlipo, wala msiwafuate;[#Lk 21:8]
24kwa kuwa, kama vile umeme umulikavyo toka upande huu chini ya mbingu hata upande huu chini ya mbingu, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu katika siku yake.[#Mt 24:26,27]
25Lakini kwanza, hana budi kupata mateso mengi, na kukataliwa na kizazi hiki.[#Lk 9:22]
26Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu.[#Mwa 6:5-8; Mt 24:37-39]
27Walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakioa na kuolewa, hata siku ile Nuhu aliyoingia katika safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote.[#Mwa 7:6-24]
28Na kadhalika, kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakinunua na kuuza, wakipanda na kujenga;[#Mwa 18:20—19:25]
29lakini siku ile Lutu aliyotoka Sodoma kulinyesha moto na kibiriti kutoka mbinguni vikawaangamiza wote.[#Mwa 19:24,25]
30Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile atakayofunuliwa Mwana wa Adamu.
31Katika siku ile, aliye juu ya dari, na mali yake imo ndani ya nyumba, asishuke ili kuitwaa; na kadhalika, aliye shambani asirejee nyuma.[#Mt 24:17-18; Mk 13:15-16; Mwa 19:26]
32Mkumbukeni mkewe Lutu.[#Mwa 19:26]
33Mtu yeyote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na yeyote atakayeiangamiza ataiponya.[#Mt 10:39; 16:25; Mk 8:35; Lk 9:24; Yn 12:25]
34Nawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa katika kitanda kimoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa.
35Wanawake wawili watakuwa wakisaga pamoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa. [[#Mt 24:40,41]
36Watu wawili watakuwa shambani, mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa.]
37Wakajibu, wakamwuliza, Wapi, Bwana? Akawaambia, Ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai.[#Ayu 39:30; Mt 24:28]