Luka 19

Luka 19

Yesu na Zakayo

1Naye alipoingia Yeriko alipita katikati yake.

2Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri.

3Huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo.

4Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile.

5Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako.

6Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha.

7Hata watu walipoona, walinung'unika wote, wakisema, Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi.[#Lk 15:2]

8Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne.[#Kut 22:1; Hes 5:6,7]

9Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Abrahamu.[#Lk 13:16; Mdo 3:25; 16:31]

10Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.[#Mt 18:11; Eze 34:16; Yn 3:17; Lk 5:32; 1 Tim 1:15]

Mfano wa mafungu kumi ya fedha

11Waliposikia hayo, aliongeza kusema mfano, kwa sababu alikuwa karibu na Yerusalemu, na wao walidhani ya kuwa ufalme wa Mungu utaonekana mara moja.[#Mt 25:14-30; #Lk 24:21; Mdo 1:6]

12Basi akasema, Mtu mmoja, kabaila, alisafiri kwenda nchi ya mbali, ili ajipatie ufalme na kurudi.[#Mk 13:34]

13Akaita watu kumi katika watumwa wake, akawapa mafungu kumi ya fedha, akawaambia, Fanyeni biashara hadi nitakaporudi.

14Lakini watu wa mji wake walimchukia, wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki huyu atutawale.[#Yn 1:11]

15Ikawa aliporudi, ameupata ufalme wake, aliamuru waitwe wale watumwa aliowapa fedha, ili ajue faida aliyopata kila mtu kwa biashara yake.

16Akaja wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi.

17Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi.[#Lk 16:10]

18Akaja wa pili, akasema, Bwana, fungu lako limeleta mafungu matano faida.

19Akamwambia huyu naye, Wewe uwe juu ya miji mitano.

20Akaja mwingine akasema, Bwana, hili ndilo fungu lako, ambalo nililiweka salama katika kitambaa.

21Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; wachukua usichoweka, wavuna usichopanda.

22Akamwambia, Nitakuhukumu kwa kinywa chako, mtumwa mwovu wewe. Ulinijua kuwa ni mtu mgumu, nichukuaye nisichoweka, na kuvuna nisichopanda;

23basi, mbona hukuiweka fedha yangu kwa watoao riba, ili nijapo niipate pamoja na faida yake?

24Akawaambia waliosimama karibu, Mnyang'anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi.

25Wakamwambia, Bwana, anayo mafungu kumi.

26Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang'anywa hata alicho nacho.[#Mt 13:12; Mk 4:25; Lk 8:18]

27Tena, wale adui zangu, wasiotaka niwatawale, waleteni hapa muwachinje mbele yangu.

Yesu aingia Yerusalemu kwa shangwe

28Na alipokwisha kusema hayo, alitangulia mbele akipanda kwenda Yerusalemu.

29Ikawa alipokaribia Bethfage na Bethania, kwenye mlima uitwao wa Mizeituni, alituma wawili katika wale wanafunzi,[#Mt 21:1-9; Mk 11:1-10; Yn 12:12-16]

30akisema, Nendeni mpaka katika kijiji kile kinachowakabili, na mtakapoingia ndani mtaona mwanapunda, amefungwa, ambaye hajapandwa na mtu yeyote bado, mfungueni mkamlete hapa.

31Na kama mtu akiwauliza, Mbona mnamfungua? Semeni hivi, Bwana anamhitaji.

32Na wale waliotumwa wakaenda wakaona kama alivyowaambia.

33Na walipokuwa wakimfungua mwanapunda, wenyewe waliwaambia, Mbona mnamfungua mwanapunda?

34Wakasema, Bwana anamhitaji.

35Wakampeleka kwa Yesu, wakatandika nguo zao juu ya mwanapunda, wakampandisha Yesu.

36Na alipokuwa akienda walitandaza nguo zao njiani.[#2 Fal 9:13]

37Na alipokuwa amekaribia mteremko wa mlima wa Mizeituni, kundi zima la wanafunzi wake walianza kufurahi na kumsifu Mungu kwa sauti kuu, kwa ajili ya matendo yote ya uwezo waliyoyaona,

38wakasema, Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; amani mbinguni, na utukufu huko juu.[#Zab 118:26; Lk 2:14]

39Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa katika mkutano wakamwambia, Mwalimu, uwakanye wanafunzi wako.

40Akajibu, akasema, Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, mawe yatanena kwa sauti kuu.

Yesu aulilia Yerusalemu

41Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia,[#2 Fal 8:11; Yn 11:35]

42akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako.[#Kum 32:29; Mt 13:14; Yn 12:38]

43Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote;

44watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiwa kwako.[#Lk 21:6; Zab 137:9]

Yesu atakasa hekalu

45Akaingia hekaluni, akaanza kuwatoa wale waliokuwa wakifanya biashara,[#Mt 21:12-16; Mk 11:15-18; Yn 2:13-16]

46akiwaambia, Imeandikwa, Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi.[#Isa 56:7; Yer 7:11]

47Naye akawa akifundisha kila siku hekaluni. Lakini wakuu wa makuhani, na waandishi, na wakuu wa watu walikuwa wakitafuta njia ya kumwangamiza;[#Lk 21:37; 22:53; Yn 18:20]

48wasione la kutenda, kwa kuwa watu wote walikuwa wakiandamana naye, wakimsikiliza.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya