Luka 23

Luka 23

Yesu mbele ya Pilato

1Kisha mkutano wote wakasimama, wakampeleka kwa Pilato.[#Mt 27:2,11-31; Mk 15:1-20; Yn 18:28—19:16; #Lk 20:25]

2Wakaanza kumshitaki, wakisema, Tumemwona huyu akipotosha taifa letu, na kuwazuia watu wasimpe Kaisari kodi, akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo, mfalme.

3Pilato akamwuliza, akisema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu akamwambia, Wewe wasema.[#1 Tim 6:13]

4Pilato akawaambia wakuu wa makuhani na mkutano, Sioni neno lililo ovu katika mtu huyu.

5Nao walisisitiza sana, wakisema, Huwataharakisha watu, akifundisha katika Yudea yote, tokea Galilaya mpaka huku.

Yesu mbele ya Herode

6Pilato aliposikia hayo aliuliza kama huyu ni mtu wa Galilaya.

7Na alipopata habari ya kuwa yu chini ya mamlaka ya Herode, alimpeleka kwa Herode, kwa kuwa yeye naye alikuwapo Yerusalemu siku zile.[#Lk 3:1]

8Herode alipomwona Yesu alifurahi sana, kwa sababu alikuwa akitaka sana kumwona tangu siku nyingi, maana amesikia habari zake, akatarajia kuona ishara iliyofanywa na yeye.[#Lk 9:9]

9Akamwuliza maneno mengi, yeye asimjibu lolote.

10Wakuu wa makuhani na waandishi wakasimama wakamshitaki kwa nguvu sana.

11Basi Herode akamdhalilisha, pamoja na askari wake, akamdhihaki, na kumvika mavazi mazuri; kisha akamrudisha kwa Pilato.

12Basi siku ile ile Herode na Pilato walipatana kwa urafiki kwa maana hapo kwanza walikuwa na uadui wao kwa wao.

Yesu ahukumiwa Kifo

13Na Pilato akawakutanisha wakuu wa makuhani, na wakubwa, na watu,

14akawaambia, Mtu huyu mmemleta kwangu kana kwamba anapotosha watu; nami, tazama, nimeamua mambo yake mbele yenu, ila sikuona kwake kosa lolote katika mambo hayo mliyomshitaki;

15wala hata Herode, kwa maana amemrudisha kwetu; basi tazama, hakuna neno lolote alilolitenda lipasalo kufa.

16Kwa hiyo nitamrudi, kisha nitamfungua. [

17Maana ilimlazimu kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa sikukuu.]

18Wakapiga kelele wote pamoja, wakisema, Mwondoe huyu, utufungulie Baraba.

19Naye ni mtu aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina iliyotokea mjini, na kwa uuaji

20Basi Pilato alisema nao mara ya pili, kwa vile alivyotaka kumfungua Yesu.

21Lakini wakapiga kelele, wakisema, Msulubishe. Msulubishe.

22Akawaambia mara ya tatu, Kwa sababu gani? Huyu ametenda uovu gani? Sikuona kwake hata neno lipasalo kufa. Basi nikiisha kumrudi nitamfungua.

23Lakini wakatoa sauti zao kwa nguvu sana, wakitaka asulubiwe. Sauti zao zikashinda.

24Pilato akahukumu kwamba haja yao ifanyike.

25Akamfungua yule aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina na uuaji, yule waliyemtaka, akamtoa Yesu wamfanyie watakavyo.

Kusulubiwa kwa Yesu

26Na walipokuwa wakimwondoa walimkamata mtu mmoja, Simoni Mkirene, aliyekuwa ametoka shambani, wakamtwika msalaba, auchukue nyuma yake Yesu.[#Mt 27:32; Mk 15:21]

27Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea.

28Yesu akawageukia, akasema, Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu.

29Kwa maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri walio tasa, na matumbo yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha.[#Lk 21:23]

30Ndipo watakapoanza kuiambia milima, Tuangukieni, na vilima, Tufunikeni.[#Hos 10:8; Ufu 6:16; 9:6]

31Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?[#1 Pet 4:17]

32Wakapelekwa na wawili wengine, wahalifu, wauawe pamoja naye.

33Na walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, ndipo walipomsulubisha yeye, na wale wahalifu, mmoja upande wa kulia, na mmoja upande wa kushoto.[#Mt 27:33-56; Mk 15:22-41; Yn 19:17-30]

34Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura.[#Zab 22:18; Mt 5:44; Isa 53:12]

35Watu wakasimama wakitazama. Wale wakuu nao walikuwa wakimfanyia mzaha, wakisema, Aliokoa wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake.[#Zab 22:7]

36Wale askari nao wakamfanyia dhihaka, wakimwendea na kumletea siki,[#Zab 69:21]

37huku wakisema, Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe.

38Na juu yake palikuwa na anwani; HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI.

39Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi.

40Lakini yule wa pili akamjibu akamkemea, akisema, Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo?

41Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lolote lisilofaa.

42Kisha akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.[#Mt 16:28]

43Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi.

Kifo cha Yesu

44Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hadi saa tisa,[#Amo 8:9]

45jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati.[#Kut 26:31-33; 36:35; Amo 9:1]

46Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.[#Zab 31:5; Mdo 7:59]

47Alipokwisha kusema hayo alikata roho. Yule jemadari alipoona yaliyotukia, alimtukuza Mungu, akisema, Hakika yake, mtu huyu alikuwa mwenye haki.

48Na makutano yote ya watu waliokuwa wamekutanika kutazama mambo hayo, walipoona yaliyotendeka, wakaenda zao kwao, wakijipigapiga vifua.

49Na wote waliojuana naye, na wale wanawake walioandamana naye toka Galilaya, wakasimama kwa mbali, wakitazama mambo hayo.[#Lk 8:2-3; Zab 38:11; 88:8]

Kuzikwa kwa Yesu

50Na tazama, akatoka mtu mmoja, jina lake Yusufu, ambaye ni mtu wa baraza, mtu mwema, mwenye haki;[#Mt 27:57-61; Mk 15:42-47; Yn 19:38-42]

51(wala hakulikubali shauri na tendo lao), naye ni mtu wa Arimathaya, mji mmoja wa Wayahudi, tena anautazamia ufalme wa Mungu;[#Lk 2:25,38]

52mtu huyo alikwenda kwa Pilato, akataka kupewa mwili wa Yesu.

53Akaushusha, akauzinga sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililochongwa mwambani, ambalo hajalazwa mtu bado ndani yake.

54Na siku ile ilikuwa siku ya Maandalio, na sabato ikaanza kuingia.

55Na wale wanawake waliokuja naye toka Galilaya walifuata, wakaliona kaburi, na jinsi mwili wake ulivyowekwa.

56Wakarudi, wakatayarisha manukato na marhamu. Na siku ya sabato walistarehe kama ilivyoamriwa.[#Kut 12:16; 20:10; Kum 5:14; Law 23:8]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya