Mathayo 10

Mathayo 10

Wanafunzi kumi na wawili

1Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina.[#Mk 6:7-13; Lk 9:1-5]

2Na majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya; Wa kwanza Simoni aliyeitwa Petro, na Andrea nduguye; Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye;[#Mk 3:14-19; Lk 6:13-16; Yn 1:40-49]

3Filipo, na Bartholomayo; Tomaso, na Mathayo mtoza ushuru; Yakobo wa Alfayo, na Thadayo;

4Simoni Mkananayo, na Yuda Iskarioti, naye ndiye aliyemsaliti.

Wajibu wa hao kumi na wawili

5Hao Kumi na Wawili Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema, Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wowote wa Wasamaria msiingie.

6Bali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.[#Mt 15:24; Mdo 13:46; Yer 50:6]

7Na katika kuenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia.[#Lk 10:4-12; #Mt 4:17; Lk 10:9]

8Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.[#Mdo 20:33]

9Msichukue dhahabu, wala fedha, wala pesa mishipini mwenu;

10wala mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; maana mfanyakazi astahili posho yake.[#1 Kor 9:14; 1 Tim 5:18; Lk 10:4; Hes 18:31]

11Na mji wowote au kijiji chochote mtakachoingia, tafuteni ni nani humo aliye mtu mwaminifu; mkae kwake hadi mtakapotoka.

12Nanyi mkiingia katika nyumba isalimuni.[#Lk 10:5,6]

13Na nyumba ile ikistahili, amani yenu na iifikie; la, kwamba haistahili, amani yenu na iwarudie ninyi.

14Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kung'uteni mavumbi ya miguuni mwenu.[#Mdo 13:51; 18:6; Lk 10:10-12]

15Amin, nawaambia, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma na Gomora kustahimili adhabu ya siku ya hukumu, kuliko mji ule.[#Mt 11:24; Mwa 19:24-28; Lk 20:47]

Mateso yajayo

16Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwamwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua.[#Lk 10:3; Yn 10:12; Mdo 20:29; Rum 16:19; Efe 5:15]

17Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga;[#Mk 13:9-11; Lk 12:11-12; 21:12-15; #Mt 24:9]

18nanyi mtachukuliwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa.[#Mt 24:14; Mdo 25:23; 27:24]

19Lakini hapo watakapowapeleka, msifikirifikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema.[#Lk 12:11,12]

20Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu.[#Yn 14:26; 1 Kor 2:4]

21Na ndugu atamsaliti nduguye ili auawe, na baba atamsaliti mwana, na wana watawainukia wazazi wao, na kuwaua.[#Mk 13:12; Lk 21:16; Mt 10:35; Mik 7:6]

22Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.[#Mt 24:9,13; Mk 13:13; Lk 21:17; Yn 15:21]

23Lakini watakapowafukuza katika mji huu, kimbilieni mwingine; kwa maana ni kweli nawaambia, Hamtaimaliza miji ya Israeli, hata ajapo Mwana wa Adamu.[#Mt 16:28]

24Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, wala mtumwa hampiti bwana wake.[#Lk 6:40; Yn 13:16; 15:20]

25Yamtosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumwa kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mwenye nyumba Beelzebuli, je! Si zaidi wale walio wa nyumbani mwake?[#Mt 9:34; 12:24; Mk 3:22; Lk 11:15]

Astahiliye kuogopewa

26Basi, msiwaogope, kwa maana hakuna neno lililositirika, ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa, ambalo halitajulikana.[#Lk 12:2-9; #Mk 4:22; Lk 8:17]

27Niwaambialo ninyi katika giza, lisemeni katika nuru; na msikialo kwa siri, lihubirini juu ya nyumba.

28Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika Jehanamu.[#Yak 4:12]

29Je! Mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja? Wala hata mmoja haanguki chini asipojua Baba yenu;

30lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote.

31Msiogope basi; bora ninyi kuliko mashomoro wengi.[#Mt 12:12]

32Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni.

33Bali mtu yeyote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.[#2 Tim 2:12; Lk 9:26]

Si Amani, bali upanga

34Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! Sikuja kuleta amani, bali upanga.[#Lk 12:51-53]

35Kwa maana nilikuja kumfitini mtu na babaye, na binti na mamaye, na mkwe na mkwe mtu;[#Mik 7:6]

36na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake.

37Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili.[#Kum 33:9; Lk 14:26,27]

38Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili.[#Mt 16:24; Mk 8:34; Lk 9:23]

39Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona.[#Mt 16:25; Mk 8:35; Lk 9:24; 17:33; Yn 12:25]

Thawabu

40Awapokeaye ninyi, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi, ampokea yeye aliyenituma.[#Mk 9:37; Lk 9:48; 10:16; Yn 12:44; 13:20; Mt 18:5]

41Ampokeaye nabii kwa kuwa ni nabii, atapata thawabu ya nabii; naye ampokeaye mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki, atapata thawabu ya mwenye haki.

42Na mtu awaye yote atakayemnywesha mmojawapo wa wadogo hawa angaa kikombe cha maji baridi, kwa kuwa ni mwanafunzi, amin, nawaambia, haitampotea kamwe thawabu yake.[#Mt 25:40; Mk 9:41]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya