The chat will start when you send the first message.
1Wakati ule mfalme Herode alisikia habari za Yesu, akawaambia watumishi wake,[#Mk 6:14,17-30; Lk 9:7-9; #Lk 3:19,20]
2Huyo ndiye Yohana Mbatizaji; amefufuka katika wafu; na kwa hiyo nguvu hizo zinatenda kazi ndani yake.
3Maana Herode alikuwa amemkamata Yohana, akamfunga, akamtia gerezani, kwa ajili ya Herodia, mke wa Filipo nduguye.[#Lk 3:19-20; Mt 11:2]
4Kwa sababu Yohana alimwambia, Si halali kwako kuwa naye.[#Law 18:16; 20:21]
5Naye alipotaka kumwua, aliwaogopa watu, maana walimwona Yohana kuwa nabii.[#Mt 21:26]
6Hata ilipofika sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti ya Herodia alicheza mbele ya watu, akampendeza Herode.
7Hata akaahidi kwa kiapo ya kwamba atampa lolote atakaloliomba.
8Naye, huku akichochewa na mamaye, akasema, Nipe hapa katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji.
9Naye mfalme akasikitika; lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya wale walioketi karamuni pamoja naye, akaamuru apewe;
10akatuma mtu, akamkata kichwa Yohana mle gerezani.[#Mt 17:12]
11Kichwa chake kikaletwa katika kombe, akapewa yule msichana; akakileta kwa mamaye.
12Wanafunzi wake wakaenda, wakamchukua yule maiti, wakamzika; kisha wakaenda wakampasha Yesu habari.
13Naye Yesu aliposikia hayo, aliondoka huko katika mashua, akaenda mahali pasipo watu, faraghani. Na makutano waliposikia, walimfuata kwa miguu kutoka mijini mwao.[#Mk 6:31-44; Lk 9:10-17; Yn 6:1-13]
14Yesu akatoka, akaona mkutano mkuu, akawahurumia, akawaponya wagonjwa wao.[#Mt 9:36]
15Hata kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na saa imekwisha pita; uwaage makutano, waende zao vijijini, wakajinunulie vyakula.
16Yesu akawaambia, Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi vyakula.
17Wakamwambia, Hamna kitu hapa ila mikate mitano na samaki wawili.
18Akasema, Nileteeni hapa.
19Akawaagiza makutano waketi katika majani; akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akabariki, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi, wanafunzi wakawapa makutano.
20Wakala wote wakashiba; wakayaokota mabaki ya vipande vya mikate, vikapu kumi na viwili, vimejaa.[#2 Fal 4:44]
21Nao waliokula walikuwa wanaume wapatao elfu tano, bila kuhesabu wanawake na watoto.
22Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande katika mashua na kutangulia mbele yake kwenda ng'ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano.[#Mk 6:45-56; Yn 6:15-21]
23Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake.[#Lk 6:12; 9:18]
24Na ile mashua imekwisha kufika katikati ya bahari, inapigwa sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa unawakabili.
25Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari.
26Wanafunzi walipomwona akitembea juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni mzimu; wakapiga yowe kwa hofu.[#Lk 24:37]
27Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo, ni mimi; msiogope.
28Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji.
29Akasema, Njoo. Petro akashuka katika mashua, akatembea juu ya maji, ili kumwendea Yesu.
30Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe.
31Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka?[#Mt 8:26]
32Nao walipopanda katika mashua, upepo ulikoma.
33Nao waliokuwamo ndani ya mashua wakamsujudia, wakisema, Hakika wewe u Mwana wa Mungu.
34Na walipokwisha kuvuka, walifika nchi ya Genesareti.
35Na watu wa mahali pale walipomtambua, walituma watu kwenda nchi zile zilizo kandokando, wakamletea wote waliokuwa wagonjwa;
36nao wakamsihi waguse hata pindo la vazi lake tu; na wote waliogusa wakaponywa kabisa.[#Mt 9:21; Lk 6:19]