Mathayo 20

Mathayo 20

Wafanya kazi katika shamba la mizabibu

1Kwa maana ufalme wa mbinguni unafanana na mtu aliyetoka alfajiri kwenda kuwaajiri wafanya kazi awapeleke katika shamba lake la mizabibu.[#Mt 21:33]

2Naye alipokwisha kupatana na wafanya kazi kuwapa kutwa dinari, aliwapeleka katika shamba lake la mizabibu.

3Akatoka mnamo saa tatu, akaona wengine wamesimama sokoni wasiokuwa na kazi;

4na hao nao akawaambia, Nendeni nanyi pia katika shamba langu la mizabibu, na iliyo haki nitawapa. Wakaenda.

5Akatoka tena mnamo saa sita na saa tisa, akafanya vile vile.

6Hata kama saa kumi na moja akatoka, akakuta wengine wamesimama, akawaambia, Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi?

7Wakamwambia, Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri. Akawaambia, nanyi pia nendeni katika shamba la mizabibu.

8Kulipokuchwa, yule bwana wa shamba akamwambia msimamizi wake, Waite wafanya kazi, uwalipe ujira wao, ukianzia wa mwisho hadi wa kwanza.[#Law 19:13; Kum 24:15]

9Na walipokuja wale wa saa kumi na moja, walipokea kila mtu dinari.

10Na wale wa kwanza walipokuja, walidhani kwamba watapokea zaidi; na hao pia wakapokea kila mtu dinari.

11Basi wakiisha kuipokea, wakamnung'unikia mwenye nyumba,

12wakisema, Hao wa mwisho wamefanya kazi saa moja tu, nawe umewasawazisha na sisi tuliostahimili taabu na joto la mchana kutwa.

13Naye akamjibu mmoja wao, akamwambia, Rafiki, sikudhulumu; hukupatana nami kwa dinari?

14Chukua iliyo yako, uende zako; napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe.

15Si halali yangu kutumia vilivyo vyangu kama nipendavyo? Au jicho lako limekuwa ovu kwa sababu ya mimi kuwa mwema?[#Rum 9:16,21; Mt 6:23]

16Vivyo hivyo wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho.[#Mt 19:30; Mk 10:31; Lk 13:30]

Yesu asema juu ya kifo chake na kufufuka kwake

17Yesu alipokuwa akipanda kwenda Yerusalemu, aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani; na njiani akawaambia,[#Mk 10:32-34; Lk 18:31-33]

18Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu; na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi; nao watamhukumu afe;[#Mt 16:21; 17:22,23]

19kisha watampeleka kwa Mataifa wapate kumdhihaki, na kumpiga mijeledi, na kumsulubisha; na siku ya tatu atafufuka.

Ombi la mama wa Yakobo na Yohana

20Ndipo mama yao wana wa Zebedayo akamwendea pamoja na wanawe, akamsujudia, na kumwomba kitu.[#Mk 10:35-45; #Mt 10:2]

21Akamwambia, Wataka nini? Akamwambia, Agiza kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wako wa kulia, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako.[#Mt 19:28]

22Yesu akajibu akasema, Hamjui mnaloliomba. Je! Mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi? Wakamwambia, Twaweza.[#Mt 26:39; Yn 18:11; Lk 12:50]

23Akawaambia, Hakika mtakinywea kikombe changu; lakini kuketi mkono wangu wa kulia na mkono wangu wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu.

24Na wale kumi waliposikia, waliwakasirikia wale ndugu wawili.[#Lk 22:24-26]

25Lakini Yesu akawaita, akasema, Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha.[#Lk 22:25-26]

26Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu yeyote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu;[#Mt 23:11; Mk 9:35; Lk 22:26]

27na mtu yeyote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu;

28kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.[#Lk 22:27; Flp 2:7; 1 Tim 2:6]

Yesu aponya vipofu wawili

29Walipokuwa wakitoka Yeriko mkutano mkubwa wakamfuata.[#Mk 10:46-52; Lk 18:35-43]

30Na tazama, vipofu wawili walikuwa wameketi kando ya njia, nao waliposikia ya kwamba Yesu anapita, walipaza sauti, wakisema, Uturehemu, Bwana, mwana wa Daudi![#Mt 15:22]

31Mkutano wakawakaripia, wanyamaze. Lakini wao wakazidi kupaza sauti, wakisema, Uturehemu, Bwana, mwana wa Daudi!

32Yesu akasimama, akawaita, akasema, Mnataka niwafanyie nini?

33Wakamwambia, Bwana, twataka macho yetu yafumbuliwe.

34Yesu akawahurumia, akawagusa macho yao; mara wakapata kuona, wakamfuata.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya