Mathayo 4

Mathayo 4

Majaribu ya Yesu

1Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ili ajaribiwe na Ibilisi.[#Mk 1:12,13; Lk 4:1-13; #Ebr 2:18; 4:15]

2Akafunga siku arubaini mchana na usiku, mwishowe akaona njaa.[#Kut 34:28; 1 Fal 19:8]

3Mjaribu akamjia akamwambia, Ikiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mikate.[#Mwa 3:1-7]

4Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.[#Kum 8:3]

5Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha hekalu,[#Mt 27:53]

6akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini; kwa maana imeandikwa,[#Zab 91:11-12]

Atakuagizia malaika zake;

Na mikononi mwao watakuchukua;

Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.

7Yesu akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako.[#Kum 6:16]

8Kisha Ibilisi akamchukua mpaka katika mlima mrefu mno, akamwonesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake,

9akamwambia, Haya yote nitakupa, ukiinama na kunisujudia.

10Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Mwabudu Bwana Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake.[#Kum 6:13]

11Kisha Ibilisi akamwacha; na tazama, wakaja malaika wakamtumikia.[#Yn 1:51; Ebr 1:6,14]

Yesu aanza huduma yake katika Galilaya

12Basi Yesu aliposikia ya kwamba Yohana amefungwa, alikwenda zake mpaka Galilaya;[#Mk 1:14,15; Lk 4:14,15; #Mt 14:3; Mk 6:17; Lk 3:19-20]

13akatoka Nazareti, akaja akakaa Kapernaumu, mji ulioko pwani, mipakani mwa Zabuloni na Naftali;[#Yn 2:12]

14ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema,[#Isa 9:1-2]

15Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali,[#Isa 9:1-2]

Njia ya bahari, ng'ambo ya Yordani,

Galilaya ya mataifa,

16Watu wale waliokaa katika giza

Wameona mwanga mkuu,

Nao waliokaa katika nchi na uvuli wa mauti

Mwanga umewazukia.

17Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.[#Mt 3:2]

Yesu awaita wanafunzi wa kwanza

18Naye alipokuwa akitembea kando ya bahari ya Galilaya, aliona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi.[#Mk 1:16-20; Lk 5:1-11; #Yn 1:40]

19Akawaambia, Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.[#Mt 13:47; Eze 47:10]

20Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.[#Mt 19:27]

21Alipoendelea, akaona ndugu wengine wawili, Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye, ambao walikuwa katika mashua pamoja na Zebedayo baba yao, wakizitengeneza nyavu zao; akawaita.

22Mara wakaiacha mashua na baba yao, wakamfuata.

Yesu awahudumia makundi ya watu

23Naye alikuwa akizunguka katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari Njema ya ufalme, na kuponya kila ugonjwa na maradhi ya kila namna waliyokuwa nayo watu.[#Mt 9:35; Mk 1:39; Lk 4:15,44; Mdo 10:38]

24Na habari zake zikaenea katika Shamu yote; wakamletea wote waliokuwa wagonjwa, walioshikwa na maradhi mbalimbali na mateso, wenye pepo, na wenye kifafa, na wenye kupooza; akawaponya.[#Mk 6:55]

25Na makutano mengi wakamfuata, kutoka Galilaya, na Dekapoli, na Yerusalemu, na Yudea, na ng'ambo ya Yordani.[#Mk 3:7,8; Lk 6:17-19]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya