Mika 2

Mika 2

Maovu ya jamii yashutumiwa

1Ole wao wakusudiao mambo maovu, na kutenda mabaya vitandani mwao! Kunapopambazuka asubuhi huyafanya, sababu wana uwezo mikononi mwao.[#Est 3:8,9; Isa 32:7; Zab 7:11-14; 36:4; Hos 7:6; Mwa 31:29]

2Nao hutamani mashamba, na kuyanyakua; na nyumba pia, nao huzichukua; nao humwonea mtu na nyumba yake, naam, mtu na urithi wake.

3Basi BWANA asema hivi, Angalia, nakusudia jambo baya juu ya jamaa hii, ambalo hamtazitoa shingo zenu, wala hamtakwenda kwa kiburi; kwa maana ni wakati mbaya.[#Yer 8:3]

4Siku hiyo watatunga mithali juu yenu, na kuomboleza kwa maombolezo ya huzuni nyingi, na kusema,

Sisi tumeangamizwa kabisa;

Yeye analibadili fungu la watu wangu;

Jinsi anavyoniondolea hilo!

Awagawia waasi mashamba yetu.

5Kwa hiyo hamtakuwa na mtu atakayeitupa kamba kwa kura katika mkutano wa BWANA.[#Kum 32:8,9]

6Msitabiri, ndivyo watabirivyo; wasiyatabiri mambo haya; lawama hazikomi.

7Je! Litasemwa neno hili, enyi nyumba ya Yakobo, Roho ya BWANA imepunguzwa? Je! Haya ni matendo yake? Je! Maneno yangu hayamfai yeye aendaye kwa unyofu?

8Lakini siku hizi mmeinuka kama adui za watu wangu; mnawapokonya joho lililo juu ya nguo za hao wapitao salama bila kutarajia vita.

9Wanawake wa watu wangu mnawatupa nje ya nyumba zao nzuri; watoto wao wachanga mnawanyang'anya utukufu wangu milele.

10Ondokeni, mwende zenu; maana hapa sipo mahali pa raha yenu; kwa sababu ya uchafu mtaangamizwa, naam, kwa maangamizo makubwa sana.[#Kum 12:9]

11Mtu akienda kwa roho ya uongo, akinena maneno ya uongo, akisema, Nitakutabiria habari ya mvinyo na kileo; mtu huyu atakuwa nabii wao watu hawa.

Ahadi kwa mabaki wa Israeli

12Hakika nitakukusanya, Ee Yakobo, nyote pia;[#Isa 11:11; Mik 4:6,7; Sef 3:19]

Bila shaka nitawakusanya waliobaki wa Israeli;

Nitawaweka pamoja kama kondoo katika zizi;

Kama kundi la kondoo katika malisho yao;

Watafanya mvumo kwa wingi wa watu;

13Avunjaye amekwea juu mbele yao;

Wamebomoa mahali, wakapita mpaka langoni,

Wakatoka nje huko;

Mfalme wao naye amepita akiwatangulia,

Naye BWANA ametangulia mbele yao.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya