Mika 4

Mika 4

Amani na usalama kwa kutii

1Lakini itakuwa katika siku za mwisho, ya kwamba mlima wa nyumba ya BWANA utawekwa imara juu ya milima, nao utainuliwa juu ya vilima; na watu wa mataifa watauendea makundi makundi.[#Isa 2:2; Eze 17:22; Dan 2:44]

2Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njooni, twende juu mlimani kwa BWANA, na nyumbani kwa Mungu wa Yakobo; naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake; kwa maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la BWANA litatoka Yerusalemu.[#Yn 6:45]

3Naye atafanya hukumu kati ya watu wa kabila nyingi, naye atawakemea mataifa wenye nguvu walio mbali; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe.[#Isa 2:4; Hos 2:18; Zab 72:7; Lk 1:33; Yoe 3:10]

4Bali wataketi kila mtu chini ya mzabibu wake, na chini ya mtini wake; wala hapana mtu atakayewatia hofu; kwa kuwa kinywa cha BWANA wa majeshi kimesema hivi.[#1 Fal 4:25; Isa 36:16; Yer 31:10; Zek 3:10]

5Kwa maana mataifa yote watakwenda, kila moja kwa jina la mungu wake, na sisi tutakwenda kwa jina la BWANA, Mungu wetu, milele na milele.[#Yer 2:11; Kut 3:14,15]

Ahadi ya kurudishwa baada ya uhamisho

6Katika siku ile, asema BWANA, nitamkusanya yeye achechemeaye, nami nitamrudisha yeye aliyefukuzwa, na yeye niliyemtesa.[#Isa 56:8; Yer 3:18; Eze 34:13,16; Sef 3:19; Zab 147:2]

7Nami nitamfanya yeye aliyechechemea kuwa mabaki, na yeye aliyetupwa mbali kuwa taifa lenye nguvu, na BWANA atawamiliki katika mlima Sayuni tangu sasa na hata milele.[#Isa 9:6; Dan 7:14; Lk 1:33; Ufu 11:15]

8Na wewe, Ee mnara wa kundi, kilima cha binti Sayuni, utajiliwa; naam, mamlaka ya kwanza yatakuja, ufalme wa binti Yerusalemu.

9Sasa mbona unapiga kelele? Je! Hakuna mfalme kwako, mshauri wako amepotea, hata umeshikwa na uchungu kama mwanamke wakati wa kuzaa?

10Uwe na uchungu, utaabike ili uzae, Ee binti Sayuni, kama mwanamke mwenye uchungu; maana sasa utatoka mjini, nawe utakaa katika mashamba; utafika hata Babeli; huko ndiko utakakookolewa; huko ndiko BWANA atakakokukomboa kutoka kwa mikono ya adui zako.

11Na sasa mataifa mengi wamekusanyika juu yako, wasemao, Na atiwe unajisi; macho yetu na yaone shari ya Sayuni.

12Lakini wao hawayajui mawazo ya BWANA, wala hawafahamu shauri lake; kwamba amewakusanya kama miganda mahali pa kupuria.

13Haya, simama upure, Ee binti Sayuni; kwa maana nitafanya pembe yako kuwa chuma, na kwato zako kuwa shaba; nawe utapondaponda mataifa mengi, na faida yao utaiweka wakfu kwa BWANA, na mali zao kwa BWANA wa dunia yote.[#Ufu 21:24]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya